Hikma za Nahjul Balagha (13) + SAUTI
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 13 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Hii ni Hikma ya 13.
إِذَا وَصَلَتْ إِلَیْکُمْ أَطْرَافُ النِّعَمِ، فَلَا تُنَفِّرُوا أَقْصَاهَا بِقِلَّهِ الشُّکْرِ
Wakati zinapoanza kukufikieni sehemu za neema za Mwenyezi Mungu, msipoteze fursa ya kufikia mwisho wake kwa uchache wa shukrani.
Katika Hikma hii ya 13 ya kitabu cha Nahjul Balagha, Amir al-Mu'minin, Ali bin Abi Talib AS anatukumbusha msingi na kanuni nyingine ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa maneno yenye mvuto sana na fasaha. Huo ndio msingi wa kanuni ya neema.
Tangu siku ya kwanza ya kuumbwa ulimwengu, Mola Mlezi amekuwa akisimamia na kutawala kanuni nyingi. Bila ya kuzijua kanuni hizo, hatuwezi kuongoka kwenye njia iliyo sawa. Inaweza kusemwa kwamba, kuwa na neema na kupata mafanikio ya dunia na Akhera kuna uhusiano wa moja kwa moja na kujua kanuni za ulimwengu wa uumbaji na kuzitumia ipasavyo. Tunapozungumzia kanuni zinazotawala dunia, mtu inaweza kumpitikia moja kwa moja akilini mwake kanuni za fizikia, hisabati, kemia na nyinginezo, lakini ni wajibu tuelewe kuwa, kanuni zinazotawala ulimwengu ni pana zaidi kuliko kujumuishwa katika mawanda haya tu. Kanuni muhimu zaidi kati ya hizi ni zile zinazotawala matendo na mwenendo wa wanadamu mbele ya Mola wa ulimwengu na mbele ya wanadamu wengine na pia mbele ya viumbe wengine wa Mwenyezi Mungu na kanuni zinazohusiana na qudra na hatima ya mwanadamu mwenyewe binafsi ya jamii yake kiujumla. Jambo ambalo ni muhimu sana kulizingatia hapa ni kwamba, kanuni hizo zinakwenda na kuathiri moja kwa moja kwenye uhusiano wa kweli na halisi kati ya matendo yake mtu na matokeo ya matendo hayo. Moja ya kanunii hizo ni ile inayoonesha uhusiano wa kweli uliopo baina ya neema na shukrani za mwanadamu na utovu wa shukrani kuhusu neema anazopata mwanadamu. Katika Hikma hii ya 13 ya Nahj al-Balagha, Imam Ali AS anatukumbusha kanuni hiyo akisema: “Wakati zinapoanza kukufikieni sehemu za neema za Mwenyezi Mungu, msipoteze fursa ya kufikia mwisho wake neema hizo kwa uchache wenu wa shukrani."
Mpenzi msikilizaji, kawaida neema nyingi humjia mtu hatua kwa hatua. Mtu mwerevu na mwenye hikma hujua ni wajibu wake kushukuru tangu mwanzoni kabisa mwa kuanza kumfikia neema hizo, ili ziweze kumfikia zote kikamilifu. Mara nyingine inatokezea, mtu anaposhindwa kushukuru kwa kidogo anachopata, si tu kidogo hicho hakiwi kikubwa, lakini pia anaweza kupoteza neema yote kabla ya kuwa kubwa na kamili kutokana na utovu wake wa shukrani.

Kwa hiyo, mtu anapoona Mwenyezi Mungu amempa neema. Kwa mfano , amempa cheo, watu wanamheshimu, au Mwenyezi Mungu amempa ujuzi na ilmu na kumjaalia kuwa na ufahamu zaidi kuliko wengine, au neema nyingine yoyote ambayo ishara zake ziko wazi, basi anapaswa kujihadhari sana zisije neema hizo zikampotea kwa kukosa kwake shukrani. Kwa sababu ulimwengu unatawaliwa na sunna na kanuni za Mwenyezi Mungu. Ni kama inavyosema sheria ya tatu ya Newton kwamba kama utapiga shuti jiwe kubwa badala ya mpira, bila ya shaka yoyote mguu wako ndio utakaoumia. Au methali iliyojaa hikma ya Kiswahili inayosema: Mpiga ngumi ukuta, huumiza mkonowe. Sababu yake ni kuwa, kwa mujibu wa kanuni inayotawala ulimwengu, kiwango chochote cha nguvu tunazoingiza kwenye kitu chochote kile, kitu hicho nacho kuturejeshea nguvu hizo kwa kiwango kile kile tunachoingiza. Kadiri kitu hicho kinapokuwa chepesi, athari tunazopokea kutoka kwake zinakuwa ndogo ikilinganishwa na kitu kinapokuwa kizito kama jabali au ukuta.
Katika kanuni ya Mwenyezi Mungu pia ni vivo hivyo. Kadiri shukrani zetu zinapokuwa nyingi na za dhati zaidi, ndivyo neema zinavyozidi kuwa na baraka nyingi na kinyume chake ni hivyo hivyo, kadiri tunavyopunguza kiwango cha shukrani zetu kwa Allah, ndivyo baraka za neema Zake kwetu zinavyozidi kupotea. Baadhi ya wafasiri wa Nahjul Balagha wanasema, neema ni kama makundi ya ndege wakati wanapokuwa wametua juu ya tawi la mti utaona ndege wengine wanawafuata pole pole na kutua na kulijaza tawi hilo. Lakini kama lile kundi la kwanza litasikia sauti isiyo ya kawaida, huruka wote na hivyo hata wale ndege wengine nao hawawezi kutua tena kwenye tawi hilo.
“Is'haq Ibn Ammar” anasimulia maneno aliyoambiwa na Imam Sadiq AS. Anasema, Imam aliniambia: Ewe Aba Is-haq! Kila pale Mwenyezi Mungu anapomjaalia neema mja Wake, na mja huyo akaheshimu na kuthamini neema hiyo kwa moyo wake wote na kumshukuru Mungu waziwazi, basi Mwenyezi Mungu humzidishia neema hiyo hata kabla ya kumaliza kushukuru kwa neema hiyo.
Aya ya saba ya Surat Ibrahim inasema:
لَئِنْ شَکَرْتُمْ لاَزیدَنَّکُمْ
Na mkishukuru nitakuzidishieni.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.