Alkhamisi, tarehe 9 Februari, 2023
Lo ni Alkhamisi tatrehe 18 Rajab inayosadifiana na tarehe 9 Februari 2023.
Siku kama ya leo miaka 1434 iliyopita alifariki dunia mtoto mdogo wa Mtume wetu Muhammad (saw), Ibrahim akiwa na umri wa miezi 18 tu.
Ibrahim ambaye alifariki dunia kutokana na maradhi alikuwa mtoto pekee wa kiume wa Mtume ambaye hakuzaliwa na Bibi Khadija (as). Mama yake alikuwa Maria al Qibtiyya ambaye alitumwa na mfalme wa Misri ya wakati huo kuwa hadimu na mtumishi wa Mtume na aliolewa na mtukufu huyo baada ya kusilimu.
Kifo cha Ibrahim kilimhuzunisha sana Mtume (saw) kwa sababu mtukufu huyo alikuwa akimpenda sana mtoto huyo.
Tarehe 18 Rajab miaka 1018 iliyopita alifariki dunia Ibn Samh huko katika mji wa mjini Andalucia.
Msomi huyo wa Kiislamu alikuwa mtaalamu wa hesabu, nyota na tabibu. Alizaliwa katika mji wa Cordoba, Andalucia mnamo mwaka 370 Hijiria. Msomi huyu wa Kiislamu alifanya utalii na utafiti mwingi katika elimu za hesabu na nyota, sambamba na kuwalea wanafunzi wa zama zake.
Kuna vitabu kadhaa vilivyoandikwa na Ibn Samh kwa lugha ya Kiarabu na miongoni mwavyo ni pamoja na kitabu kiitwacho "Al Madkhalu Ila al Handasah", "Al Muamalat" na "Kitabuz Ziyj."
Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, yaani tarehe 20 Bahman 1357 Hijiria Shamsia, vibaraka wa gadi ya mfalme Shah wa Iran, walivamia moja ya kambi za kikosi cha Jeshi la Anga mjini Tehran majira ya usiku, baada ya kundi la makamanda wa jeshi hilo kutangaza uungaji mkono wao kwa Mapinduzi ya Kiislamu na utiifu wao kwa Imam Ruhullah Khomeini.
Baada ya kutangazwa habari hiyo, wananchi Waislamu wa Iran kutoka pembe zote za mji wa Tehran walielekea katika kambi ya kikosi cha Jeshi la Anga ili kuwasadia wanajeshi hao ambao walikuwa wakipambana na vibaraka hao wa mfalme Shah.
Licha ya kutokuwa na silaha za maana wananchi hao walifanikiwa kuzima shambulio la vibaraka hao na kwa utaratibu huo, hatua ya mwisho ya kuuangushwa utawala wa Shah nchini Iran ikawa imeanza.
Katika siku kama ya leo miaka 39 iliyopita sawa na tarehe 9 Februari 1984, alifariki dunia Yuri Andropov, mmoja wa viongozi wa Urusi ya zamani.
Andropov ambaye alikuwa mwanasiasa mkubwa wa Urusi ya zamani alizaliwa tarehe 15 Juni 1914 ambapo akiwa kijana alijiunga na harakati za kisiasa na Chama cha Kikomonisti. Mwaka 1953 Yuri Andropov aliteuliwa kuwa balozi wa Urusi ya zamani nchini Hungary ambapo wakati nchi yake ilipoivamia Hungary mwaka 1956, alitwaa uongozi wa operesheni hiyo ya kijeshi dhidi ya nchi hiyo na kutekeleza ukandamizaji na umwagaji damu dhidi ya wapigania uhuru wa Hungary. Mwaka 1967 Yuri Andropov aliteuliwa kuwa mkuu wa shirika la ujasusi la Urusi ya zamani KGB ambapo aliendelea kuliongoza shirika hilo kwa kipindi cha miaka 15 yaani hadi alipofariki dunia Leonid Brezhnev, Kiongozi wa wakati huo wa Urusi ya zamani hapo mwaka 1982.
Miezi saba tangu kiongozi huyo afariki dunia, Andropov aliteuliwa kuwa katibu mkuu wa Chama cha Kikomonisti cha Urusi ya zamani, ambacho ni cheo cha juu kabisa nchini humo.
Aliendelea kusimamia uongozi wa chama hicho kwa kipindi cha miaka 15, hadi alipofariki dunia. Katika kipindi chake kuliongezeka mashindano ya uundaji wa silaha za nyuklia. *
Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, wapiganaji shupavu wa Iran walianzisha operesheni iliyopewa jina la Walfajr 8 kwa kushambulia ngome za jeshi la utawala wa zamani wa Iraq katika eneo la kusini zaidi la mpaka wa nchi mbili hizi.
Maelfu ya wapiganaji wa Iran walivuka Mto Arvand na kufanikiwa kuuteka mji wa Faw unaopatikana kusini mashariki mwa Iraq, katika siku ya kwanza ya operesheni hiyo. Operesheni hiyo ilikuwa ya ghafla na tata kwa upande wa kijeshi na iliwashangaza weledi wa masuala ya kijeshi na kisiasa ulimwenguni na utawala wa zamani wa Iraq.
Operesheni ya Walfajr-8 ilitekelezwa kwa lengo la kuushinikiza utawala wa Saddam uache kuikalia kwa mabavu ardhi ya Iran na kuilipa fidia Tehran kutokana na hasara na maafa yaliyosababishwa na uvamizi wa Iraq.
Na siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, baada ya Chama cha Wokovu wa Kiislamu cha Algeria (FIS) kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa Bunge, wanajeshi waliokuwa wakitawala nchini humo, walibatilisha matokeo ya uchaguzi huo na kukipiga marufuku chama hicho, hali iliyopelekea kuzuka machafuko makubwa.
Machafuko hayo yalipelekea kuuawa watu wengi nchini Algeria.