Sura ya Al-Ah'qaaf, aya ya 11-14 (Darsa ya 923)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 923 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 46 ya Ah'qaaf. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 11 ya sura hiyo ambayo inasema:
وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لِلَّذِينَ آمَنُوا لَوْ كَانَ خَيْرًا مَّا سَبَقُونَا إِلَيْهِ ۚ وَإِذْ لَمْ يَهْتَدُوا بِهِ فَسَيَقُولُونَ هَٰذَا إِفْكٌ قَدِيمٌ
Na walio kufuru waliwaambia walio amini: Lau hii ingelikuwa ni kheri, wasingeli tutangulia. Na walipo kosa kuongoka wakasema: Huu ni uzushi wa zamani.
Wakati Bwana Mtume Muhammad SAW alipoanza kuwalingania watu Uislamu, masikini, wanyonge na watumwa ndio waliokuwa watu wa mwanzo kusilimu na kumwamini Nabii huyo wa Allah, kwa sababu wao hawakuwa na mali wala maslahi haramu ambayo kwa kufanya hivyo yangekuwa hatarini; na hawakuwa na ghururi na kiburi cha kuwafanya wampinge Bwana Mtume SAW. Kusilimu matabaka ya wanyonge katika jamii kuliwagusa na kuwakera maashrafu na wakubwa wa Makureishi wa Makka, ambao walijitokeza na kusema: hawa ni watu mafakiri, hohehahe na wenye akili ndogo. Kama dini hii ingekuwa ya haki na ya kweli, tungesilimu na kuiamini sisi kwanza, ambao tuna akili na uelewa mkubwa zaidi wa mambo pamoja na madaraka, mali na utajiri. Maneno hayo ya ghururi waliyosema makafiri na yasiyo na mantiki yoyote, yalitokana na kiburi na ukaidi, kwa sababu tatizo lilikuwa ni wao wenyewe, si dini ya haki ya Uislamu. Kwani kama wingu la kiburi na ghururi lisingekuwa limegubika nyoyo zao, laiti kama mvinyo wa mali, vyeo na matamanio ya nafsi usingekuwa umeziharibu akili zao na lau kama wangezivua nafsi zao joho la kujitukuza na kujiona bora kuliko watu wengine wakawa na nyoyo safi na zenye kiu ya kuijua haki kama walivyokuwa watu masikini na wanyonge, nao pia wangevutiwa na Uislamu na kusilimu haraka. Kisha aya inaendelea kueleza kwamba: kwa sababu wao hawakuukubali uongofu wa Qur’ani, wanakimbilia kusema: Qur’ani si maneno ya Mwenyezi Mungu, bali kama zilivyo ngano na simulizi zingine za kale, ni maneno yaliyotungwa na yasiyo na msingi wowote. Walitoa tuhuma hizo dhidi ya Kitabu hicho cha Allah kama kisingizio tu cha kuhalalisha kutosilimu kwao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, makafiri ni watu wanaojiona mahodari na wenye akili zaidi kuliko Waislamu na kudhani kwamba dini na itikadi yao ni bora kuliko Uislamu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa tuhuma mbovu inazonasibishwa nazo Qur’ani, Bwana Mtume pamoja na Uislamu zinatokana na kiburi, ghururi, inadi na ukaidi; si hoja na mantiki.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 12 ambayo inasema:
وَمِن قَبْلِهِ كِتَابُ مُوسَىٰ إِمَامًا وَرَحْمَةً ۚ وَهَٰذَا كِتَابٌ مُّصَدِّقٌ لِّسَانًا عَرَبِيًّا لِّيُنذِرَ الَّذِينَ ظَلَمُوا وَبُشْرَىٰ لِلْمُحْسِنِينَ
Na kabla yake kilikuwapo Kitabu cha Musa, kuwa kiongozi na rehema. Na hiki ni Kitabu chenye kusadikisha na cha lugha ya Kiarabu, ili kiwaonye walio dhulumu, na kiwe ni bishara kwa watendao mema.
