Jan 31, 2024 16:36 UTC
  • Tarehe 12 Bahman, kumbukumbu ya kurejea Iran Imam Khomeini; kuanza Alfajiri Kumi

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Wasikilizaji wapenzi, Alkhamisi ya tarehe Mosi Februari wiki hii inasadifiana na tarehe 12 Bahman ambayo ni kumbukumbu ya moja ya matukio makubwa katika historia ya zama hizi, tukio la tarehe 12 Bahman 1357 kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia iliyosadifiana na tarehe Mosi Februari 1979.

Hiyo ni siku ya kihistoria kwani Imam Ruhullah Khomeini, muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku kama hii alirejea hapa nchini baada ya kuwa uhamishoni kwa muda wa miaka 14 na kutia nguvu Mapinduzi ya Kiislamu. Kurejea nchini Iran Imam Khomeini ulikuwa ni utangulizi wa harakati isiyo na mithili ya wananchi na kufikia ushindi Mapinduzi ya Kiislamu, mapinduzi ambayo hayana mfano katika karne za hivi karibuni.

 Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yanahesabiwa kuwa mapinduzi muhimu na makubwa zaidi katika nusu ya pili ya karne ya 20 Miladia. Kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu kwa hakika ilikuwa ni kufikiwa azma ya taifa kubwa kwa ajili ya kujipatia mamlaka ya kujitawala, heshima na kujipapatua kutoka kwenye udhibiti na satwa ya madola ya kibeberu. Katika kipindi ambacho ulimwengu ulikuwa umegawanyika katika kambi mbili kuu za Magharibi na Mashariki, mapinduzi ya wananchi wa Iran yalikuwa yakitoa kaulimbiu ya "Si Mashariki si Magharibi, bali ni Jamhuri ya Kiislamu." Mapinduzi hayo ya Kiislamu yalipata ushindi tarehe 12 Februaria 1979 (22 Bahman 1357 Hijria Shamsia).

 Kuanzia tarehe Mosi Februari hadi 12 ya mwezi huo mwaka 1979 siku ambayo mapinduzi hayo yalipata ushindi yaani katika kipindi cha siku kumi kulitokea matukio mbalimbali nchini Iran ambayo yalipelekea kusambaratishwa mfumo wa kifisadi wa utawala wa kifalme wa Shah. Siku hizo kumi zinazojulikana katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwa jina la Alfajiri Kumi zilivuruga mahesabu yote ya utawala wa Shah pamoja na waungaji mkono wake ikiwemo Marekani. Miongoni mwa mipango michafu iliyogonga mwamba ni kushindwa njama za kuzuia kurejea nchini Imam Khomeini.

Imam Ruhuullah Khomeini

 Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu anasema kuhusiana na siku hii kwamba: Tarehe 12 Bahman (Februari Mosi) kwa maana halisi ya neno, ni siku ya kuanza nguvu ya Uislamu. Licha ya kwamba katika tarehe hii kidhahiri mfumo wa kitaghuti ulikuwa unaonekana upo madarakani, lakini ukweli wa mambo ni kwamba haukuwa na madaraka yoyote. Kimsingi ni kwamba, kurejea Imam Khomeini humu nchini kulikwenda sambamba na kusambaratika mfumo huo fasidi. Viongozi wa utawala huo waliokuweko madarakani wakati huo walikuwa wakifanya juhudi zisizo na maana, ili waweze kuukoa mfumo huo ili ubakie japo kwa siku kadhaa tu nyingine, lakini hilo halikuwezekana kabisa.

 Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yaliyopata ushindi kwa uongozi wa Imam Khomeini MA, hayawezi kulinganishwa na mapinduzi yoyote yale yaliyotokea kwenye mataifa mengine ya dunia katika pande zake mbalimbali za kisiasa, kiuchumi, kijamiii na kiutamaduni. Ukweli wa mambo ni kuwa, ukiacha Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran hakuna mapinduzi mengine yoyote yale duniani ambayo yana sifa na vigezo vya mapinduzi ya kweli ambayo ndani yake kuna itikadi zote, thamani za jamii iliyofanya mapinduzi hayo na kuweko ushiriki wa matabaka yote ya watu.

 Imam Khomeini anasema kuhusiana na kulinganishwa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na mapinduzi mengine ya dunia kwamba: Someni na mfanye utafiti kuhusiana na mapinduzi ya Ufaransa na mapinduzi yale ya Sovieti. Watu waone kabla ya mapinduzi hayo kulikuwa na nini na baada ya mapinduzi hayo kuna nini. Je wananchi wamepata kitu chochote kupitia mapinduzi hayo?

