Kuongezeka wimbi la watu wanaosilimu baada ya mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza
(last modified Thu, 01 Aug 2024 09:10:48 GMT )
Aug 01, 2024 09:10 UTC
  • Kuongezeka wimbi la watu wanaosilimu baada ya mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza

Kasi ya watu wanaosilimu barani Ulaya imeongezeka kwa asilimia 400 tangu kuanza mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza mwezi Oktoba mwaka jana.

Ripoti zinasema kuwa, wimbi la watu wanaosilimu barani Ulaya limeongezeka kwa asilimia 400 tangu utawala wa Israel uanzishe vita na mashambulizi ya kikatili ya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza. Suala hilo linaweza kueleweka vyema kwa kutazama video nyingi katika mitandao ya kijamii ambazo zimekuwa zikisambaa tangu kuanza mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya Wapalestina huko Gaza; na katika video hizo Wamagharibi wanaeleza hamu yao ya kusoma Qur'ani ili kufahamu siri ya mapambno ya watu wa Palestina. 

Tabiri mbalimbali zinaonyesha kuwa, hadi kufikia katikati ya karne hii, Waislamu watakuwa wakiunda humusi au moja ya tano ya jamii ya watu wa Ulaya. Utabiri huu umetiwa nguvu na utafiti wa Kituo cha Utafiti cha Pew, ambacho kinasema kuwa ifikapo mwaka 2050, idadi ya Waislamu nchini Ujerumani itafikia asilimia 20, Ufaransa asilimia 18, na Uingereza asilimia 17. 

Katika utafiti huo uliopewa jina la "Lini na katika Nchi Gani Waislamu wa Ulaya Watakuwa wengi?" kumefikiwa natija kwamba, Waislamu watakuwa wengi zaidi katika nchi za Uswidi, Ufaransa na Ugiriki katika kipindi cha miaka 100 ijayo. Huko Ubelgiji na Bulgaria inatarajiwa kuwa tukio hili litajiri baada ya takriban miaka 115, huku idadi ya Waislamu ikiwa kubwa zaidi baada ya karibu miaka 150 huko Italia, Luxenmbourg na Uingereza. 

Kuongezeka idadi ya Waislamu barani Ulaya 

Makadirio yanaonyesha kuwa Ufaransa ina idadi kubwa ya Waislamu miongoni mwa nchi kubwa za Ulaya. Utafiti wa mwezi Juni mwaka 2023 wa Taasisi ya Takwimu na Utafiti wa Masuala ya Uchumi ya Ufaransa umeonyesha kuwa asilimia 10 ya wananchi wa Ufaransa ni Waislamu; huku makadirio mengine yakionyesha kuwa, idadi hiyo inafikia asilimia 15.   

Hivi karibuni pia gazeti la Kituruki la Yeni Shafiq lilionyesha klipu za makumi ya wanawake raia wa Australia waliosilimu baada ya kuathiriwa na kusimama kidete na istiqama ya watu wa Palestina. Gazeti hilo limethibitisha kuwa wanawake kadhaa wamesilimu katika Msikiti wa Meadow Heights huko Melbourne, Australia. Gazeti hilo limeongeza kuwa, kusimama imara na imani thabiti ya Wapalestina vimewashangaza wanawake wa Australia na kuwatia ari ya kujiunga na dini tukufu ya Uislamu. 

Katika wiki za karibuni, mtandao wa kijamii wa TiKToK pia ulionyesha filamu za vijana wa Kimarekani hasa wanawake wakisoma Qur'ani kwa furahana kwamba wameshangazwa na muhtawa wa kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu na kuamua kuifuata dini ya haki. 

Picha za watu waliodhulumiwa wa Gaza baada ya vita vya Israel vya Oktoba mwaka jana zilizochapishwa katika vyombo vya habari zimezidisha hamu na shauku ya baadhi ya raia wa Marekani kutaka kujua mafundisho ya Uislamu na Qur'ani, hasa vijana wa Gen-Z ambao wamefahamu mafundisho ya Qur'ani na kuvutiwa sana. 

Mwakilishi wa ngazi ya juu wa kundi hilo, Megan Rice, binti Mmarekani mwenye asili ya Afrika, mwezi mmoja uliopita alituma ujumbe katika mtandao wa kijamii wa TikTok akieleza kuvutiwa na muqawama wa wananchi wa Palestina mkabala wa jinai dhidi ya binadamu zinazotekelezwa na Israel.  

Baadhi ya watu walimshauri Megan asome Qur'ani Tukufu ili kufahamu msingi wa imani na istiqama ya Wapalestina; na Rice mwenyewe haraka alianza kusoma kitabu hicho. Megan Rice alisoma sura, aya na tasfiri ya Qur'ani kwa njia ya mtandao. Kisha Mmarekani huyo alianzisha Klabu ya "Wasomaji Vitabu vya Kidini Duniani". Kadiri Rice alivyokuwa akisoma Qur'ani ndivyo alivyozidi kutambua ni kwa kiasi gani maudhui yake yanawiana na mfumo wake wa imani.

Rice alifikia natija kuwa, Qur'ani inapinga utamaduni wa kuchupa mipaka, ni dhidi ya dhulma na ukandamizaji na inawaunga mkono na kuwatetea wanawake. Rice alisilimu  baada ya mwezi mmoja. 

Rice si mtu pekee katika uwanja huu. Ripoti zinaonyesha kuwa kuna idadi kubwa ya vijana waliokisoma kitabu hiki ili kupata ufahamu mzuri wa dini ya Uislamu ambayo kwa kawaida huchafuliwa katika vyombo vya habari vya Magharibi na pia kwa lengo la kuonyesha mshikamano na Waislamu wa Gaza.

Mwanaharakati, Megan Rice 

Gazeti la Guardian la Uingereza linasema kuwa video zilizorushwa kwenye mtandao wa kijamii wa Tik Tok kwa hashtag "quranbookclub"  hadi sasa zimetazamwa mara milioni 1.9, na watumiaji wengi wa hashtag hiyo wanaweka picha na video zao wakiwa na vitabu vya Qur'ani Tukufu walivyonunua  wakisoma aya za kitabu hicho kwa mara ya kwanza.

Naye Ahmad Mansour mwandishi wa habari mtajika raia wa Misri anayefanya kazi katika televisheni ya al Jazeera ya Qatar ameandika katika makala yake kuwa: Matukio ya Ukanda wa Gaza na namna wanamapambano wa Kipalestina wanavyoshirikiana katika medani ya vita na wanavyoamiliana vyema na mateka wa Israel yameonyesha taswira ya wazi ya Uislamu. Mansour ameashiria fedha nyingi zinazotumiwa na utawala wa Israel na nchi za Magharibi ili kuchafua sura safi ya Uislamu na kueneza propaganda chafu dhidi ya dini hiyo ya Mwenyezi Mungu (Islamophobia) na kusema: Watu wa Ukanda wa Gaza wamezima na kubatilisha njama hizo; na sasa wamekuwa sababu na kubadilika mtazamo wa watu wa Ulaya na Marekani kuhusu Uislamu. 

 

Tags