Apr 29, 2025 02:13 UTC
  • Jumanne, Aprili 29, 2025

Leo ni Jumanne tarehe Mosi Mfunguo Pili Dulqaada 1446 Hijria sawa na Aprili 29 mwaka 2025 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1273 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya kutegemewa, alizaliwa Bibi Fatima Maasuma, binti yake Imam Musa al-Kadhim (as) ambaye ni miongoni mwa wajukuu watukufu wa Bwana Mtume (SAW).

Fatima Maasuma (as) alikuwa hatibu hodari, mwalimu mahiri, zahidi na mcha-Mungu mkubwa. Alipatwa na maradhi alipokuwa njiani kuelekea Khorasan, huko kaskazini mashariki mwa Iran, kwa ajili ya kumtembelea kaka yake yaani Imam Ali bin Musa al Ridha (as) na akafariki dunia katika mji mtakatifu wa Qum baada ya kukaa hapo kwa siku 17.

Leo hii ziara la mtukufu huyo linatembelewa na mamilioni ya waumini kila mwaka kutoka pembe mbalimbali za dunia.     

Miaka 171 iliyopita siku kama leo Henri Poincare mtaalamu wa sayansi na hisabati wa Ufaransa alizaliwa katika mji wa Nancy nchini humo.

Poincare alikuwa mahiri katika somo la hisabati na alianza kufanya utafiti katika uwanja huo. Chunguzi mbalimbali zilizofanywa na mwanahisabati huyo wa Kifaransa kuhusiana na masuala ya uchanganuzi wa kimahesabu, mwangaza, umeme n.k zimetajwa kuwa muhimu na sahihi.

Henri Poincare

Siku kama ya leo miaka 97 iliyopita sawa na tarehe 29 mwezi Aprili mwaka 1928, nchini Uturuki herufi za Kilatini zilitambuliwa rasmi na kuchukua nafasi ya zile za Kiarabu.

Hatua hiyo ilichukuliwa katika njama za kuipiga vita dini ya Uislamu na badala yake kuingizwa tamaduni za Kimagharibi katika jamii ya wananchi wa Uturuki. Mchakato huo ulianzishwa na Mustafa Kamal maarufu kwa jina la Ataturk kuanzia mwaka 1923. Mfumo wa Jamhuri ulishika hatamu za uongozi huko Uturuki chini ya Ataturk kuanzia mwezi Oktoba mwaka 1923 baada ya kuanguka kwa utawala wa Othmania uliodumu kwa miaka 623 nchini humo.

Ataturk

Miaka 79 iliyopita katika siku kama ya leo majeshi ya Muungano yalipata pigo kubwa mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia.

Vikosi vya nchi Waitifaki wa Ulaya vilifanya mashambulizi ya pande zote dhidi ya Italia baada ya kusambaratishwa safu ya ulinzi ya Ujerumani. Italia ilikuwa muitifaki wa Ujerumani chini ya uongozi wa Musolini. Baada ya ushindi huo askari karibu milioni moja wa Ujerumani waliokuwa nchini Italia walijisalimisha kwa majeshi ya Waitifaki.   

Katika siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, yaani tarehe 9 Ordibehesht mwaka 1378 Hijria Shamsia, wawakilishi wa duru ya kwanza ya Mabaraza ya Kiislamu ya Miji na Vijiji nchini Iran walianza kazi zao na siku hii inajulikana hapa nchini kwa jina la Siku ya Mabaraza.

Kwa kuzingatia kwamba, katika Uislamu suala la mashauriano na kuwa na fikra moja lina umuhimu mno, katika Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia, Mabaraza yana nafasi muhimu na ni dhihirisho la urada ya wananchi katika mfumo wa kidini nchini Iran wenye ridhaa ya wananchi.

Katika sheria hii Mabaraza mbalimbali huchaguliwa na wananchi kwa ajili ya kuongoza masuala tofauti ya nchi ambapo Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu (Bunge la Iran) na Baraza la Wanazuoni Wanazuoni Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu ni miongoni mwa mabaraza hayo.