 Imam Khomeini ambaye alikuwa na utambuzi kamili kuhusiana na hali ya kisiasa, kiutamaduni na jamii ya Iran katika miaka ya kupamba moto harakati za mapinduzi na kabla ya hapo, anatambua sababu kuu na siri ya mafanikio ya mapinduzi hayo mabadiliko ya kiroho na kiimani ya wananchi. Katika mazingira kama haya; wananchi wakabadilika kupitia hotuba na maneno ya Imam Khomeini sambamba na mapenzi ya Mwenyezi Mungu, wananchi hao wakawa hawana woga kwa utawala dhalimu wa Shah na ndio maana wakasimama kidete dhidi ya utawala huo.

Imam Khomeini akihutubia wananchi mara baada ya kuwasili nchini Iran kutoka uhamishoni nchini Ufaransa

 Baada ya kuzungumza yote hayo, tumeona ni vyema hapa tuzungumzie kwa muhtasari yaliyosemwa na watu mbalimbali kuhusu shakhsia ya kimataifa ya Imam Khomeini MA katika kupambana ya ubeberu na uistikbari. Imam Khomeini, mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alikuwa ni kiongozi shupavu na imara ambaye aliutikisa ulimwengu kwa fikra zake huru na uongozi wake wa kishujaa katika kilele cha kipindi cha Vita Baridi mwishoni mwa miaka ya 70. Imam Khomeini alipapalilia na kufanya zipate nguvu damu mpya katika harakati za Kiislamu na za kupigania uhuru na ukombozi duniani. Kijumla ni kwamba, Imam Khomeini si tu ni shakhsia anayeheshimika kimataifa na kupendwa na walimwengu, bali mitazamo na fikra zake za kupambana na dhulma na ubeberu ni jambo linaloenziwa sana na kufuatwa na wapigania haki na uhuru ulimwenguni.

 Tuanze na mtazamo wa Tajammul Hosseini, Mkuu wa Harakati ya Shahidi Hosseini ya nchini Pakistan huku akifafanua kwamba Imam Khomeini (MA) alifanikiwa pakubwa na kuweza kuweka mfano mzuri wa kufuatwa katika jamii ya Kiislamu kutokana na busara na ikhlasi yake, amesisitiza kuwa athari za mfano huo ni suala linaloonekana wazi miongoni mwa harakati za kupigania uhuru na ukombozi duniani.

Anasema kwa msingi huo tunaweza kusema bila ya kusita kwamba mfungamano mkubwa uliopo kati ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na thamani za Kiislamu na vilevile fikra za mafundisho ya Kiislamu za Imam Khomneini (MA) ndicho chanzo kikuu cha kuendelea kudumu fikra za Kiongozi huyo mashuhuri wa Kiislamu.

Njia na fikra za Imam (MA) katika kukabiliana na uistikbari na ubeberu wa madola ya Magharibi, fikra ambazo bila ya shaka zinatokana na mafundisho ya dini tukufu ya Uislamu, zimeweza kuvuka mipaka na kuwavutia walimwengu wa mataifa tofauti, jambo ambalo ni kinyume na matakwa ya madola ya kiistikbari ambayo tangu yalipopata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu hadi hivi sasa, hayajaacha fursa yoyote ya kufanya njama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Moja ya picha za kihistoria za Imam Khomeini MA

Maulana Qamar Hasnain, Mkurugenzi wa Jamaat al-Fatima ya India, yeye anasema katika mwelekeo huo huo kwamba: "Historia na maisha ya Imam Khomeini (MA) yana mafunzo mengi, na ujumbe aliouwasilisha kwa ulimwengu ni muhimu sana na wenye taathira kubwa ambazo zingalipo hadi leo. Miongoni mwa ujumbe wake muhimu zaidi ni tangazo la Siku ya Quds la kuiunga mkono Palestina kwa hoja kuwa Quds na ardhi za Palestina zinapaswa kuwa huru na kwamba Waislamu wote wanawajibika kuungana kwa ajili ya kufikia lengo hilo."

 Hilo ndilo jambo linalowafanya Wazayuni wanaoikalia kwa mabavu ardhi za Palestina waingiwe na kiwewe na kufanya kila wanaloweza kwa ajili ya kuzuia kuenea ulimwenguni fikra za Imam Khomeini MA. Ni kwa sababu hiyo ndio maana wamekuwa wakiendesha kwa makusudi siasa za jinai na ukandamizaji dhidi ya makundi ya Wapalestina wasio na hatia ili fikra za Imam Khomeini zisiweze kuandaa mazingira ya maghasibu hao wa Kizayuni kupata mapigo makubwa zaidi kutoka kwa Wapalestina na Waislamu kwa ujumla.

