Jumamosi, 3 Juni, 2023
Leo ni Jumamosi tarehe 14 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1444 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 3 Juni 2023 Miladia.
Miaka 521 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 3 Juni 1502 Miladia, yalitokea mauaji ya kutisha ya halaiki ya Calicut yaliyofanywa na baharia maarufu wa Kireno Vasco da Gama. Calicut, ambayo leo hii inajulikana kwa jina la Kozhikode, ni mji wa bandari ulioko Madras kusini mwa India. Mji huo wa bandari, ndio mahali pa mwanzo alipowasili Vasco da Gama mwaka 1498 na kuukalia. Na kama walivyokuwa wakoloni wengine, alijiona kuwa yeye ndiye mmliki wa asili wa India. Wakati mabaharia mia nane Waarabu walipowasili katika bandari hiyo ya Calicut kwa lengo la kufanya biashara ya mchele, Vasco da Gama aliamuru wakamatwe; kwanza wakakatwa mikono, masikio na pua na kisha yakachomwa moto majahazi yao na wote wakauliwa kwa halaiki.***
Siku kama ya leo miaka 356 iliyopita, yaani tarehe 3 Juni, 1667 Miladia, kwa mara ya kwanza katika historia ya utabibu na upasuaji, ilifanywa operesheni ya kutia damu ndani ya mwili ya mwanadamu. Operesheni hiyo ilifanywa na tabibu wa Kifaransa aitwaye Jean Baptiste Denis. Kutiwa damu ndani ya mwili wa mgonjwa yalikuwa mageuzi makubwa katika sayansi ya utabibu, kwa sababu hadi kabla ya hapo wagonjwa wengi walikuwa wakipoteza maisha kutokana na kuishiwa na damu kwa wingi mwilini au kwa upungufu wa damu. Katika majaribio yake ya mwanzo, tabibu huyo wa Kifaransa aliingiza damu ya kondoo ndani ya mwili ya mtu, lakini baadaye akawa anawatia wagonjwa damu za wanadamu wenzao. ***
Siku kama ya leo miaka 166 iliyopita alizaliwa, Jacques de Morgan, mtaalamu wa historia ya maumbile na mwanasayansi wa masuala ya ardhi wa nchini Ufaransa. Awali alisafiri nchi tofauti kwa ajili ya kuvumbua madini mbalimbali ambapo kwa muda fulani alijishughulisha pia na uvumbuzi wa masuala ya historia nchini Misri. Tangu mwaka 1889 Miladia na kwa muda wa miaka mitatu Morgan alifanya utafiti kuhusiana na masuala ya kale nchini Iran huku akiandika vitabu katika uwanja huo. Kuanzia mwaka 1889 na kuendelea kwa miaka 15 baadaye alikuwa msimamizi wa kamisheni ya masuala ya kihistoria nchini Ufaransa ambapo aliendeleza utafiti wake katika maeneo mbalimbali ya dunia. Jacques de Morgan alifariki dunia mwaka 1924. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na kitabu cha 'Mwanadamu Kabla ya Historia' 'Operesheni ya Kielimu Mjini Paris' na 'Utangulizi wa Historia ya Mashariki.' ***
Miaka 60 iliyopita katika siku kama hii ya leo, yaani tarehe 3 Juni 1963, Imam Khomeini (MA), mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na kwa mnasaba wa Ashura ya Imam Hussein (AS) alitoa hotuba kali na ya kihistoria dhidi ya utawala wa kiimla wa Kipahlavi. Hotuba hiyo ilitolewa mbele ya hadhara kubwa ya wananchi wakiwemo maulamaa na wanafunzi wa kidini wa chuo cha Fayziyyah katika mji wa Qom, licha ya vizuizi na vitisho vikali vilivyotolewa na utawala wa Shah. Katika hotuba yake, Imam Khomeini alikosoa vikali vitendo vya kihaini vya Shah na vibaraka wake na kufichua mbele ya wananchi Waislamu wa Iran usaliti waliokuwa wakifanya. Katika sehemu moja ya hotuba hiyo, Imam Khomeini alisema: "Hawa wanaupinga Uislamu wenyewe pamoja na mashekhe na wana nia ya kuuangamiza. Enyi watu, Uislamu wetu na nchi yetu viko hatarini. Tuna wasiwasi mkubwa na tunasikitikishwa na hali ya Iran na hali ya walioshika hatamu za utawala."
Miaka 7 iliyopita katika siku kama ya leo, tarehe 3 Juni 2016 aliaga dunia Muhammad Ali, nguli wa ndondi za uzito wa juu duniani. Muhammad Ali ambaye alizaliwa Januari 17, 1942 kwa jina la Cassius Marcellus Clay, Jr alikuwa mmoja wa mabondia mashuhuri na watajika zaidi wa mchezo wa masumbwi katika uzito wa juu duniani. Alitwaa taji la ubingwa wa ndondi za uzito wa juu akiwa na umri wa miaka 22 tu. Baada ya kusilimu, mbali na ubondia, Muhammad Ali alijihusisha pia na harakati za kisiasa, jambo ambalo lilimpa umashuhuri zaidi duniani kulinganisha na mabondia wengine. Ali ambaye alitambuliwa na wengi kama mwanamichezo nyota wa karne ya 20, baada ya kuyahimili kwa miaka 32 maradhi ya Parkinson, hatimaye alifariki dunia hospitalini katika siku kama ya leo kutokana na matatizo ya kupumua. ***