Kutokana na tuhuma ambazo washirikina wa Makka walikuwa wakitoa dhidi ya Qur’ani na Bwana Mtume SAW, na kudai kwao kwamba kitabu hicho cha Allah ni ngano zisizo na msingi wowote, aya hii inasema: moja ya alama za ukweli wa kitabu hiki cha Qur’ani ni kwamba jina na sifa za Mtume Muhammad SAW zimetajwa ndani ya Taurati. Isitoshe, aya za Qur’ani zinaendana na kusadikishana na zile za Taurati. Hii inaonyesha kuwa, vitabu viwili hivyo vimeteremshwa kutoka kwenye asili na chimbuko moja. Japokuwa lugha ya Taurati ni ya Kiebrania; na lugha ya Qur’ani ni ya Kiarabu, lakini muhtawa na yaliyomo ndani ya vitabu vyote hivyo viwili ni kuhusu kuwalingania watu wamwamini Mwenyezi Mungu na kutii maamrisho yake; na lengo la vyote viwili ni kupambana na madhalimu na kuwapa maonyo na indhari na vilevile kutoa bishara ya ushindi, saada na fanaka kwa waja watendao mema. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kuteremshwa vitabu vya mbinguni ni moja ya utaratibu, ambao Allah SWT ameutumia katika zama zote za historia kwa ajili ya mwongozo wa wanadamu. Vitabu hivyo vinaafikiana na kuthibitishana; si kupingana wala kukanushana. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kitabu cha mbinguni ni dhihirisho la rehma za Mwenyezi Mungu; na jamii yoyote ile hupata rehma za Mola inapokifanya kitabu chake kuwa ndio dira na mwongozo wake. Halikadhalika aya hii inatuelimisha kwamba, kumwamini Mwenyezi Mungu hakuendani na kuwafanyia dhulma watu. Imani ya kweli na yenye faida ni ile inayomfanya mtu awe mtenda mema na ihsani kwa viumbe wenzake.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 13 na 14 za sura yetu ya Ah’qaaf ambazo zinasema:
إِنَّ الَّذِينَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا فَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ
Hakika walio sema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu; kisha wakawa na msimamo, hawatakuwa na khofu, wala hawatahuzunika.
أُولَٰئِكَ أَصْحَابُ الْجَنَّةِ خَالِدِينَ فِيهَا جَزَاءً بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ
Hao ndio watu wa Peponi, watadumu humo, ni malipo kwa waliyo kuwa wakiyatenda.
Aya hizi zinatoa taswira ya waumini wa kweli, ambao Mitume na vitabu vya mbinguni vimeletwa kwa ajili ya kulea na kutoa watu kama hao na kueleza kwamba: waabudu wa tauhidi na Mungu pekee wa haki husema, Mola wetu sisi ni Allah na hubaki kuwa thabiti katika njia na imani hiyo. Ni wazi kwamba kumwamini Mwenyezi Mungu moyoni tu au kutamka kwa ulimi baadhi ya maneno tu, hakutoshi kuthibitisha kuwa mtu amemwamini kikwelikweli Mwenyezi Mungu, bali katika matendo pia, inatupasa tufanye kama alivyotuamuru Yeye Mola na tuwe na istiqama ya kubaki imara na thabiti katika njia hiyo. Isije ikawa tunapofikwa na baadhi ya misukosuko na matatizo, tunaipoteza johari ya imani na kuiacha njia ya Allah na badala yake, tukapaparika kujikusanyia mali na utajiri na kujali kuridhisha hawaa na matamanio ya nafsi zetu; na hasa katika zama hizi, ambapo kutokana na kukithiri mambo ya kumtumbukiza mtu kirahisi kwenye ufisadi, ufuska, mahusiano holela ya kijinsia na dimbwi la madhambi, kuitunza mtu imani yake ni kazi ngumu, ambayo haiwezekani kirahisi bila ya kuwa na istiqama na msimamo thabiti. Na tab’an Mwenyezi Mungu Mtukufu atawapa waumini wa kweli malipo mema duniani na akhera, ikiwemo kuwapa ushuwari na utulivu hata katika maisha ya hapa duniani. Watu kama hao hawawi na woga wala hofu yoyote ya matukio yajayo, wala majonzi na huzuni kwa yaliyopita. Mkabala wake, kuna matajiri wengi na watu wenye nguvu kubwa za madaraka, ambao kidhahiri wanaonekana wamenawiri kwa siha za kimwili, lakini hawana umakini wala utulivu wa moyo na akili, kiasi kwamba wanapotaka kuondoa msongo wa mawazo na tafrani walizonazo, baadhi ya wakati huishia kubwia vidonge vya kupoza maumivu au hata mihadarati na madawa ya kulevya. Kwa upande wa waumini wa kweli, mbali na kupata ushwari na utulivu wa moyo na roho, ambayo ni malipo yao mema ya hapa duniani, huko akhera pia Allah SWT atawalipa Pepo wale waliofuata njia ya tauhidi na wakabaki kuwa thabiti na wenye istiqama katika njia hiyo; pepo ambayo akili ya mwanadamu haiwezi kutasawiri ukubwa wake wala muda wa kuishi ndani yake. Kwani watu wa peponi wataishi humo milele na kustareheshwa kwa neema zake zisizomalizika. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kusema tu tumeamini na kuikubali tauhidi kwa ulimi tu hakutoshi, bali muhimu zaidi, ni kuwa na istiqama na kuendelea kuwa thabiti katika njia hiyo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, mtu anayemwamini kikweli Mwenyezi Mungu, ghairi ya Yeye Allah SWT hawi na woga wala hofu ya mtu au kitu chochote kile. Wa aidha aya hizi zinatutaka tujue kwamba, simanzi kwa yaliyopita huwa nazo watu wajutao kwa kufuata njia isiyo sahihi na ya makosa; lakini kwa wale wanaojitahidi muda wote kufuata na kushikamana na njia ya haki, hao hawapatwi na majuto wala majonzi na simanzi kwa waliyotanguliza huko nyuma. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 923 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azipe uthabiti imani zetu, atutakabalie amali zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/