Imtiaz Razavi, mhadhiri wa chuo kikuu na mwanaharakati wa kijamii wa Pakistan anatathmini upeo wa kimataifa wa mbinu na fikra za Imam Khomeini katika kupambana na ubeberu na udhalimu wa madola ya kikoloni ya Magharibi na kusema: "Kupitia ujumbe wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Khomeini (MA) aliweza kuuamsha umma wa Kiislamu na kuandaa mazingira ya kusaidiwa wanyonge duniani na wakati huo huo kuwahamasisha Waislamu kupambana na ubeberu wa kimataifa. Kupitia ujumbe huo aliweza kuwathibitishia walimwengu wote kiujumla kwamba ubeberu na dhulma kamwe havidumu, na kwamba hatupaswi kujidhalilisha na kukubali kuburuzwa na siasa haramu ya maadui, bali tunapaswa kupambana nao kwa ajili ya kueneza uadilifu duniani."

Umati wa wananchi wa Tehran katika maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran

 

Maulana Mazhar Abbas Ghazi, mmoja wa maulamaa na wanaharakati wa wa Kiislamu wa mjini New Delhi India, anaamini kwamba Imam Khomeini MA alianzisha mapinduzi makubwa, ambayo hayajawahi kuonekana tena duniani.

 Anasema: "Sisi mjini New Delhi na Waislamu wote duniani tumeathirika na shakhsia ya Imam Khomeini. Hili ni jambo la kushangaza sana. Muasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu alikuwa shakhsia na mchamungu mkubwa ambaye hajawahi kuonekana mfano wake katika zama za karibuni. Alikuzwa na kulelewa katika mazingira ya kiroho kiasi kwamba alikuwa na nafasi kubwa katika masuala ya kielimu, ujasiri, thamani za kimaadili na nyanja nyingine nyingi. Kwa vyovyote vile, Imam Khomeini (MA) si shakhisia wa zama wala kizazi kimoja tu.

 Pia anasema: Kwa fikra zake zilizosimama juu ya msingi wa mafundisho ya Uislamu, alithibitisha kuwa, kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu, watu wanaweza kuendesha mapambano kwa ushujaa na hatimaye kuwashinda madhalimu bila ya matatizo makubwa. Hilo ni jambo ambalo limekaririwa na kuthibitishwa kivitendo katika historia ya mwanadamu. Kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa madamu historia itaendelea kuwa hai, fikra na mawazo ya Imam Khomeini (MA) pia yataendela kuwa hai."

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei akiomba dua na kusali ndani ya Haram ya Imam Khomeini kusini mwa Tehran MA ikiwa ni sehemu ya kuanza maadhimisho ya Bahman 22 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuundwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

 

Ni kwa sababu hiyo pia ndio maana, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei akasema kuwa, Imam Khomeini MA ni mmoja wa shakhsia wenye taathira kubwa katika historia. Katika moja ya miongozo yake ya busara, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, amesema, Imam Ruhullah Khomeini MA ni miongoni mwa viongozi na shakhsia waliotoa taathira kubwa katika historia na kusisitiza kuwa: Viongozi wa aina hii hawawezi kufutwa au sura yao haiwezi kupotoshwa. Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, alisema hayo kwenye hotuba yake kwa taifa kwa mnasaba wa hauli ya mwaka wa 34 wa kufariki dunia Imam Khomeini (RA). Alisema: Yumkini kukafanyika upotoshaji katika kipindi fulani kuhusu Imam Khomeini, lakini jua hilo halitabaki nyuma ya mawingu.

 Katika sehemu nyingine ya miongozo yake hiyo, Ayatullah Khamenei alisema: Imam Khomeini alifanya mageuzi matatu makubwa na yasiyo na kifani katika ngazi ya nchi, katika ngazi ya Umma wa Kiislamu na katika ngazi ya dunia, ambayo huenda yasitokee tena katika siku zijazo. Alitoa mfano kwa kusema, Imam Khomeini (RA) alivunja muundo wa kisiasa wa kifalme na badala yake akaanzisha demokrasia iliyosimama juu ya msingi wa dini ya Kiislamu. Aliondoa mfumo usio wa Kiislamu kwenye medani, akabadilisha udikteta na mahala pake akaweka uhuru. Alijenga hali ya kujiamini mahali pa kutokuwa na utambulisho, na alibadilisha hali ya kuwa tegemezi kwa wageni na kuifanya hali ya 'sisi wenyewe tunaweza'.

Pia alisema: Kizazi kipya kina haja ya kumtambua vyema Imam Ruhullah Khomeini na kufafanua kwa kusema: Mageuzi yaliyofanywa na Imam Khomeini MA yamekabilika kote ulimwenguni na kwamba upinzani wa madola ya kibeberu ambayo yanafanya kila linalowezekana kukabiliana na ufufuaji wa masuala ya kiroho hayawezi kufuta taathira kubwa ya mwanachuoni huyo mkubwa wa zama za hivi karibuni.

Tags