Jun 15, 2023 05:52 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha (21)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 20 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Hii ni hikma ya 21.

قُرِنَتِ الْهَیْبَةُ بِالْخَیْبَةِ وَ الْحَیَاءُ بِالْحِرْمَانِ وَ الْفُرْصَةُ تَمُرُّ مَرَّ السَّحَابِ فَانْتَهِزُوا فُرَصَ الْخَیْرِ

Woga umefungamanishwa na kukata tamaa na haya imefungamanishwa na kujinyima na fursa hupita kwa kasi ya mawingu, hivyo tumieni fursa ya kutenda mema

Wasikilizaji wapenzi, Hikima hii ya 21 ya Nahjul Balagha, kama yalivyo maneno mengine ya Imam Ali (AS), maudhui yake ni yenye thamani kubwa. Kupitia hikma hii, Imam Ali AS anaashiria sababu tatu kuu za mtu kupoteza na kujinyima haki zake. Moja ya sababu hizo ni woga na hofu. Bila ya shaka, kuogopa mtu mambo na vitu hatari ni hali kimaumbile ambayo Mwenyezi Mungu amemuumba nayo mwanadamu, ili kumlinda. Ni maumbile ya mwanadamu kutumia neema ya hofu kujiondoa haraka kwenye eneo la hatari wakati anapokumbwa nayo kama vile kuvamiwa na mnyama hatari na matukio mengine yasiyo ya kawaida. Au kwa mfano mafuriko makubwa yanapotokea na mtu akawa yuko kwenye njia ya mafuriko hayo, moyo wake huingia hofu na kumfanya aondoke haraka sehemu hiyo. Yote hayo ni katika neema za Allah na ni katika faida za hofu. Lakini hofu na woga huo unapokuwa mkubwa kupindukia na unapofanywa kwa mambo yasiyostahiki kuwa na woga nayo, hapo wa kulaumiwa ni mtu anayeendekeza hofu na woga kama huo kwa kujinyima yeye mwenyewe baadhi ya neema za Mwenyezi Mungu. Mifano iko mingi , ikiwa ni pamoja na matukio yaliyotokea katika mapambano ya Imam Husain AS huko Karbala. Wengi waliogopa kumhami mjukuu wa Mtume na walimwacha Imam Husain (AS) peke yake. Hofu hiyo isiyo sahihi ya watu hawa iliwafanya wanyimwe neema kubwa ya kuuawa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu, kumhami Imam wa zama zao na kupata heshima ya milele.

Kuona haya, sawa kabisa na woga, nako kuna pande mbili, upande wa kulaumiwa na upande wa kusifiwa. Haya inayopasa kusifiwa ni ya mtu anayemuonea haya Muumba wake na nafsi yake na akajiepusha na kila kitendo kiovu na cha madhambi na kinachopingana na akili na sheria za Mwenyezi Mungu. Lakini haya inayopaswa kulaumiwa ni ya mtu anayeoona haya kumwabudu Mola wake kwa sababu wenzake watamuona hajastaarabika. Au kujiepusha na kujifunza sayansi na elimu, au kuuliza maswali juu ya mambo asiyoyajua, au kupigania haki yake mbele ya hakimu dhalimu n.k. Haya ya aina hiyo huitwa ni uzembe na husababisha hasara kwa wanadamu. Imepokewa Hadith kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) ambayo inasema: “Haya ziko za aina mbili. Haya ya busara na hikma na haya ya kipumbavu. Haya ya busara na hikma inatokana na ilmu na maarifa, lakini haya ya kipumbavu inatokana na ujahili na ujinga. 

Katika kipengee cha tatu cha hikma hii ya 21 ya Nahjul Balagha, Imam Ali AS anazungumzia umuhimu wa kutumia vizuri fursa zinazojitokeza na kusema: "Fursa hupita kwa kasi ya mawingu, basi tumia vizuri fursa za kutenda mema. 

Fursa ina maana ya kuwa tayari suhula na sababu zote za kutenda jambo zuri. Ni kama vile mazingira yote kuwa yameandaliwa kwa ajili ya kutafuta ilmu lakini mtu akapoteza fursa hiyo licha ya kwamba ni mzima wa mwili, ana akili timamu, nzuri na kipaji. Mwalimu bingwa na mstahiki yuko tayari kumfundisha na mazingira mazuri ya kielimu yapo kwake lakini akapoteza fursa hiyo. Fursa hutokea katika masuala tofauti lakini hazidumu, hutoweka kwa kutokea mabadiliko madogo tu, hivyo mwenye hikma hutumia vizuri fursa anazopata. 

Alaakullihaal, neema zote za Mwenyezi Mungu alizowekewa mwanadamu hapa duniani kama fursa ya ujana, afya, usalama, uzima wa kiroho na kiakili bali pia umri na maisha ya mwanadamu ni katika fursa zinazopita haraka sana, na ikiwa hatutazitumia vizuri fursa hizo, matokeo yake ni majuto na kusaga meno.

Tags