Jumatatu, tarehe 5 Juni, 2023
Leo ni Jumatatu tarehe 16 Dhulqaada 1444 Hijria sawa na tarehe 5 Juni 2023.
Katika siku kama ya leo miaka 240 iliyopita baluni lilirushwa angani kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya jitihada za mwanadamu za kutaka kupaa angani.
Baluni hilo lilikuwa na watu wawili, mmoja wao akiwa ni mwanafizikia wa Kifaransa aliyejulikana kwa jina la Jean-Francois Pilatre de Rozier.
Tangu alipokuwa shuleni de Rozier alikuwa akifikiria jinsi ya kutengeneza chombo cha kupaa angani na hatimaye baada ya r kutengeneza baluni, naye pia alitengeneza baluni lake na akapaa angani nalo katika siku kama hii ya leo.
Mwanafizikia huyo alianguka chini na kufariki dunia katika moja ya safari zake za uhakiki angani.
Siku kama ya leo miaka 135 iliyopita Ayatullah Zainul Abidin Mazandarani mmoja wa maulamaa wakubwa wa Kiirani aliaga dunia.
Baada ya kuhitimu masomo ya awali, Ayatullah Mazandarani alielekea katika hauza ya kielimu ya Najaf huko Iraq ili kukamilisha masomo ya kidini. Akiwa huko mwanazuoni huyo alifunzwa na maustadhi wakubwa wa zama hizo wa hauza ya Najaf kama vile Sheikh Murtadha Ansari na kufikia daraja ya juu ya kielimu na kimaanawi.
Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, wananchi Waislamu wa Iran baada ya kupata habari kwamba Imam Khomeini (MA) alikuwa amekamatwa na utawala dhalimu wa Shah, walifanya maandamano makubwa kote nchini dhidi ya utawala huo.
Siku kadhaa kabla yake, Imam Khomeini alikuwa ametoa hotuba kali katika Chuo cha Kidini cha Faidhiyya akifichua maovu yaliyokuwa yakifanywa na utawala wa Shah, jambo ambalo liliuchukiza sana utawala huo na kuamua kumtia nguvuni. Suala hilo liliwakasirisha sana wananchi wa Iran ambao waliamua kufanya maandamano ya kushinikiza kuachiliwa kwake mara moja.
Ili kukabiliana na wimbi la malalamiko hayo, utawala wa Shah uliamua kuwashambulia waandamanaji ambapo uliua na kuwajeruhi wengi kati yao.
Harakati hiyo ya mapambano ambayo inafahamika humu nchini kama Mapambano ya Tarehe 15 Khordad, kwa hakika ulikuwa mwanzo wa mapambano ya Mapinduzi ya Kiislamu ya wananchi shupavu wa Iran dhidi ya utawala wa kitaghuti wa Shah, mapambano ambayo yaliainisha mustakbali wa kisiasa na kijamii wa Iran.
Mapambano hayo yaliendelea kwa uongozi shupavu wa Imam Khomeini hadi Mapinduzi ya Kiislamu yalipofikia ushindi mwaka 1979.
Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, vita vya tatu vikuu kati ya utawala ghasibu wa Israel na nchi za Kiarabu vilianza.
Katika uvamizi wa kushtukiza na wa ghafla, ndege za kivita za Israel ziliingia katika anga ya nchi za Misri, Syria na Jordan na kushambulia kwa muda wa masaa mawili mfululizo majeshi na taasisi za anga za nchi hizo na kukaribia kuvitokomeza kabisa.
Baada ya hapo jeshi la nchi kavu la Israel lililokuwa likiungwa mkono na Marekani pamoja na Uingereza, kwa muda wa siku sita, lilivamia kwa silaha nzitonzito na za kisasa majeshi ya nchi tatu zilizotajwa za Kiarabu na kuyashinda kabisa.
Miaka 19 iliyopita Ronald Reagan, rais wa zamani wa Marekani aliaga dunia kutokana na ugonjwa wa kusahau wa Alzheimer.
Alizaliwa mwaka 1911 na kuhitimu masomo yake ya juu katika taaluma ya uchumi na masuala ya kijamii. Reagan alianza kufanya kazi kwenye redio na kisha akawa msanii kwenye televisheni.
Taratibu alianza kujishughulisha na masuala ya siasa ambapo kwanza alikuwa mwanachama wa chama cha Democrats na kisha kujiunga na chama cha Republicans.
Mwaka 1970 Ronald Reagan aliteuliwa na chama hicho kuwa gavana wa California na kisha mwaka 1980 akafanikiwa kuwa rais wa Marekani baada ya kumshinda mpinzani wake Jimmy Carter.
Katika kipindi cha uongozi wake wa miaka minane Reagan alitekeleza siasa za kijeshi na kichokozi dhidi ya nchi nyingine za dunia. Alianzisha mpango wa kijeshi wa Star Wars na kutoa amri ya kufanyika mashambulio ya kijeshi dhidi ya baadhi ya nchi. Pia alichochea na kuunga mkono kijeshi, kifedha, kipropaganda na kisiasa uvamizi wa utawala wa kidekteta wa Saddam Hussein wa Iraq dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.