Jun 05, 2023 21:59 UTC
  • Jumanne, tarehe 06 Juni, 2023

Leo ni Jumanne tarehe 17 Mfunguo Pili Dhilqaada 1444 Hijria sawa na tarehe 06 Juni 2023.

Siku kama ya leo miaka 1265 iliyopita Imam Mussa al Kadhim (as) ambaye ni miongoni mwa Ahlubait wa Mtume wetu Muhammad (saw) alibaidishwa na kupelekwa uhamishoni nchini Iraq kutoka Madina kwa amri ya mtawala dhalimu, Haroun Rashid. Mtukufu huyo aliwasili Iraq tarehe 7 Dhilhija 179 Hijria na kufungwa katika jela mji huo. Kwa muda, Imam aliwekwa katika jela ya Issa bin Ja'far aliyekuwa mtawala wa Basra, lakini mtawala huyo alimwandikia barua Haroun Rashid akimuomba amkabidhi Imam kwa mtu mwingine, kwa sababu hakupata ushahidi wowote dhidi ya mtukufu huyo. Haroun Rashid alimpeleka tena uhamishoni Imam mjini Baghdad na akamtaka waziri wake, Fadhl bin Rabi' amuue mjukuu huyo wa Mtume. Waziri huyo alikataa na hivyo Haroun alimtaka mtu aliyejulikana kwa jina la Yahya bin Khalid Barmaki atekeleze amri hiyo. Hatimaye Imam Kadhim (as) aliuuliwa shahidi na muovu huyo kwa amri ya mtawala Haroun Rashid.

Siku kama ya leo, miaka 224 iliyopita, alizaliwa Alexander Pushkin, malenga na mwandishi mkubwa wa Urusi mjini Moscow.

Pushkin, alipata umaarufu mkubwa mwaka 1820, baada ya kusambaza majmui ya kitabu kilichosheheni mashairi. Muda mfupi baadaye malenga huyo akatunga shairi lililohusu uhuru, suala lililopelekea kubaidishwa kwake.

Katika shairi hilo Alexander Pushkin alielezea kwa kina umuhimu wa uhuru.

Alexander Pushkin

 

Katika siku kama ya leo miaka 89 iliyopita alifariki dunia Ayatullahil Udhma Sheikh Abdulkarim Hairi Yazdi fakihi na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu ambaye aliasisi chuo kikuu cha kidini cha Qum.

Alimu huyo alizaliwa katika eneo la Yazd katikati mwa Iran na baada ya kupata elimu ya mwanzo alielekea nchini Iraq ili kuendelea na masomo ambako alipata elimu na maarifa kutoka kwa maulamaa maarufu wa zama hizo na kufikia daraja ya juu ya ijitihad.

Ayatullah Hairi Yazdi aliporejea Iran alihisi haja ya kuwepo chuo chenye nguvu cha elimu ya dini na kwa minajili hiyo mwaka 1340 Hijiria Shamsia alinzisha Hauza ya Qum ambayo ni chuo kikuu cha kidini katika mji huo mtakatifu. Hauza ya Qum ilipanuka kwa kasi na hivi sasa ni miongoni mwa vituo muhimu vya elimu katika ulimwengu wa Kiislamu.

Ayatullahil Udhma Sheikh Abdulkarim Hairi Yazdi

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kwa mara nyingine tena lilianzisha mashambulizi dhidi ya ardhi ya Lebanon.

Katika uvamizi huo, jeshi la Israel liliuvamia na kuudhibiti mji mkuu wa nchi hiyo, Bairut. Aidha askari hao wa utawala haramu wa Kizayuni, waliharibu miundombinu, viwanda na viunga vya mji huo, sanjari na kutekeleza jinai mbalimbali dhidi ya wakazi wake.

Uvamizi huo ulifanyika kwa kisingizio cha kudhamini usalama wa Wazayuni huko kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Mwezi Septemba mwaka huo huo, jeshi hilo likatekeleza mauaji ya umati dhidi ya wakimbizi wa Kipalestina katika kambi mbili za sabra nashatila karibu na mji mkuu wa Lebanona, Bairut. Hata hivyo mwezi Mei mwaka 2000, kufuatia ushindi wa wanamapamgano wa Hizbullah, wanajeshi vamizi wa Israel walilazimika kuondoka kwa madhila katika maeneo yote ya Lebanon waliyokuwa wameyakalia kwa mabavu.

Beirut mwaka 1982

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 6 Juni 1984, jeshi la India lilishambulia hekalu kubwa la Masingasinga lililojulikana kama Hekalu la Dhahabu katika mjini wa Amritsar makao makuu ya jimbo la Punjab, magharibi mwa India na kuua waasi wa Kisingasinga wasiopungua 1,000.

Serikali ya India ilidai kuwa shambulio hilo lilifanywa baada ya kupatikana habari za kufichwa silaha nyingi kwenye hekalu hilo, kwa shabaha ya kuanzisha uasi na mashambulizi dhidi ya serikali kuu.

Masingasinga hao nao walilipiza kisasi kwa kumuuwa Indira Ghandi, Waziri Mkuu wa India mwaka huohuo, kiongozi ambaye ndiye aliyetoa amri ya kushambuliwa hekalu hilo.

Hekalu la Dhahabu

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita tarehe 16 Khordad 1368 Hijria Shamsia, sawa na tarehe 6 Juni, mwaka 1989 mamilioni ya wananchi wa Iran waliokuwa na huzuni kubwa waliuzika mwili wa Imam Khomeini (MA) Mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, karibu na makaburi ya mashahidi wa vita vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran ya Kiislamu, ya Behesht az-Zahra (as), pambizoni mwa mji wa Tehran. Zaidi ya wananchi na Waislamu milioni kumi kutoka miji mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi walishiriki kwenye mazishi hayo ya kihistoria. Kabla ya hapo wananchi wa Iran, waliuaga mwili wa Imam Khomeini, katika eneo la Musalla hapa mjini Tehran, na baadaye kuelekea eneo la Behesht az-Zahra kwa ajili ya mazishi.

Mahali ulipozikwa mwili wa Hayati Imam Ruhullah Khomeini