Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (66)
Hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo na karibuni kujiunga nami tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu.
Kipindi chetu kilichopita kilitupia jicho kwa mukhtasari maisha na historia ya Mirza Muhammad Taqi Shirazi. Sehemu ya 66 ya mfululizo huu juma hili, itamtambulisha na kumzungumia mmoja wa Marjaa mwingine mkubwa wa Kishia ambaye si mwingine bali ni Mulla Muhammad Kadhim Khorasani mashuhuri zaidi kwa jina la Akhund Khorasani. Ni matumaini yangu kuwa mtakuwa nami hadi mwisho wa dakika hizi chache kutegea sikio yale niliyokuandalieni kwa juma hili. Karibuni.
Mulla Muhammad Kadhim Khorasani mashuhuri zaidi kwa jina la Akhund Khorasani alizaliwa 1255 Hijria katika mji wa Mash'had moja ya miji muhimu ya kidini ya Iran. Alimu huyu ni mmoja wa wanafunzi mashuhuri wa Mirza Shirazi wa Kwanza na ana cheo na daraja kubwa mno miongoni mwa wanazuoni na Maulamaa. Hata hivyo ili kumfahamu vyema alimu, msomi na Marjaa huyu mkubwa kuna ulazima wa kufanya mapitio japo kwa haraka haraka kuhusiana na matukio yaliyojiri katika kipindi cha uhai wake.
Takribani miaka 9 kabla ya kuanza Vita vya Kwanza vya Dunia, kulikuwa kukitokea matukio muhimu ya kisiasa nchini Iran. Baada ya ubunifu na hatua muhimu na isiyo na kifani ya Mirza wa Kwanza ya kuharamisha matumizi ya tumbaku na kuyaunganisha matabaka mbalimbali ya wananchi katika mapambano dhidi ya mkoloni Muingereza ambapo wananchi wa Iran walikuwa na kumbukubu nzuri ya umoja huo, wakiwa na hamu na shauku kubwa walikuwa wakitaka umoja mwingine kwa ajili ya kupambana na watawala wa ufalme wa Qajar na kufikia uadilifu.
Watawala wa Qajar ambao walikuwa wakijiona kuwa wamiliki wa roho, raia na utajiri wa Iran, walikuwa wakichukua maamuzi tena bila ya hekima na ubunifu ya kufanya miamala na madola ya Magharibi na kuyapatia upendeleo wa ajabu madola ya Ulaya ikiwemo Uingereza. Kutokuwa na ustahiki wa kuongoza watawala wa Qajar hilo lilipelekea kuwaongezeka kila siku umasikini wa wananchi na hali mbaya ya kimaisha. Jambo hilo likapelekea kuibuka malalamiko makubwa na jumuishi ya wananchi mjini Tehran. Ili kukabiliana na malalamiko hayo ya kupigania uadilifu, utawala wa Qajar ulilazimika kutumia mabavu na mkono wa chuma. Si hayo tu bali hata ulifanya mauaji ili kukandamiza malalamiko hayo ya wananchi. Maulamaa wa Tehran wakionyesha malalamiko yao walielekea Qum na kufanya mgomo wa kuketi katika haram ya bibi Fatma Maasuma (as). Maulamaa hao wakatangaza matakwa yao ambapo pamoja na mambo mengine ni kuasisiwa idara maalumu ya kushughulikia haki na uadilifu ambayo itawalazimisha viongozi akiwemo Shah kuchunga na kuheshimu sheria za Kiislamu na haki za Waislamu.
Wakati Maulamaa wa Tehran wakiwa wameelekea Qum, baadhi ya wananchi ambao walikuwa wakiwatambua vibaraka wa Uingereza mjini Tehran kuwa ndio wenye nguvu na mamlaka, wakihofia roho na uhai wao na wa familia zao walikimbilia na kuomba hifadhi katika ubalozi wa Uingereza. Ni katika hali hiyo ndipo mkoloni Muingereza alipoamua kutumia fursa hiyo kuingilia masuala ya ndani ya Iran. Maulamaa na Marajii ambao walikuwa wakiona kuwa, kutokea mapinduzi ni jambo lisilo na shaka, wakiwa na lengo la kuzuia kupotoshwa mapinduzi ya wananchi wa Iran na kuyaongoza upande na katika njia ya mafundisho ya dini, walijitokeza katika medani na kuwa bega kwa bega na wananchi. Hatua hiyo kwa mara nyingine tena ilipelekea kutokea umoja baina ya wananchi, wanafikra na viongozi wa dini na huo ukawa mwanzo mapinduzi yaliyojulikana kwa jina la Enghelāb-e Mashrūteh yaani Mapinduzi ya Katiba.
Zama na kipindi hiki kilisadifiana na uwepo wa Marajii mbalimbali nchini Iraq ambao kwa pamoja walikuwa na jukumu la uongozi wa jamii ya Kiislamu. Marajii wawili wakubwa zaidi katika zama hizo walikuwa na misimamo tofauti kuhusiana na mapinduzi haya. Akhund Khorasan ambaye ni maudhui ya kipindi chetu cha juma hili, alikuwa mmoja wa Marajii ambaye alisimama na kuunga mkono kwa nguvu zake zote Mapinduzi ya Katiba. Kwa upande wake Muhaqqiq Yazdi tangu awali yeye alikuwa akipingana na harakati hii. Muhaqqiq Yazdi alikuwa akiamini kwamba, kuanzia mwanzo tu wa harakati hiyo inapaswa kuwa wazi kwamba, Majlisi ya Ushauri wa Kitaifa (Bunge) sio mtungaji wa sheria bali ni mtekelezaji wa sheria na kanuni za Kiislamu. Lakini Akkhund Khorasani yeye alikuwa akiamini kwamba, asili ya harakati hii ni wenzo kwa ajili ya kuwekea mipaka dhulma za watawala na ndio maana alikuwa akiunga mkono na kutangaza kuwa, ni wajibu kushiriki katika harakati hii.
Kujiunga kwake na wafuasi wake na harakati ya kupigania katiba kuliyafanya mapinduzi hayo yapate ushindi kwa muda si mrefu. Na kwa utaratibu huo, baada ya kufanyika uchaguzi, Bunge la Kwanza la Katiba likaanza kazi 1285 Hijria Shamsia iliyosadifiana na 1324 Hijria Qamaria.
Baada ya Bunge kuanza kazi, kukaundwa kamati ambayo ilipewa jukumu la kuandika katiba. Kamati hiyo haikuzingatia hukumu na sheria za Kiislamu bali ilizingatia katiba ya Ubelgiji na Ufaransa na katiba hiyo hatimaye ikapasishwa kwa saini ya Shah. Hiki ndicho kitu ambacho Mullah Muhammad Kadhim Yazid au Muhaqqiq Yazdi kama anavyojulikana alikuwa amekitahadharisha hapo kabla. Hatimaye kwa miongozo ya Muhaqqiq Yazdi kutoka Najaf na ufuatiliahji wa baadhi ya Maulamaa wa Tehran kama Sheikh Fadhlullah Nuri, kukapasishwa vipengee kamilishi vya katiba.
Siku kadhaa baada ya mtawala wa wakati huo Muzafar al-Din Shah akaaga dunia na mwanawe yaani Muhammad Ali Shah akashika hatamu za uongozi. Akhund Khhorasan alimuandika barua Muhammad Ali Shah na kumnasihi mtawala huyo kijana kwamba, achunge vigezo vya kisheria na afanye hima na juhudi kwa ajili ya mamlaka ya kujitawala nchi na uadilifu katika jamii. Hata hivyo, kinyume na misimamo yake ya dhahiri, Muhammad Ali Shah alikusudia kuitawala nchi kidikteka na kimabavu.
Mapinduzi ambayo kwa kiwango kikubwa yalikuwa yamepata ushhindi na yalikuwa ni mdaiwa wa mahudhurio ya wananchi na viongozi wa dini. Hata hivyo wanafikra ambao tangu awali walikuwa na matarajio ya kuishi maisha ya Kimaghharibi, walikuwa wakiona kuwa, uwepo wa viongozi wa dini ni kikwazo kwao cha kufikkia malengo yao. Hilo ndilo lililopepelekea kuibuka hitilafu baina ya wanafikra wenye fikra na Kimagharibi na wanazuoni wa kidini. Wanafikra hao wakitumia vyombo vyao vya habari walianza kuvunjia heshima matukkufu ya Kiislamu na cheo cha uongozi wa kidini. Katika hali hiyo, Ayatullah Sheikh Fadhlullah Nouri alinyongwa kutokana na misimamo yake thabiti. Ni kuanzia wakati huo ambapo ilithibiti pia kwa Akhund Khorasani juu ya kukengeuka njia yake mapinduzi hayo.
Mbali na harakati za kisiasa, Akhund Khhorasani hakuwa nyuma pia katika harakati za kijamii ambapo alikuwa na harakati kubwa na nyingi huko Najaf. Alijenga vyuo vitatuuvya kidini na vyuo kadhaa vya taaluma mpya katika miji ya Najaf, Karbala na Baghdad huuko Iraq. Akisaidiana na wanafunzi wake alianzisha majarida kadhaa mjini Najaf kwa lengo la kueneza maarifa na mafundisho ya dini. Mwanazuoni huyu amendika vitabu vingi pia katika nyanja mbalimbali. Hata hivyo kitabu chake mashuhuri ni Kifayat al-Usul.
Watu wanaomtambuau kwa karibu Akhund Khorasani wanasema kuwa, alikuwa mcha Mungu, mwenye akili sana, mwingi wa maarifa, mpana wa kifua cha kukubali kuupokea maoni na ukosoaji na mtu aliyekuwa na hima kubwa katika mambo.
Baada ya miaka mingi ya hinma na juhudi kubwa katika njia ya kueneza mafundisho ya Uislamu, hatimaye tarehe 20 Dhulhhija 1329 Hijria, Akhund Khorasani aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 74. Waliowengi wanaamini kwamba, kifo chake kilitokana na kupewa sumu na vibaraka wa Uingereza. Kaburi la alimu hiyo linapatikana jirani na haram ya Imam Ali ibn Abi Twalib (as) katika mji wa Najaf, Iraq.
Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo uumefikia tamati tukutane tena wiki ijayo panapo majaaliwa yake Mola.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh