Sura ya Qaaf, aya ya 38-45 (Darsa ya 953)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 953 na sura tunayoizungumzia kwa sasa ni ya 50 ya Qaaf. Tunaianza darsa yetu ya leo kwa aya yake ya 38 hadi ya 40 ambazo zinasema:
وَلَقَدْ خَلَقْنَا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ وَمَا مَسَّنَا مِن لُّغُوبٍ
Na bila ya shaka tumeziumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina ya viwili hivyo mnamo siku sita; na wala haukutugusa uchovu.
فَاصْبِرْ عَلَىٰ مَا يَقُولُونَ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ الْغُرُوبِ
Basi vumilia kwa hayo wasemayo, na mtakase kwa kumsifu Mola wako Mlezi kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuchwa.
وَمِنَ اللَّيْلِ فَسَبِّحْهُ وَأَدْبَارَ السُّجُودِ
Na katika usiku pia mtakase, na baada ya kusujudu.
Katika darsa iliyopita tulibainisha nukta kadhaa kuhusu kujiri kwa Kiyama na kuhusu wakanushaji wa tukio hilo zito na adhimu. Aya hizi tulizosoma zinazungumzia tena qudra na uwezo wa Allah SWT na kueleza kwamba: vipi watu wanakuwa na shaka ya kujiri kwa Kiyama, ilhali ulimwengu huu uliopo pamoja na adhama na ukubwa wake wote uliumbwa na Yeye Mola kwa muda wa siku sita; na kuumbwa kwake hakukumchosha Yeye wala kumpa tabu na usumbufu wowote! Kisha baada ya maelezo hayo, Mwenyezi Mungu Mtukufu anamhutubu Mtume wake kwa kumwambia: usiudhike wala usihuzunishwe na kutiwa unyonge na maneno ya wakanushaji wa kufufuliwa viumbe, bali iimarishe subira na ustahamilivu wako na zivumilie kauli zao kwa kumdhukuru na kumkumbuka Mola wako, katika nyakati mbalimbali za usiku na mchana. Baadhi ya tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kwamba, japokuwa Allahu Jalla Fii U’laahu alikuwa na uwezo wa kuumba ulimwengu wote wa viumbe kwa lahadha moja tu ya kufumba na kufumbua, lakini anaelezea na kutilia mkazo kuumbwa kwa ulimwengu hatua kwa hatua ili kubainisha kwamba mfumo na kanuni ya sababu na visababishi ndiyo inayotawala katika uendeshaji wa ulimwengu huo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, ulimwengu wa viumbe ni mpana na mkubwa mno. Adhama ya ulimwengu huu inadhihirisha na kuonyesha kwa uwazi kabisa qudra na uwezo usio na ukomo wala mpaka wa Allah SWT. Aidha, aya hizi zinatuusia kwamba, tuhuma, kauli chafu na kusemwa vibaya na wapinzani visiwe sababu ya sisi kulegalega na kurudi nyuma katika msimamo wetu wa kuibainisha haki, bali tuendelee kushikamana na njia yetu ya kuitangaza kwa juhudi na uthabiti na kwa subira na uvumilivu. Halikadhalika, aya hizi zinatuonyesha kuwa kumdhukuru na kumkumbuka Allah katika saa na nyakati zote ndio nguzo na msukumo bora wa kutupa subira na uvumilivu wa kuhimili matatizo na misukosuko. Vilevile aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba, japokuwa Mwenyezi Mungu SWT hafungiki na muda, lakini kuna nyakati maalumu za Sala ambazo zina taathira kubwa, fadhila nyingi na utukufu zaidi.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 41 hadi 44 ya sura yetu ya Qaaf ambazo zinasema:
وَاسْتَمِعْ يَوْمَ يُنَادِ الْمُنَادِ مِن مَّكَانٍ قَرِيبٍ
Na sikiliza siku atapo nadi mnadi kutoka pahala karibu.
يَوْمَ يَسْمَعُونَ الصَّيْحَةَ بِالْحَقِّ ۚ ذَٰلِكَ يَوْمُ الْخُرُوجِ
Siku watakapo sikia ukelele wa haki. Hiyo ndiyo siku ya kutoka (makaburini).
إِنَّا نَحْنُ نُحْيِي وَنُمِيتُ وَإِلَيْنَا الْمَصِيرُ
Hakika Sisi tunahuisha na tunafisha, na kwetu Sisi ndio marejeo.
يَوْمَ تَشَقَّقُ الْأَرْضُ عَنْهُمْ سِرَاعًا ۚ ذَٰلِكَ حَشْرٌ عَلَيْنَا يَسِيرٌ
Siku itapo wapasukia ardhi upesi upesi! Mkusanyo huo kwetu ni mwepesi.
Aya hizi zinasimulia yatakayojiri wakati wa ufunguzi wa kongamano zito na adhimu la Siku ya Kiyama ambalo litaanza kwa mahudhurio na mkusanyiko wa umati usio na kifani wa walimwengu na kwa mlingano wa mbinguni wa Allahu Jalla Jalaaluh. Mlingano na wito huo wa mbinguni utasambaa na kuenea kwenye anga kiasi cha kusikika kwa karibu mno na kila atakayehudhurishwa kwenye mkusanyiko huo wa siku ya kufufuliwa viumbe. Adhama ya mlingano huo itakuwa kubwa mno kiasi cha kuifanya milima na ardhi ipasuke, wafu watoke makaburini na watu wote waliotawanyika huku na kule wakusanyike wote mahala pamoja. Katika aya hizi tulizosoma, imegusiwa pia nukta kwamba, Mungu yuleyule ambaye aliwaumba watu mara ya kwanza hapa duniani kisha akawafisha, ndiye huyohuyo atakayewafufua tena siku hiyo ili waendelee kufuata njia inayoendana na lengo la kuumbwa kwao. Miongoni mwa mafunzo tunayopata katika aya hizi ni pamoja na mosi: Maadi, yaani kufufuliwa kwa viumbe ni tukio la kimwili. Mwanadamu mmoja mmoja atafufuka na kutoka ardhini na kuhudhurishwa kwenye uwanja wa Kiyama. Na pili ni kuwa uhai na mauti yako kwenye mamlaka ya Mwenyezi Mungu peke yake na hii ni hoja madhubuti zaidi ya kuonyesha uwezekano wa wafu wote kufufuliwa tena na Yeye Mola Siku ya Kiyama.
Darsa yetu hii inahitimishwa na aya ya 45, ambayo ndiyo aya ya mwisho ya Suratu-Qaaf isemayo:
نَّحْنُ أَعْلَمُ بِمَا يَقُولُونَ ۖ وَمَا أَنتَ عَلَيْهِم بِجَبَّارٍ ۖ فَذَكِّرْ بِالْقُرْآنِ مَن يَخَافُ وَعِيدِ
Sisi tunajua sana wayasemayo. Wala wewe si Jabari juu yao. Basi mkumbushe kwa Qur'ani anaye ogopa onyo (langu).
Aya hii inaendeleza yaliyozungumziwa katika aya zilizotangulia; na kwa mara nyingine inamhutubu Bwana Mtume SAW na kumwambia: sisi tunayajua wayasemayo wakanushaji wa kufufuliwa kwa viumbe katika kuukadhibitsha wito wako na namna wanavyowazuia watu wengine wasikuamini; lakini usiwe na matarajio kwamba watu wote watakuamini na kuifuata haki, kwa sababu tumemuumba na kumfanya mwanadamu kiumbe huru na kumpa haki ya kuchagua. Wajibu wako wewe ambaye ni Mtume ni kufikisha ujumbe na wito wa Mola wako na kuwapa indhari watu juu ya hatima ya matendo na amali zao. Wewe hujatumwa umlazimishe mtu yeyote aikubali dini kwa nguvu na kumshurutisha kwamba lazima auamini na kuukubali wito wako. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kwa kuwa Qur’ani ndio wenzo bora wa ukumbusho, msingi mkuu wa mawaidha ya kiakhlaqi na utoaji maonyo na indhari kwa watu inapasa uwe ni aya za Qur’ani, si kauli za kiutashi zinazotokana na ubunifu wa watu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, usuli na misingi ya dini za mbinguni inaendana na fitra na maumbile na imejengwa ndani ya nafsi za wanadamu wote. Kitu pekee kinachohitajika ni ukumbusho. Na kwa hiyo, kinachotekelezwa na Mitume wa Allah ni kufanya jitihada na idili ya kuiamsha fitra na maumbile hayo ya wanadamu yaliyofichika na kusahaulika kwa kutumia mbinu ya maonyo na indhari. Vilevile aya hii inatutaka tuelewe kwamba jukumu na wajibu wa Mitume ni kuitangaza na kuieneza dini, si kumlazimisha na kumshurutisha mtu yeyote, kwa sababu dini inatakiwa ikubaliwe na kufuatwa kwa matakwa na hiari yake mtu. Wa aidha tunajifunza kutokana na aya hii kwamba, kuwa na imani ya kuthibiti ahadi za Mwenyezi Mungu juu ya malipo ya thawabu na adhabu Siku ya Kiyama kunaziandalia nafsi mazingira mazuri ya kuzikubali nasaha na mawaidha ya Manabii wa Allah. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 953 ya Qur’ani imefikia tamati na ndio iliyotukamilishia pia tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura ya 50 ya Qaaf. Inshallah tuwe tumeaidhika na kunufaika na yote tuliyojifunza katika sura hii. Tunamwomba Allah azifanye thabiti imani zetu, atughufirie madhambi yetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/