May 23, 2023 08:09 UTC
  • Jumatatu, tarehe 22 Mei, mwaka 2023

Leo ni Jumatatu tarehe Pili Mfunguo Pili Dhulqaada 1444 Hijria sawa na Mei 22 mwaka 2023.

Tarehe Mosi Khordad mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsiya ni siku ya kumuenzi Muḥammad Saddruddin Qawam Shirazi maarufu kama Ṣadr al-Muta'allihīn na Mulla Sadra, mwanafalsafa na arif mkubwa wa Kiislamu. Alizaliwa tarehe 9 Jamadil Ula mwaka 980 Hijria Qamaria huko Shiraz. Awali alielekea katika mji wa Qazvin ambao katika zama hizo ulikuwa mji mkuu wa utawala wa Safavi na kuhudhuria darsa na masomo kwa walimu wakubwa kama Sheikh Bahai. Alisoma fiqhi, usul, Hadithi na hisabati kwa Sheikh Bahai na  mantiki, falsafa na Irfan kwa Mirdamad. Mulla Sadra alipa elimu kama sayansi asilia, hisabati, nujumu na nyota kwa Hakim Abul Qasim Mir Fendereski, mmoja wa maulamaa wakubwa wa zama zake. Mulla Sadra ametoa mchango mkubwa sana kwa falsafa ya Kiislamu. Mwanachuoni huyo mkubwa wa Kiislamu amevirithisha vizazi vya baada yake zaidi ya vitabu 40 na kitabu cha  al Asfar al-arba‘a  ndio maarufu zaidi. Mwanafasafa na mwanachuoni huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia mwaka 1050 Hijria huko Basra nchini Iraq akiwa na umri wa miaka 70 na akazikwa katika mji huo huo. 

Mulla Sadra

Miaka 1133 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Ibn Khuzaima, mpokezi wa Hadithi na faqih mashuhuri wa karne ya 4 Hijria. Ibn Khuzaima alianza kutafuta elimu katika miji na nchi mbalimbali akiwa bado kijana. Mwanazuoni huyo ameandika vitabu vingi kikiwemo kile cha al Tauhid wa Ithbat Sifatu al Raab.

Siku kama ya leo miaka 164 iliyopita, alizaliwa Arthur Conan Doyle mwandishi wa Scotland. Awali Doyle alisomea elimu ya tiba, hata hivyo kutokana na kwamba hakufaulu katika uga huo ndipo akaamua kujiunga na taaluma ya uandishi. Licha ya kwamba Doyle aliandika visa vingi lakini kilichompa umashuhuri ni majmui ya visa vya polisi vilivyoitwa Sherlock Holmes. Arthur Conan Doyle alifariki dunia mwaka 1930.

Arthur Conan Doyle

Siku kama ya leo miaka 138 iliyopita yaani mwaka 1885 aliaga dunia Victor Hugo mwandishi na malenga mashuhuri wa Kifaransa akiwa na umri wa miaka 83. Hugo alikuwa muungaji mkono mkuu wa mabadiliko kwa maslahi ya matabaka ya wanyonge na masikini nchini humo. Victor Hugo alijitosa kwenye uwanja wa kisiasa akiwa na umri wa miaka 25 na kufanikiwa kuchaguliwa kuwa mbunge. Lakini ulipofika wakati wa utawala wa Napoleon wa Tatu alijiengua kwenye uwanja huo na kubaidishwa kwa muda wa miaka 20 baada ya kupinga siasa za dikteta Napoleon wa Tatu.

Victor Hugo

Siku kama ya leo miaka 111 iliyopita yaani mwaka 1912 alizaliwa Herbert Charles Brown mwanakemia wa Uingereza. Brown alizaliwa mwaka 1912 mjini London na familia yake ikahamia Marekani kabla ya hata kutimiza miaka miwili. Alijiunga na chuo kikuu cha Chicago mwaka 1935 na kusomea kozi ya Kemia na kuendelea na masomo hadi alipofanikiwa kuwa mhazili wa chuo kikuu. Mwaka 1979 alitunukiwa tunzo ya Nobel katika taaluma ya kemia kutokana na jitihada alizofanya katika ugunduzi wa michanganyiko mipya ya kemia kaboni au Organic Chemistry. Herbert Charles Brown alifariki dunia mwaka 2004.

Herbert Charles Brown

Miaka 43 iliyopita katika siku kama hii ya leo sawa na tarehe Mosi mwezi Khordad mwaka 1359 Hijria Shamsiya ulianza mzingiro wa kiuchumi wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Marekani ambayo baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ilipoteza maslahi yake haramu nchini Iran ilianza kuiwekea Iran mzingiro wa kiuchumi lengo likiwa ni kuwashinikiza wananchi Waislamu na wanamapambano wa Iran na vilevile kuulazimisha utawala wa Jamhuri ya Kiislamu kufanya mapatano na serikali ya Washington. Baada ya uamuzi huo wa serikali ya Marekani; Imamu Khomeini (M.A) Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alitangaza kuwa uhai wa uchumi wa nchi mbalimbali hautegemei madola makubwa na kulihutubu taifa la Iran kuwa: Kamwe msiogope vikwazo vya kiuchumi; kama mtatuwekea mzingiro wa kiuchumi basi tutaimarika zaidi na ni kwa maslahi yetu."

Siku kama hii ya leo miaka 37 iliyopita Omar Tilmisani mmoja wa viongozi wa Harakati ya Ikhwanul Muslimin ya Misri aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 1904 katika eneo la Tilmisan nchini Algeria. Tilmisani alihitimu masomo yake ya shahada katika taaluma ya sheria na mwaka 1928 akawa mwanachama wa Ikhwanul Muslimin  baada ya kuasisiwa harakati hiyo. Tilmisani ambaye alimpita kwa miaka miwili Hassan al Banna kiongozi wa harakati hiyo anahesabiwa kuwa mmoja wa makada wakongwe wa harakati hiyo. Hatimaye Omar Tilmisani aliaga dunia tarehe 22 Mei 1986 akiwa na umri wa miaka 82 baada ya kupatwa na maradhi ya ini na figo.

Omar Tilmisani