Ijumaa, Juni 30, 2023
Leo ni Ijumaa tarehe 11 Mfunguo Tatu Dhulhija 1444 Hijria, sawa na tarehe 30 Juni 2023 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 103 iliyopita, yalianza mapambano ya raia wa Iraq chini ya uongozi wa Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Shirazi dhidi ya wavamizi wa Uingereza. Itakumbukwa kuwa baada ya kumalizika Vita vya Kwanza vya Dunia na kufuatia makubaliano ya waitifaki wa vita hivyo juu ya kugawana utawala wa Othmania, uongozi na usimamizi wa Iraq, Jordan na Palestina ulikabidhiwa mkoloni Mwingereza. Kuanzia wakati huo ukoloni wa London ukaanza rasmi kupora vyanzo na utajiri mkubwa wa nchi hizo. Baada ya kubainika makubaliano hayo ya kugawana mataifa ya Waislamu, kuliibuka mapinduzi makubwa katika maeneo yote ya Iraq. Aidha baada ya Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Shirazi kutoa fatwa ya jihadi, raia wa nchi hiyo walisimama kukabiliana na ukoloni huo wa Uingereza dhidi ya nchi yao. Hata hivyo kutokana na uungaji mkono mkubwa wa madola ya kikoloni ya Magharibi kwa Uingereza na kadhalika njama mbalimbali za adui, mapinduzi hayo ya wananchi hayakuweza kufikia malengo yake makuu na badala yake Faisal Hussein akateuliwa kuwa mfalme wa Iraq.
Siku kama ya leo miaka 63 iliyopita Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (Zaire ya zamani) ilijitangazia uhuru na Joseph Kasavubu akawa rais wa nchi hiyo, huku Patrice Lumumba akiwa Waziri Mkuu. Kongo ilikoloniwa na Ubelgiji. Mapambano ya kudai uhuru yaliyoongozwa na Patrice Lumumba yalishika kasi katika miaka ya mwisho ya kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia na kupelekea nchi hiyo kujipatia uhuru wake. Hata hivyo baada ya Kongo kupata uhuru zilianza harakati nyingi za uasi zilizokuwa zikiungwa mkono na Ubelgiji. Katika upande mwingine kulishadidi mapigano kati ya Lumumba na Musa Chumbe kiongozi aliyekuwa akiungwa mkono na Ubelgiji. Hatimaye mnamo mwaka 1965 Jenerali Mobutu Sese Seko aliyeungwa mkono na Marekani alifanya mapinduzi ya kijeshi na kutwaa madaraka ya nchi hiyo ambapo badaye alianza kuwakandamiza wananchi masikini wa Kongo.
Miaka 34 iliyopita katika siku kama ya leo, Jenerali Omar Hassan Ahmad Al Bashir wa Sudan aliongoza mapinduzi ya kijeshi na kuuangusha utawala wa Swadiq Al Mahdi bila ya umwagaji damu. Utawala huo ulikuwa ukikabiliwa na matatizo mbalimbali ya ndani. Baada ya mapinduzi hayo Omar Hassan Al Bashir kwa kushirikiana na Hassan Al Turabi alianzisha chama cha Kongress ya Kitaifa huku yeye akiwa mwenyekiti wa chama hicho na rais wa nchi. Baada ya Al Bashir kutwaa urais alijitahidi kujitenga na siasa za Marekani, hatua ambayo iliipelekea serikali ya Washington kuichukia Khartoum na kuchukuua hatua za kiaduai dhidi ya serikali ya Al Bashir. Miongoni mwa hatua za kiadui zilizochukuliwa na Marekani dhidi ya Sudan ni kuwaunga mkono waasi wa Kusini mwa Sudan ambapo mwaka 2011 eneo hilo la kusini lilijitenga na Sudan na kujitangazia uhuru wake. Hata hivyo al Bashir alibadilisha mielekeo yake na kuwa tegemezi kwa utawala mwa kifalme wa Saudi Arabia. Utawala wa al Bashir ulitafunwa na ufisadi, utumiaji mbaya wa madaraka, hali mbaya ya uchumi na kufuata kibubusa sera za Saudi Arabia katika vita vya Yemen. Mambo haya yaliwakasirisha Wasudani walioanzisha harakati ya upinzani dhidi ya al Bashir na hatimaye tarehe 11 Aprili mwaka 2019 kiongozi huyo alilazimika kung'atuka madarakani na kutiwa nguvuni kwa tuhuma za ufisadi na utakatishaji wa fedha chafu. Omar al Bashir anatumikia adhabu ya kifungo.
Na katika siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, mfumo wa utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini ulihitimishwa. Kuanzia mwaka 1948, wazungu walio wachache nchini Afrika Kusini walianza kutekeleza siasa za kibaguzi dhidi ya wazalendo weusi. Kwa mujibu wa siasa hizo, wazungu waliokuwa wakiunda asilimia 20 tu ya wananchi wa Afrika Kusini walihesabiwa kuwa jamii bora zaidi na iliyokuwa na nafasi muhimu katika uendeshaji wa masuala ya nchi hiyo. Sheria za kibaguzi kama vile za kupiga marufuku watu weusi kuoana na watu weupe na vilevile kushiriki katika harakati za kisiasa ni baadhi tu ya sheria za kibaguzi zilizotekelezwa na makaburu nchini Afrika Kusini. Siasa hizo ziliwakasirisha mno walimwengu na nchi nyingi duniani kukata uhusiano na utawala huo.