Feb 03, 2023 03:05 UTC
  • Ijumaa, tarehe 3 Februari, 2023

Leo ni Ijumaa tarehe 12 mwezi Rajab 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe 3 Februari 2023.

Siku kama ya leo miaka 1412 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria alifariki dunia Abbas bin Abdul Muttalib, ami yake Bwana Mtume SAW na mmoja wa shakhsia wakubwa wa Kikuraishi.

Alijulikana kwa tabia njema, mwenendo mzuri, busara na maarifa ya hali ya juu. Baadhi ya wanahistoria wanaamini kwamba, Abbas bin Abdul Muttalib aliukubali Uislamu kwa siri kabla ya Bwana Mtume kuhamia Madina na alikuwa akimpelekea Mtume habari za harakati za washirikina mjini Makka.

Mwaka wa 8 Hijria Abbas bin Abdul Muttalib aliungana na Waislamu na baada ya Fat'hu Makka aliteuliwa na Bwana Mtume kuchukua jukumu la kutoa huduma ya maji kwa watu wanaozuru Nyumba ya Mwenyezi Mungu, al-Kaaba. 

Katika siku kama ya leo miaka 555 iliyopita, alifariki dunia mvumbuzi wa mashine ya uchapishaji, Johannes Gutenberg.

Mvumbuzi huyo alizaliwa nchini Ujerumani lakini alihamia Strasbourg, Ufaransa na akaanza kujishughulisha na kazi za kiufundi.

Mwaka 1443 au 1444 Gutenberg alifanikiwa kutengeneza mashine ya uchapishaji na kupiga hatua muhimu katika uchapishaji na uenezaji wa elimu na maarifa kati ya wanadamu. Katika zama zake, Johannes Gutenberg pia alichapisha kitabu cha Biblia maarufu kwa jina la' Gutenberg Bible.'

Johannes Gutenberg

Miaka 193 iliyopita katika siku kama ya leo, Ugiriki ilipata uhuru wake kutoka kwa utawala wa Othmania.

Ugiriki ambayo kijiografia ipo kusini mashariki mwa Ulaya ni moja kati ya nchi zenye tamaduni kongwe duniani. Mwaka 338 kabla ya kuzaliwa Nabii Isa (a.s), mfalme wa Macedonia aliivamia Ugiriki na karne moja baadaye nchi hiyo ikawa chini ya mamlaka ya utawala wa Roma na baadaye Roma ya Mashariki. 

Katika kipicdi chote cha karne ya 19, Ugiriki ilishuhudia mapigano vita na vurugu za ndani na nje. Hatimaye katika siku kama ya leo nchi hiyo ikajipatia uhuru.

Siku kama ya leo miaka 108 iliyopita, mfereji wa Suez uliokuwa ukidhibitiwa na Uingereza, ulishambuliwa na vikosi vya majeshi ya Ujerumani na utawala wa Othmaniya katika Vita vya Kwanza vya Dunia.

Udhibiti wa mfereji huo wa Suez ulikuwa na umuhimu mkubwa kwa pande mbili zilizokuwa zikipigana katika Vita vya Kwanza vya Dunia kutokana na ukweli kwamba, mfereji huo ndio unaounganisha Bahari ya Mediterania na Bahari Nyekundu.

Uingereza ambayo haikuwa tayari kupoteza makoloni yake ya Asia, ilipigana vikali na majeshi ya Ujerumani na utawala wa Othmaniya na kupata ushindi.

Mfereji wa Suez uliendelea kudhibitiwa na Uingereza hadi ulipotaifishwa na kiongozi wa Misri Gamal Abdul Nasir hapo mwaka 1956 na kufanywa kuwa mali ya taifa.

Mfereji wa Suez

Katika siku kama ya leo miaka 99 iliyopita, Woodrow Wilson Rais wa 28 wa Marekani alifariki dunia.

Woodrow Wilson alizaliwa 1913 na akiwa na umri wa miaka 57 alichukua hatamu za uongozi wa Rais wa Marekani. Kama walivyokuwa Marais waliomtangulia wa Marekani, na yeye alikita zaidi katika kuingilia masuala ya ndani ya Amerika ya Kati.

Kipindi cha urais wa Woodrow Wilson kilitawaliwa na uingiliaji na uvamizi wa kijeshi dhidi ya maeneo mbalimbali duniani. Nusu ya kipindi cha utawala wa Woodrow Wilson, kilishuhudia Marekani ikishughulishwa na vita. Nchi zilizoshambuliwa kijeshi na Marekani katika uongozi wa Rais Woodrow Wilson ni Haiti, Guatemala, Dominican na Cuba.

Woodrow Wilson

Tarehe 14 Bahman 1357 Hijria Shamsia yaani siku kama hii ya leo miaka 44 iliyopita, wananchi wa Iran walipokuwa katika sherehe na shamrashamra za kurejea nchini Imam Khomeini akitokea uhamishoni nje ya nchi, Imam alizungumza na waandishi habari akieleza misimamo ya mfumo ujao wa utawala wa Kiislamu hapa nchini na kutangaza kuwa ataunda serikali ya mpito ya mapinduzi muda mfupi baadaye.

Imam Khomeini alitangaza kuwa serikali hiyo ya mpito itakuwa na jukumu la kutayarisha kura ya maoni ya Katiba mpya ya Iran. Vile vile alimtahadharisha Shapour Bakhtiar Waziri Mkuu wa serikali ya wakati huo ya Shah kwamba, iwapo ataendelea kuwakandamiza wananchi angetangaza vita vya jihadi. Imam Khomeini vile vile alilitaka jeshi lijiunge na mapambano ya wananchi dhidi ya utawala wa Shah.

Wakati huo pia ilitangazwa kwamba, Wamarekani elfu 35 walikuwa wamekwishaondoka katika ardhi ya Iran na kwamba wengine elfu 10 wako mbioni kuondoka. 

Na miaka 13 iliyopita katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria Shamsia, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilirusha kwa mafanikio roketi ya kwanza ya kupeleka satalaiti angani iliyojulikana kwa jina la Omid.

Miaka iliyofuata Iran ilituma viumbe hai angani kwa mafanikio ikiwa ni pamoja na kobe na tumbili, na hatua hiyo iliingiza Iran katika klabu ya nchi zenye teknolojia ya anga za mbali tena katika kipindi hicho cha vikwazo vikali vya kiuchumi vya nchi za Magharibi.