Msikiti, Dhihirisho la Utambulisho wa Uislamu (Maalumu Siku ya Msikiti Duniani)
Mwaka 2003, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilipendekeza katika mkutano wa 30 wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Kiislamu mjini Tehran, kwamba kutokana na nafasi muhimu ya misikiti katika kuimarisha umoja na mshikamano wa Waislamu, iainishwe siku moja kuwa Siku ya Kimataifa ya Msikiti.
Baada ya pendekezo hilo, washiriki wa mkutano huo waliidhinisha kwamba, tarehe 21 Agosti ya kila mwaka ambayo ni siku ya kumbukumbu ya jinai iliyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuchoma moto Msikiti wa Al-Aqsa, ipewe jina la "Siku ya Msikiti Duniani". Katika azimio hilo, nchi za Kiislamu zilitakiwa kuheshimu nafasi ya misikiti na kuilinda kama eneo takatifu la imani ya Tauhidi na kumwabudu Mungu Mmoja.
Tarehe 21 Agosti 1969, Msikiti wa Al-Aqsa, kibla cha kwanza cha Waislamu na kituo cha Mitume na Mawalii wa Mwenyezi Mungu, ulichomwa moto na Mzayuni katika kitendo cha uadui ili kufuta athari na turathi za kihistoria na kidini za msikiti huo mtukufu. Baada ya hapo, Wazayuni wameendelea kushambulia na kuchafua eneo hilo takatifu ili kuandaa njia ya kuliharibu kikamilifu. Kitendo cha Wazayuni cha kuchoma moto Msikiti wa Al-Aqsa kilikabiliwa na hisia kali kutoka kwa Waislamu na wanazuoni wa kidini duniani kote. Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuhusu jinai ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuchoma moto Msikiti wa Al-Aqsa kwamba: “Tukio la kuchomwa moto Msikiti wa Al-Aqsa linaonyesha muelekeo wa kudumu wa ulimwengu wa kibeberu dhidi ya madhihirisho ya utambulisho wa Kiislamu, na kwa sababu hii, linapaswa kubaki hai katika akili na fikra za Waislamu."

Msikiti ni alama na nembo muhimu zaidi ya Uislamu katika kila mji na nchi, sawa za Kiislamu au zisizo za Kiislamu. Kila siku, Waislamu huelekea kwenye misikiti kufanya ibada yao kuu zaidi, yaani Swala; na katika maeneo hayo matakatifu, humuomba na kunong'ona na Mola wao Mlezi wakiwa katika safu zilizonyooka na zenye mpangilio makhsusi. Tunasoma katika Aya ya 18 ya Suratul Jinn kwamba:
وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّهِ فَلا تَدْعُوا مَعَ اللَّهِ أَحَدًا
“Na hakika misikiti ni ya Mwenyezi Mungu, basi msimuombe yeyote pamoja na Mwenyezi Mungu." Mtume Muhammad (saw) pia anasema katika Hadithi Qudsyy kuhusu umuhimu wa msikiti kwamba, Mwenyezi Mungu SW amesema:
قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اَللَّهُ عَلَیْهِ وَ آلِهِ : قَالَ اَللَّهُ تَبَارَکَ وَ تَعَالَى إِنَّ بُیُوتِی فِی اَلْأَرْضِ اَلْمَسَاجِدُ تُضِیءُ لِأَهْلِ اَلسَّمَاءِ کَمَا تُضِیءُ اَلنُّجُومُ لِأَهْلِ اَلْأَرْضِ أَلاَ طُوبَى لِمَنْ کَانَتِ اَلْمَسَاجِدُ بُیُوتَهُ
"Misikiti ndiyo nyumba zangu katika ardhi, huviangazia vilivyoko mbinguni kama nyota zinavyowaangaza watu wa ardhini. Hakika wamebarikiwa wale ambao nyumba zao ni misikiti.." Kwa sababu hiyo, Uislamu umelipa umuhimu na nafasi maalumu suala la ujenzi wa misikiti na kuhudhuria maeneo hayo kwa ajili ya ibada na kadhalika.
