Sura ya Qaaf, aya ya 23-30 (Darsa ya 951)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 951 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 50 ya Qaaf. Tunaianza darsa yetu kwa aya yake ya 23 hadi ya 26 ambazo zinasema:
وَقَالَ قَرِينُهُ هَٰذَا مَا لَدَيَّ عَتِيدٌ
Na (malaika) aliye pamoja naye atasema: Haya ndiyo yaliyo tayari kwangu.
أَلْقِيَا فِي جَهَنَّمَ كُلَّ كَفَّارٍ عَنِيدٍ
(Wataambiwa malaika) Mtupeni katika Jahannamu kila kafiri mwenye inadi,
مَّنَّاعٍ لِّلْخَيْرِ مُعْتَدٍ مُّرِيبٍ
Azuiaye kheri, arukaye mipaka, mwenye kutia shaka,
الَّذِي جَعَلَ مَعَ اللَّهِ إِلَٰهًا آخَرَ فَأَلْقِيَاهُ فِي الْعَذَابِ الشَّدِيدِ
Ambaye amemfanya mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu. Basi mtupeni katika adhabu kali.
Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizowazungumzia malaika wanaoandamana na mtu muda wote, ambao huandika na kuhifadhi mambo yake yote mema na mabaya anayoyafanya hapa duniani, na ambao Siku ya Kiyama watamuelekeza pia mwanadamu ama peponi au motoni. Aya hizi tulizosoma zinasema, kwa kuzingatia namna litakavyokuwa daftari la amali lilioandaliwa na malaika hao, mwanadamu atahudhurishwa kwenye mahakama ya Kiyama; na hapo Allah SWT atawatenganisha waovu waliokufuru na wema walioiamini haki, na kuwalipa waovu hao malipo ya amali zao. Sababu ni kuwa watu hao walimkufuru Mwenyezi Mungu kwa kuifanyia haki inadi na ukaidi; na katika matendo pia waliliwekea kizuizi kila jambo la kheri. Watu wa aina hiyo hukiuka na kuvuka mipaka ya Mwenyezi Mungu na kuwatia shaka pia watu wengine wasiikubali na kuifuata njia ya haki. Na mbali ya Yeye Mola wa haki aliyetukuka na kutakasika, wanawashawishi na kuwaelekeza pia watu kwenye waola wengine. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kama ukafiri na kumkanusha Allah kutakuwa kumetokana na ujinga tu na kutojua huwepo matumaini ya mtu kurejea kwenye haki. Lakini kama inadi, ukaidi, taasubi na ukereketwa ndivyo vinavyomfanya mtu amkufuru na kumkana Mwenyezi Mungu, basi kadiri siku zinavyopita ndivyo mtu huyo atakavyozidi kuselelea kwenye ukafiri, na wala hakutakuwa na matarajio na uwezekano wa yeye kumwamini Allah. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kinyume na waumini, ambao ni watu wa mambo ya kheri na wanawalingania na kuwaita wenzao kwenye mambo mema, wakanushaji wa haki huwa wanawazuia watu kufanya mema na ya kheri. Wa aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba, adhabu ya moto ina viwango kadhaa na inategemea kiwango cha ukafiri, shirki na madhambi ya mtu.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 27 hadi ya 30 ya sura yetu ya Qaaf ambazo zinasema:
قَالَ قَرِينُهُ رَبَّنَا مَا أَطْغَيْتُهُ وَلَٰكِن كَانَ فِي ضَلَالٍ بَعِيدٍ
Mwenzake atasema: Ee Mola wetu Mlezi! Sikumpoteza mimi, bali yeye mwenyewe alikuwa katika upotovu wa mbali kabisa.
قَالَ لَا تَخْتَصِمُوا لَدَيَّ وَقَدْ قَدَّمْتُ إِلَيْكُم بِالْوَعِيدِ
(Mwenyezi Mungu) atasema: Msigombane mbele yangu. Nilikwisha kutangulizieni onyo langu.
مَا يُبَدَّلُ الْقَوْلُ لَدَيَّ وَمَا أَنَا بِظَلَّامٍ لِّلْعَبِيدِ
Kwangu haibadilishwi kauli, wala Mimi siwadhulumu waja wangu.
