Krismasi 2024 na Zawadi za Damu
Mwaka huu mpya wa 2024 ulianza tofauti na miaka yote iliyopita. Katika ukumbusho wa kuzaliwa Nabii Isa Masih, mji wa Bait Laham (Bethlehem), mahali alikozaliwa Mtume huyo wa Mungu, uligubikwa na kimya na hali ya huzuni na majonzi, badala ya sherehe na shamrashamra.
Hii ni kwa sababu kiwingu cheusi cha mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel huko Gaza kilikuwa kizito kwenye Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na katika kanisa la Nativity, au Basilica of the Nativity, mahali alipozaliwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, Isa Masihi (as). Wiki kadhaa kabla, makanisa yalitangaza kwamba yako kwenye maombolezo ya watu wa Gaza waliouawa katika mashambulizi ya Israel, na kwamba mwaka mpya wa 2024 hakutakuwa na mapambo ya Krismasi kwenye mti mkubwa wa msonobari katika uwanja wa eneo hilo la kale la mji wa Yerusalemu, na wala mishumaa haitawashwa kwa ajili ya sherehe ya kuzaliwa Isa Masia.
Mwaka huu Wakristo wanaoishi Ukingo wa Magharibi huko Palestina, kinyume na ada ya miaka iliyopita, waliweka masanamu na rosari zao takatifu kati ya vifusi na seng'enge ili kuonyesha mshikamano wao na watu wa Gaza wanaoendelea kuuawa kikatili.

Umm Shadi, mwanamke Mkristo wa Kipalestina, alionekana akiwa amekaa peke yake katika nyumba yake huko Bethlehemu. Hakukuwa na athari za mapambo ya Sikukuu ya Krismasi katika kona za nyumba yake, na badala ya kufurahi kutokana na kuwadia sikukuu hiyo, alikuwa akitazama picha za jamaa zake wa Ukanda wa Gaza, ambao wameuawa shahidi katika mashambulizi ya Israel. Umm Shadi anasema: “Sikukuu ya Krismasi haina maana wakati watu wetu wanaendelea kuuliwa huko Gaza kwa sababu tunaomboleza na kuhuzunika. Hakuna mtu anataka kusherehekea Krismasi katika hali kama hii, wakati watoto wa Gaza wanasumbuliwa na njaa na hofu."
Umm Shadi aliadhimisha siku ya kuzaliwa Yesu Kristo kwa wasiwasi na huzuni, huku akiomboleza kuuawa shahidi baadhi ya jamaa zake katika mashambulizi ya Israel huko Gaza; na kama ishara ya mshikamano wake na Wapalestina wenzake, Waislamu na Wakristo, ameamua kutosherehekea kabisa sikukuu hiyo.
Wapalestina wengi walizingirwa na vikosi vya jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika kanisa la Mtakatifu Porphyrus katika mji wa Gaza, wakati wanajeshi hao walipokuwa wakivunja na kuiharibu nyumba za raia na kuua watu karibu na kanisa hilo. Wanawake na watoto wadogo walinyimwa huduma za matibabu, maji, chakula na kadhalika.
Katika kipindi chote cha zaidi ya miezi mitatu iliyopita, maelfu ya mabomu na makombora yamemiminwa juu ya vichwa vya watu wa Gaza kwa ndege za kivita za Kimarekani zinazotumiwa na jeshi la Israel. Katika kipindi hicho cha Krismasi, mashambulizi ya Wazayuni dhidi ya watoto wa Kipalestina, wanawake na wanaume raia wa kawaida, yalikuwa makali sana kiasi kwamba Wakristo wengi wanaoishi katika ardhi hiyo hawakutambua hata kuwasili kwa mwaka mpya. Wakati mikokoteni ya Krismasi katika siku za kusherehekea mwaka mpya wa Miladia, zilikuwa zikigawa zawadi kwa watu wa nchi mbalimbali hususan za Kikristo duniani, huko Gaza raia walikuwa wakiburuta mikokoteni, matoroli na hata wanyama kama punda na farasi kubeba maiti za watoto, wanawake na wanaume waliokuwa wamezama katika damu baada ya kuuliwa shahidi katika mshambulizi ya Israel.

Serikali za nchi za Magharibi zilipuuza maafa yanayofanyika Ukanda wa Gaza katikati ya sherehe za Krismasi, wakati ambao kila mwaka mji wa Bethlehem, mahali alipozaliwa Yesu Kristo, katika Ukingo wa Magharibi huko Palestina, hushuhudia mahudhurio makubwa ya Wakristo kutoka maeneo mbalimbali ya dunia. Kinyume chake, katika siku hizo, walimwengu wameshuhudia mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Gaza yanayoendelea kufanywa hadi sasa na utawala wa Kizayuni wa Israel unaoungwa mkono na kusaidiwa na nchi za Magharibi.
