Feb 10, 2021 02:32 UTC
  • Jumatano tarehe 10 Februari 2021

Leo ni Jumatano tarehe 26 Jamadithani 1442 Hijria sawa na tarehe 10 Februari mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 258 iliyopita ulitiwa saini mkataba baina ya Uingereza na Ufaransa katika mji wa Paris. Wafaransa waliutaja mkataba huo kuwa mbaya sana. Hii ni kutokana na kuwa, baada ya miaka mingi ya vita na mivutano na Uingereza, Ufaransa ilikubali kufumbia macho madai yake yote na maslahi yake ya kikoloni huko India na Canada. Sababu ya kutiwa saini mkataba huo ni kwamba, katika kipidi hicho Ufaransa ilikuwa imedhoofika kutokana na kujihusisha na vita mbalimbali barani Ulaya, na kwa upande wa kijeshi na kiuchumi haikuwa na ubavu wa kuendelea kupigana vita na Uingereza.

Mkataba wa Paris

Siku kama ya leo miaka 130 iliyopita alifariki dunia Sophia Krukovsky mwanahisabati wa Russia. Alizaliwa mwaka 1850 mjini Moscow. Licha ya kuwa alipendelea sana elimu ya hisabati, lakini kutokana na sababu za kibaguzi hakuweza kujiunga na chuo kikuu na ni kwa msingi huo ndio maana akaelekea nchini Ujerumani na kujifunza elimu ya hisabati na fizikia. Pamoja na hayo Sophia Krukovsky alikabiliwa na matatizo mengi kabla ya kufanikiwa kujiunga na chuo kikuu. Kufuatia hali hiyo alilazimika kusoma elimu hiyo kwa mwalimu wa hisabati nje ya chuo kikuu. Mwaka 1874 Sophia Krukovsky alitunukiwa shahada ya juu ya Uzamivu (PhD) bila kuhudhuria chuoni. Aidha mwaka 1888 alitunukiwa zawadi yenye itibari katika chuo cha academia nchini Ufaransa. Kuanzia mwaka 1884 hadi mwaka 1891 alipofariki dunia alijishughulisha na kazi ya ufundishaji wa hisabati katika Chuo Kikuu cha Stockholm, Sweden.

Sophia Krukovsky 

Siku kama ya leo miaka  71 iliyopita yaani tarehe 10 Februari mwaka 1950, Joseph Mc Carthy Seneta wa chama cha Republican cha nchini Marekani aliwasilisha orodha ya majina ya wafanyakazi 205 wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo akiwatuhumu kuunga mkono ukomonisti na kuifanyia ujasusi Urusi ya zamani. Hatua hiyo ilipelekea kuanza kwa kile kilichojulikana kama "Mc Carthisim" huko nchini Marekani, ambapo kwa mujibu wake wanafikra, wataalamu na viongozi mbalimbali wa Marekani walifuatiliwa na kusakwa baada ya kutuhumiwa kuwa na mitazamo na fikra za Kikomonisti na kuifanyia ujasusi Urusi ya zamani. Kamisheni ya Mc Carthisim ambayo ilikabiliwa na upinzani mkubwa, iliwafuta kazi karibu watumishi wa serikali wapatao 2000 huku idadi kubwa ya wataalamu na wasomi wakiswekwa jela kwa tuhuma zisizokuwa na msingi.

Joseph Mc Carthy

Katika siku kama ya leo miaka 74 iliyopita, tawala za waitifaki na zile zilizokuwa zikihasimiana katika Vita vya Pili vya Dunia zilisaini makubaliano ya amani. Katika siku hiyo, Marekani, Urusi ya zamani, Uingereza na Ufaransa zilisaini makubaliano ya amani na nchi zilizoshindwa katika vita hivyo yaani Italia, Finland, Poland, Hungary, Romania na Bulgaria, na kwa utaratibu huo nchi sita hizo kwa mara nyingine tena zikajipatia uhuru.

Tarehe 22 Bahman miaka 42 iliyopita Iran ilikuwa katika siku ya kihistoria itakayokumbukwa siku zote. Siku hiyo wananchi waliokuwa wakipiga takbira na kutoa nara za kimapinduzi chini ya uongozi wa Ayatullah Ruhullah Khomeini walihitimisha kipindi cha giza totoro katika historia ya Iran kwa kuung'oa madarakani utawala wa kidikteta wa Shah Pahlavi. Wananchi wanamapinduzi wa Iran, wanaume kwa wanawake, vijana kwa wazee na watu wa matabaka yote walisimama kidete wakipambana na mizinga na vifaru vya jeshi la Shah na kujisabilia kwa ajili ya Mapinduzi ya Kiislamu. Mapambano ya wananchi Waislamu wa Iran yalienea nchini kote huku wafuasi wa Imam Ruhullah Khomeini wakiwa katika juhudi za kumaliza kabisa mabaki ya utawala wa kidhalimu wa kifalme. Wakati ilipotangazwa habari kwamba vifaru vya majeshi ya Shah vilikuwa njiani kuelekea Tehran kwa ajili ya kukandamiza harakati za mapinduzi zilizokuwa zinaelekea kileleni, wananchi wa miji mbalimbali walijitokeza na kupambana na majeshi hayo huku wakifunga njia na kuzuia misafara ya vifaru hivyo. Baadhi ya makamanda wa ngazi za juu wa jeshi la Shah waliuawa na wananchi katika mapambano hayo na kulilazimisha jeshi kutopendelea upande wowote. Siku hiyo pia wananchi wanamapinduzi walitwaa Shirika la Redio na Televisheni la Iran kutoka kwenye udhibiti wa jeshi. Muda mfupi baadaye lilitolewa tangazo katika redio ya taifa likitangaza kwamba "Hii ni Sauti ya Mapinduzi ya Kiislamu". Sauti hiyo ilitangaza ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuporomoka utawala wa kidhalimu wa kifalme uliotawala Iran kwa kipindi cha miaka 2500.

Siku ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu