May 15, 2023 09:59 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha (15)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 15 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Hii ni Hikma ya 15.

 مَا کُلُّ مَفْتُونٍ یُعَاتَبُ

Si kila apatikanaye kwenye fitna hulaumiwa.

Wakati fulani kunakuwa na fitna katika jamii na haki na batili huchanganyika kwa namna ambayo ni watu wenye maarifa, imani, busuri na utambuzi tu ndio wanaoweza kutofautisha baina ya haki na batili na kushikamana na haki. Katika hikma hii ya 15 ya Nahjul Balagha, Imam Ali AS anatukumbusha matatizo ya ukosefu wa utambuzi wa watu, ambao baadhi yao hata walikuwa ni shakhsia wa kutegemewa katika jamii ya Kiislamu.

Talha na Zubair, shakhsia wawili wakubwa katika Uislamu. Walikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kutoa bay'a na kiapo cha utii kwa Imam Ali (AS) katika siku za awali kabisa za kuchukua madaraka. Siku moja baada ya kiapo cha utii, walikuja kwa Amirul-Muminin Ali AS na kudai fungu kubwa kuliko watu wengine. Lakini Imam aliwakaktaliwa. Na aliwaambia wazi kwamba hatawapa hata chembe ya zaidi ya haki yao halisi. Baada ya kupata majibu hayo, walikwenda kwenye mji wa Basra na kuua na kupora watu. Wa;oamzosha vita dhidi ya kiongozi wa zama zao, vita ambavyo baadaye vilijulikana kwa jina la Vita vya Jamal, yaani vita vya ngamia.

Imam Ali AS alitumia nafasi yake kama mtawala, kuamuru Jihadi ya kuwalinda watu wa Basra. Watu wote walikuwa tayari kwa Jihad, isipokuwa watu wanne maarufu katika umma wa Kiislamu! Watu hao wanne walipaswa kuwa mbele katika jihadi kuliko watu wa kawaida ili kama kungezuka shaka yoyote miongoni mwa wa watu wa kawaida, wapate kuwaongoza njiia sahihi.

Imam Ali AS aliwauliza watu hao wanne, mmoja wao akiwa ni “Saad bin Abil Waqqas”, kwa nini mmekaa nyuma na hamji kwenye Jihad? Saad alimji akimwambia, “Nina wasiwasi na usahihi wa Jihad hii kwa sababu inatubidi kupigana na Waislamu na maswahaba wa Mtume (SAW). Ikiwa unaweza kunipa upanga ambao unaua tu makafiri na hauui waumini, basi nitakuja pamoja nawe!

Maneno haya yanatoa ufafanuzi kuhusu fitna na kushindwa kupambanua baina ya haki na batili. Imam Ali AS aliwaambia: Inukeni na nendeni majumbani mwenu ili msiwatie shaka wengine. Baada ya wao kuondoka, Imam aliwaambia Waislamu:

مَا کُلُّ مَفْتُونٍ یُعَاتَبُ

Si kila apatikanaye kwenye fitna hulaumiwa.

Mtu ambaye kweli ameghafilika na hajui wala kuelewa ukweli, huzinduliwa na kuamshwa kupitia kulaumiwa. Lakini mtu anayejua ukweli na uhakika, lakini ikawa anajipupambaza, hawezi kuamshwa. Kumlaumu mtu kama huyo kwa nia ya kumzindua, huwa hakuna maana. Kupoteza nguvu zake mtu kujaribu kumzindua mtu kama huyu si jambo la hikma, maana ukweli anaujua na anafanya makusudi kujifanya haujui. Kiujumla ni kwamba hikma na busara inahitajika katika matendo yote ya Muislamu. Hata kukemea na kulaumu, hakupaswi kufanywa kwa hasira na dharau, bali lazima kufanywe kwa lengo la kumuamsha aliyeghafilika na kumuweka kwenye njia na mkondo sahihi.