يَوْمَ نَقُولُ لِجَهَنَّمَ هَلِ امْتَلَأْتِ وَتَقُولُ هَلْ مِن مَّزِيدٍ
Siku tutapo iambia Jahannamu: Je! Umejaa? Nayo itasema: Je! Kuna ziada?
Katika aya hizi wamezungumziwa wale aliokuwa nao mtu hapa duniani ambao watakuwa sababu ya yeye kuingizwa motoni, kama marafiki wabaya na vinara wa ukafiri wakiongozwa na shetani. Wakati watu wote watakapotambua nini itakuwa hatima yao halisi katika siku hiyo ya Kiyama, watu waovu watagombana na kupapurana wao kwa wao na viongozi wao mafisadi pamoja na shetani, huku kila mmoja akijaribu kumbebesha mwenzake dhima ya mzigo wa madhambi wake. Waovu hao watawaambia wale waliowafuata, kama isingelikuwa nyinyi, sisi tungeliamini. Au watawaambia: sisi tumekuwa wenye kuhasirika na kuishia kwenye hilaki na masaibu haya kwa sababu ya kukufuateni nyinyi. Pamoja na hayo, mabishano na misutano hiyo haitakuwa na taathira yoyote kwa adhabu waliyoandaliwa, wala wao hawatapata ahueni na wepesi wa kupunguziwa adhabu hiyo. Shetani na yeye kwa upande wake atajitetea kwa kusema: Ewe Mola wangu, mimi sikumlazimisha mtu yeyote akukufuru au aasi kutekeleza amri zako, bali wao wenyewe waliipuuza njia yako wakaghiriki kwenye lindi la upotofu. Pamoja na hayo, watu wa motoni watang'ang'ania kumbebesha dhima shetani ili kuhalalisha madhambi yao na kupotea kwao. Hapo ndipo itanadiwa kutoka Mwenyezi Mungu Jalla Jalaaluh na kuhitimishwa mabishano na misutano ya watu wa motoni kwa kuwaambia watu hao: sasa si wakati tena wa kusema hayo, hatima ya kila mtu imeshabainika wazi na ataadhibiwa kulingana na makosa yake, hatopunguziwa wala kuzidishiwa. Na wala isije ikampitikia mtu akadhani kwamba ukubwa wa Jahanamu una mpaka maalumu, na kwa hivyo kwa kuwepo umati mkubwa wa wafanya madhambi makubwa makubwa na mazito zaidi haitaweza kufika zamu yake yeye. Moto huo wa kutisha utawahutubu na kuwaita waovu na wafanya madhambi na kuuliza: kuna kingine chochote zaidi ya hiki?! Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, sisi sio tunaowachagua wale watakaokuwa baba na mama zetu, au kaka na dada zetu, lakini ni sisi wenyewe ndio tunaowachagua wenza, masahibu na marafiki zetu; na wao wana taathira kubwa sana katika hatima na mwisho wetu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, Siku ya Kiyama mtu hatoweza kuwabebesha mzigo wa makosa yake marafiki wabaya, viongozi waovu na madhalimu au hata shetani, kisha yeye mwenyewe akajiondolea dhima na masuulia ya makosa hayo. Vilevile aya hizi zinatutaka tufahamu kwamba Mwenyezi Mungu SWT hajaacha kukamilisha dhima katika suala la kufikisha uongofu kwa watu wote, hata ihisike kwamba amewafanyia dhulma waja wake; na vivyo hivyo hatalifumbia macho suala la kuwaadhibu madhalimu, kwa sababu kuwapunguzia adhabu madhalimu kutakuwa sawa na kuwadhulumu watenda mema na wale waliodhulumiwa. Halikadhalika aya hizi zinatuelimisha kuwa, watu waovu wataadhibiwa kwa kutiwa motoni kwa sababu ya dhulma walizozifanyia nafsi zao; na si kwamba wao watadhulumiwa na Allah SWT, kwa sababu Yeye Mola hamdhulumu katu mja wake yeyote. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 951 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa na wenza wema na marafiki wazuri ambao watakuwa sababu ya sisi kufuzu katika dunia na akhera yetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/