Miongoni mwa mambo yanayoupa umuhimu mkubwa msikiti ni kwamba katika kipindi chote cha historia tangu mwanzo wa Uislamu, maeneo hayo hayajawahi kuzingatiwa kuwa ni sehemu takatifu ya ibada pekee. Bali, ushahidi wa kihistoria unaonyesha kuwa, misikiti imekuwa chombo muhimu zaidi cha kukuza na kusambaza ujumbe na neno la Mungu, maadili mema na mafundisho ya kidini kutokana na sifa zake maalumu. Ingawa, kwa kawaida, misikiti huzingatiwa kwanza kama mahali patakatifu na vituo vya ibada na shughuli za kidini, lakini pia hatuwezi kupuuza kazi zake muhimu za kielimu na kitamaduni katika kipindi chote cha historia.
Ili kufikisha ujumbe wake wa uokovu kwa watu na kuwaongoza kwenye njia iliyonyooka, Mtume (SAW) alipanua wigo wa wito wake kwa kutumia msikiti wa kwanza uliojengwa Madina. Msikiti huo wa kwanza ulikuwa kitovu cha elimu, ulinganiaji, kutoa hukumu na kukata kesi baina ya watu, na kupanga mambo ya kisiasa, kijeshi na kiutamaduni. Baada ya Mtume, Imam Ali bin Abi Twalib (as) pia alifuata nyayo za mtukufu huyo katika mfumo wake wa elimu na malezi. Katika kipindi hicho, shughuli za kisayansi na kielimu zilifanyika msikitini. Katika mikutano mbalimbali, Imamu Ali (AS) alifundisha maarifa ya Kiislamu katika vikao vilivyokuwa vikifanyika msikitini na alikuwa akiketi msikitini kufanya midahalo na mijadala ya kisayansi na kielimu. Hali hiyo iliendelezwa na wafuasi wa Ahlul Bait (AS) baada ya kuuliwa shahidi Imam Ali bin Abi Twalib (AS), na taratibu misikiti, shule na maktaba zilianzishwa huko Baghdad na katika maeneo menginezo ya Ulimwengu wa Kiislamu.
Kuhusiana na msikiti na utambulisho unaowapa Waislamu, Ayatullah Ali Khamenei anasema: "Kujenga msikiti, kwanza huko Quba na kisha Madina, ni mojawapo ya mipango na ubunifu mzuri na bora zaidi wa Uislamu katika zama za mwanzoni mwa uundaji wa jamii ya Kiislamu. Msikiti ulikuwa Nyumba ya Mwenyezi Mungu na nyumba ya watu, eneo la watu kunong'ona na Mola wao na makutanio ya umati wa watu, kituo cha dhikri na kupaa kiroho na wakati huo huo uwanja wa elimu, jihadi na mipango ya kidunia mahali pa ibada na kituo cha kupanga sera na siasa; mambo haya yaliyofanyika kwa pamoja msikitini, yanawakilisha sura ya msikiti wa Kiislamu, na kuonyesha tofauti ya maeneo ya ibada ya Waislamu na maeneo ya ibada za dini nyingine... Msikiti ni dhihirisho la mfungamano wa dunia na Akhera na muungano wa mtu binafsi na jamii katika mtazamo na fikra za Kiislamu. Kwa mtazamo huu, mioyo yetu inakwenda mbio kwa ajili ya msikiti na kujawa na shauku na hisia ya uwajibikaji….
Takwimu za ongezeko la watu waliosilimu katika nchi za Magharibi zimekuwa zikichapishwa kila mwaka. Harakati na vuguvugu la Waislamu katika jamii za Kimagharibi na nafasi ya misikiti katika kukuza utamaduni adhimu wa Uislamu, kama dini inayomtengeneza binadamu, kumkamilisha, na kumfanya mpenda amani na uadilifu, vinaweza kuonekana vyema zaidi katika maneno Waislamu wapya. Shin Gaimon, kijana wa Kijapani aliyesilimu hivi karibuni, anasimulia kisa cha kusilimu kwake akisema: “Wakati nilipoweka mgu wangu ndani ya msikiti wa mji wa Morgan, jambo la kwanza nililohisi lilikuwa amani. Kwa sababu viatu vinavuliwa kabla ya kuingia msikitini, na hata kutembea msikitini hakuvurugi amani yake, na roho ya utulivu ilihisika kila kona ya msikiti. Dhana ya rehma na wema wa Mwenyezi Mungu katika Uislamu ilikuwa na taathira kubwa kwangu na ilibadili mtazamo wangu kuhusu Uislamu. Wakati tunaposwali, ni kana kwamba Mwenyezi Mungu amesimama mbele yetu na tunazungumza naye moja kwa moja; matokeo yake, tunajifunza kuhudhurisha fikra na moyo na kujaribu kufika kwenye amani ya kweli na kuondoa wasiwasi katika dhati na nafsi zetu."
Kwa hakika, inatupasa kusema kuwa, misikiti ni maeneo muhimu sana ya kidini yanayofanya kazi nyingi zinazohusiana na afya ya akili na nafsi. Utafiti umeonyesha kuwa, kuhudhuria msikitini kunaweza kuwa na ufanisi mkubwa katika kuondoa matatizo kama vile upweke, huzuni, msongo wa mawazo na hata tabia ya kujitenga na watu. Mikusanyiko ya kidini katika misikiti, ambako Waislamu hufanya kazi na shughuli zao kwa umoja, huimarisha uhusiano wao wa kihisia na kujenga ukaribu zaidi baina yao. Kuepuka tabia ya kujitenga na watu, kuondokana na huzuni za maisha, na kujisikia kuwa na nguvu katika ushirikiano na muawana na Waislamu wenzako, yote haya ni sehemu ya matibabu ya kisaikolojia, ambayo yanaweza kupatikana kwa kuhudhuria msikitini chini ya mwanga wa ibada ya Swala na kunong'ona na Mola Muumba, kandokando ya watu wema na wenye imani.
Kama tujuavyo sisi sote, programu kuu na muhimu zaidi ya kidini inayofanyika misikitini ni ibada ya Swala. Ibada hiyo ni aina ya maombi kwa Mwenyezi Mungu ambayo hufanywa kwa pamoja na kwa utaratibu maalumu, kwa njia ya harakati zenye maana makhsusi za kimwili na kiroho. Mahudhurio ya Waislamu misikitini na kutekeleza ibada hiyo kwa pamoja, huwafanya wajihisi kwamba, wote wako chini ya uangalizi na upendo wa Mola wao Mlezi.
Katika upande mwingine misikiti inalea kizazi chenye imani na wanamapinduzi waliojipamba kwa sifa na maadili mema, ambao ndio msingi wa harakati za mapambano dhidi ya dhulma na uonevu kote duniani. Kwa maneno mengine ni kuwa, msikiti ni ngome ya mapambano dhidi ya njama za maadui, na handaki za kulinda thamani na matukufu ya kibinadamu. Kwani, hotuba na mafundisho yanayotolewa na maimamu wa jamaa katika Swala za kila siku, Swala za Ijumaa na hata Idi, mara nyingi huwatambulisha maadui wa Uislamu na kuweka wazi njia za kubatilisha njama na mipango yao. Vilevile, misikiti katika utamaduni wa Kiislamu, inatambuliwa kama vituo vya huduma kwa manufaa ya umma. Kuanzisha taasisi za kutoa karadha njema, kutoa mikopo kwa wahitaji, huduma za ushauri nasaha, na kutoa misaada kwa familia maskini na zenye matatizo ni miongoni mwa mambo ambayo hufanywa misikitini. Shughuli hizi, sambamba na kuimarisha moyo wa ukarimu na upendo miongoni mwa watu, zinasaidia pia katika kuboresha afya ya akili na nafsi za waumini.