May 27, 2023 05:47 UTC
  • Sura ya Fat-h, aya ya 26-29 (Darsa ya 943)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 943 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 48 ya Al Fat-h. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 26 ya sura hiyo ambayo inasema:

إِذْ جَعَلَ الَّذِينَ كَفَرُوا فِي قُلُوبِهِمُ الْحَمِيَّةَ حَمِيَّةَ الْجَاهِلِيَّةِ فَأَنزَلَ اللَّهُ سَكِينَتَهُ عَلَىٰ رَسُولِهِ وَعَلَى الْمُؤْمِنِينَ وَأَلْزَمَهُمْ كَلِمَةَ التَّقْوَىٰ وَكَانُوا أَحَقَّ بِهَا وَأَهْلَهَا ۚ وَكَانَ اللَّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا

Pale walio kufuru walipo tia nyoyoni mwao mori, mori wa kijinga, basi hapo Mwenyezi Mungu aliteremsha utulivu juu ya Mtume wake na juu ya Waumini, na akawalazimisha neno la kumcha (Mwenyezi Mungu). Na wao walikuwa ndio wenye haki nalo na wenye kustahili. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu. 

Katika darsa kadhaa zilizopita tumezungumzia Sulhu ya Hudaibiya, eneo lililoko karibu na Makka; suluhu ambayo ilifikiwa kati ya Bwana Mtume Muhammad SAW na wakubwa wa washirikina wa mji huo. Aya hii tuliyosoma inazungumzia moja ya sababu za ukafiri, ambayo ni watu kuwa na mori na ukereketwa usio na msingi juu ya mambo na kueleza kwamba: taasubi, mori na ghururi za kijahilia ziliwafanya washirikina wasikubali kumruhusu Bwana Mtume SAW na masahaba zake waingie Makka kwa ajili ya kufanya Umra na kutekeleza amali ya uchinjaji katika ibada hiyo. Washirikina hao wa Kikureishi walikuwa wakisema: Hawa Waislamu walituulia baba zetu na ndugu zetu katika vita vya Badr na Uhud. Iweje leo tuwaruhusu waingie kwenye mjii wetu wa Makka na kurudi walikotoka salama usalimini? Waliyasema hayo ilhali walikuwa wakifahamu kwamba kuzuru Nyumba ya Allah ya Al-Kaaba kumeruhusiwa kwa watu wote; na ardhi ya Makka ni haram tukufu ya amani, kiasi kwamba hata kama mtu angekutana na aliyemuulia baba yake katika ardhi hiyo au wakati wa amali za Hija na Umra, asingemsumbua wala kumfanya chochote. Lakini mkabala wake, Allah SWT alishusha utulivu kwa Bwana Mtume na masahaba zake na kuzijaza nyoyo zao subira na uvumilivu; na kwa hiyo ili kuepusha umwagaji damu katika haram na eneo lake hilo la amani, wakaamua waghairi kutekeleza kwa muda matakwa waliyokusudia; na badala yake wakafungiana na washirikina mkataba wa suluhu, ambao uliwafungulia njia ya kwenda kuzuru Nyumba ya Mwenyezi Mungu katika miaka iliyofuatia. Hali ya kuwa laiti kama na wao pia wangepandwa na taasubi na mori wa kijahilia, moto wa vita ungewaka katika ardhi hiyo takatifu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, taasubi za aina yoyote katika masuala ya kifikra na matendo, ambazo zinatokana na utamaduni wa kijahilia usio na mantiki wala hoja sahihi, hazikubaliki katika Uislamu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, sharti mojawapo la imani ya kweli, taqwa na uchamungu ni kudumisha utulivu na kutumia muamala na mlahaka wa kimantiki bila hasira na ukali, katika masuala ya binafsi na ya kijamii.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 27 ambayo inasema:

لَّقَدْ صَدَقَ اللَّهُ رَسُولَهُ الرُّؤْيَا بِالْحَقِّ ۖ لَتَدْخُلُنَّ الْمَسْجِدَ الْحَرَامَ إِن شَاءَ اللَّهُ آمِنِينَ مُحَلِّقِينَ رُءُوسَكُمْ وَمُقَصِّرِينَ لَا تَخَافُونَ ۖ فَعَلِمَ مَا لَمْ تَعْلَمُوا فَجَعَلَ مِن دُونِ ذَٰلِكَ فَتْحًا قَرِيبًا

Hakika Mwenyezi Mungu amemtimizia Mtume wake ndoto ya haki. Bila ya shaka nyinyi mtauingia Msikiti Mtakatifu, Inshallah, kwa salama, na hali mmenyoa vichwa vyenu na mmepunguza nywele. Hamtakuwa na khofu. Yeye alijua msiyo yajua. Mbali na haya alikupeni ushindi ulio karibu. 

Kabla Waislamu hawajaondoka kuelekea Makka, Bwana Mtume SAW aliota ndoto, kwamba yeye na masahaba zake wanaingia Masjidul-Haram, Msikiti mtukufu wa Makka kwa ajili ya kufanya amali za Umra; na akawasimulia masahaba zake ndoto hiyo aliyoota. Masahaba walidhani tafsiri ya ndoto hiyo itathibiti katika mwaka uleule. Kwa hivyo wakati washirikina walipowawekea kizuizi na kuwafungia njia wasiingie Makka, baadhi ya Waislamu waliingiwa na shaka na kujisemea, hivi inawezekana kweli ndoto ya Mtume isiwe ya kweli!? Hapo ndipo ilipoteremshwa aya hii kusisitiza kwamba ndoto hiyo ni ya kweli na ni hakika kabisa kwamba hatimaye nyinyi nyote mtaingia Msikiti Mtukufu. Kulingana na makubaliano yaliyofikiwa kwenye mkataba wa Sulhu ya Hudaibiya, mwaka uliofuatia washirikina walifungua njia na kuiacha Makka wazi kwa muda wa siku tatu; na Waislamu wakaweza kutekeleza kwa kutanafasi na kwa utulivu kamili amali za Umra. Tab'an baada ya muda, washirikina wa Kikureishi walihalifu makubaliano ya mkataba huo, na katika mwaka wa nane Hijria Waislamu wakafanikiwa kuikomboa Makka bila ya vita wala umwagaji damu wowote. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, tuwe na hakika kuwa ahadi za Mwenyezi Mungu zitathibiti tu, japokuwa yamkini kulingana na ujuzi na hikma yake, kuthibiti kwake kunaweza kukachukua muda, lakini ucheleweshwaji huo usiwe sababu ya sisi kuingiwa na shaka na hatihati. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, ikiwa kukubali suluhu kutatokana na kuzingatia maslaha na manufaa ya jamii; na si kwa sababu ya woga wa kumhofu adui, si hasha athari za suluhu hiyo zikawa na baraka nyingi na kuwa utangulizi wa ushindi dhidi ya adui.

Ifuatayo sasa ni aya ya 28 ambayo inasema:

هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ ۚ وَكَفَىٰ بِاللَّهِ شَهِيدًا

Yeye ndiye aliye mtuma Mtume wake kwa uwongofu na Dini ya Haki, ili ishinde dini zote. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Shahidi.

Aya hii inaendeleza maudhui iliyozungumziwa katika aya iliyopita, iliyowapa Waislamu ahadi ya ushindi dhidi ya washirikina wa Makka na kueleza kwamba: ushindi huu utaendelea; na itafika zama ambapo Uislamu utatawala duniani na kuzishinda dini na itikadi zingine zote, kwa sababu maneno ya Mwenyezi Mungu ni haki; na utawaongoza na kuwaelekeza watu kwenye saada na fanaka. Kwa mujibu wa Hadithi mutawaatir, ambazo zimepokewa na kukubaliwa na Waislamu wote, katika aakhiru-zaman ahadi hiyo ya Allah SWT itatimizwa na mtu anayetokana na kizazi cha Bwana Mtume Muhammad SAW aitwaye "Mahdi". Kwa msaada na ushirikiano wa wanyonge na wanaodhulumiwa duniani, mtukufu huyo atasimama kupambana na watawala madhalimu na watumiaji mabavu. Kwa msaada wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, Imam Mahdi (AF) atawashinda madhalimu na kusimamisha uadilifu na amani ulimwenguni kote. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kwa irada na matakwa ya Allah, dini ya haki itaenea ulimwengu mzima na kupatikana njia na sababu za kuongoka na kufuata walimwengu dini ya Mwenyezi Mungu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, dini zilizopita zilikuwa makhususi kwa watu wa zama fulani, lakini kinyume na dini hizo, mafundisho ya Uislamu hayahusu zama na watu maalumu. Na kwa sababu hiyo, Waislamu inawapasa watekeleze ipasavyo jukumu na wajibu wao kwa kuitambulisha kwa walimwengu sura safi na halisi ya Uislamu.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 29 na ya mwisho ya sura yetu ya al-Fat-h ambayo inasema:

مُّحَمَّدٌ رَّسُولُ اللَّهِ ۚ وَالَّذِينَ مَعَهُ أَشِدَّاءُ عَلَى الْكُفَّارِ رُحَمَاءُ بَيْنَهُمْ ۖ تَرَاهُمْ رُكَّعًا سُجَّدًا يَبْتَغُونَ فَضْلًا مِّنَ اللَّهِ وَرِضْوَانًا ۖ سِيمَاهُمْ فِي وُجُوهِهِم مِّنْ أَثَرِ السُّجُودِ ۚ ذَٰلِكَ مَثَلُهُمْ فِي التَّوْرَاةِ ۚ وَمَثَلُهُمْ فِي الْإِنجِيلِ كَزَرْعٍ أَخْرَجَ شَطْأَهُ فَآزَرَهُ فَاسْتَغْلَظَ فَاسْتَوَىٰ عَلَىٰ سُوقِهِ يُعْجِبُ الزُّرَّاعَ لِيَغِيظَ بِهِمُ الْكُفَّارَ ۗ وَعَدَ اللَّهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ مِنْهُم مَّغْفِرَةً وَأَجْرًا عَظِيمً

Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na walio pamoja naye ni imara mbele ya makafiri, na wanahurumiana wao kwa wao. Utawaona wakirukuu na kusujudu wakitafuta fadhila na radhi za Mwenyezi Mungu. Alama zao zi katika nyuso zao, kwa athari ya kusujudu. Huu ndio mfano wao katika Taurati. Na mfano wao katika Injili ni kama mmea uliotoa matawi yake, kisha yakautia nguvu, ukawa mnene, ukasimama sawasawa juu ya shina lake, ukawapendeza wakulima, ili kuwakasirisha makafiri kwa ajili yao. Mwenyezi Mungu amewaahidi walio amini na wakatenda mema katika wao maghufira na ujira mkubwa. 

Aya hii, ambayo kama tulivyotangulia kueleza, ndio aya ya mwisho ya Suratul-Fat-h, inataja masharti yanayolazimu kutimizwa ili kuthibiti ahadi iliyotolewa na Mwenyezi Mungu katika aya iliyotangulia na kueleza kwamba: ili Uislamu uzishinde dini zingine, inapasa Waislamu waratibu mahusiano yao, kuanzia watu binafsi na ya kijamii kulingana na sifa hizi nne zifuatazo: Mosi: katika kuamiliana na maadui wawe na ushujaa, ukali, uthabiti na ujasiri. Pili: katika kuamiliana na Waislamu na waumini wenzao wawe na huruma, upole, upendo na urafiki. Tatu: muamala wao na Allah SWT uwe wa kuabudu na kudhihirisha uja kwake kwa ikhlasi. Na nne: kuhusiana na wao wenyewe binafsi wajipinde na kufanya juhudi kwa ajili kujiletea ustawi na maendeleo na kujitawala kiuchumi na kisiasa. Iwapo Waislamu watazifanya nukta nne hizo kuwa ndio dira ya kuongozea mambo yao, sio tu hapa duniani watawashinda maadui zao, lakini huko akhera pia watapata maghufira na rehma za Mwenyezi Mungu Mtukufu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, Uislamu ni dini iliyokamilika yenye ratiba na mwongozo kwa ajili ya vipengee na pande zote za maisha ya mwanadamu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, haitawezekana Uislamu kuwa dini na mfumo wa ulimwengu mzima, pasi na kufuatwa sawasawa sira na suna za Bwana Mtume Muhammad SAW na kuwepo wafuasi wakweli na wenye msimamo thabiti. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba, taswira na sifa za wafuasi wa Bwana Mtume SAW zimeelezewa ndani ya Taurati na Injili pia. Halikadhalika aya hii inatutaka tuelewe kwamba uongezekaji wa kiidadi na ukuaji wa kiubora wa Waislamu unawaudhi na kuwakasirisha maadui. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 943 ya Qur'ani imefikia tamati, na ndio inayotukamilishia tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura hii ya 48 ya al Fat-h. Inshaallah tuwe tumeaidhika na kuelimika na yote tuliyojifunza katika sura hii. Tunamwomba Allah aharakishe kudhihiri kwa mwokozi wa ulimwengu Imamu wa Zama, Imam Mahdi (AF) na kuuwezesha Uislamu kutawala ulimwenguni kote na kusimamisha haki na uadilifu kwa walimwengu wote. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/