Tangazo la uungaji mkono wa kisiasa na kijeshi wa viongozi wa nchi za Magharibi kwa utawala wa Kizayuni limezuia kupitishwa maazimio ya kusitisha vita huko Gaza katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Matokeo ya jinai na mauaji hayo ya halaiki ni kuuawa shahidi zaidi ya Wapalestina elfu 23 wakiwemo maelfu ya watoto na wanawake, zaidi ya elfu 60 kujeruhiwa na kuharibiwa zaidi ya asilimia 70 ya majengo ya mji wa Gaza. Ni kana kwamba maneno ya Yesu Kristo hayasikilizwi tena katika dunia ya sasa. Nabii huyo mwema wa Mwenyezi Mungu alikuwa akiwaambia wafuasi wake kwamba: wasiwe kama watawala madhalimu. Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu alileta ujumbe wa kuwapenda wanadamu wengine na alifanya jitihada kubwa za kutekeleza uadilifu na kupiga vita dhulma. Daima alikuwa akisimama baina ya wafuasi wake na kuwalingannia watu upendo, kujiepusha na dhulma na uonevu. Katika Qur'ani Tukufu, Suratu Maryam, Aya za 31 na 32, Isa Masia (AS) anajitambulisha kuwa ni kiumbe aliyebarikiwa popote pale awapo, ni kwamba ameusiwa kumtendea mema mama yake, na asiwe jabari na mtu muovu.
Imeelezwa katika mafundisho ya Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu kwamba: “Kwa haki nawaambia, chumba kikishika moto, moto huo utaenea kutoka chumba kimoja hadi kingine mpaka vyumba vingi vitakapoungua; isipokuwa pale watakipata chumba cha kwanza na kukiondoa kabisa; wakati huo hakutakuwa tena na mahali pa moto. Hayo ndiyo maafa ya dhalimu wa kwanza ambaye akizuiliwa, hakutakuwa na kiongozi dhalimu baada yake…. Kama ambavyo iwapo moto haupati kuni na ubao katika nyumba ya kwanza, hautaunguza chochote."
Nora, mwanamke wa Kikristo wa Palestina, anasema: Kristo alikuja baina ya wanadamu na kwa kuja kwake, alieneza upendo na urafiki na kuweka mikono yake juu ya vichwa vya watu maskini na waliokandamizwa. Wakati wote wa kuwepo kwake baina ya wanaadamu hakusita kupambana na uovu na kulingania wema. Lakini sasa hakuna jema lolote, na uhalifu na uovu umefika kileleni.
Kinachojiri hii leo huko Gaza ni matokeo ya ukatili na jinai za miaka 75 za utawala bandia wa Israel.
Takriban watu milioni 2 wakazi wa Gaza ni Waislamu, na zaidi ya Wakristo wa Orthodox 10,000 pia wanaishi katika eneo hilo. Wakristo wa dhehebu hili husherehekea kuzaliwa kwa Isa Masia tarehe 7 Januari.
Leo, Gaza ni uwanja wa mpambano baina ya haki na batili. Ni medani ya vita baina ya ubeberu na imani, na baina ya nguvu ya imani dhidi ya nguvu ya giza. Nguvu ya ubeberu inayotumia mashinikizo ya kijeshi, inaendeleza mashambulizi ya mabomu na kufanya uhalifu wa kivita, na nguvu ya imani, ambayo kidhahiri inaonekana haina zana sawa za kijeshi, inasimama kidete na silaha na zana chache sana lakini kwa imani na azma thabiti. Leo hii jamii ya wanadamu inatazama taswira ya ajabu ya imani na kusimama kidete kwa watu ambao nyumba zao zinharibiwa na wapendwa wao wanauawa kikatili kutokana na mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni wa Israel, lakini wote -watu wazina na watoto- wanakariri kwa ndimi na utulivu, kamili wakisema: Hasbuna Allah wa Niimal-Wakil (Mwenyezi Mungu anatutosha, Naye ni mbora wa kutegemewa).
Leo, dhamiri ya ubinadamu na binadamu huru wanaumizwa na jinai na ukatili huu wa kutisha. Kwa mujibu wa Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu: "Kwa wakisimama kidete, subira na kwa kutojisalimisha, watu wa Gaza, wameondoa nikabu na barakoa kwenye nyuso za uongo wa eti kutetea haki za binadamu wa nchi kama Marekani, Ufaransa na Uingereza zimefedheheshwa. Watu wa Gaza wanafikisha ujumbe kwa ulimwengu kwamba mlingano wa nguvu umebadilika sana katika mapambano ya kambi ya Muqawama na utawala ghasibu wa Israel na kuna matumaini kuwa mwaka huu mpya wa 2024 utaambatana na kurejea watu kwenye mafundisho ya Mitume wa Mwenyezi Mungu kama Ibrahim, Nuhu, Musa, Isa na Muhammad (amani ya mwenyezi Mungu iwe juu yao wote).
