Ramadhani, Mwezi wa Dhifa ya Mwenyezi Mungu (25)
(last modified Thu, 27 Mar 2025 06:31:17 GMT )
Mar 27, 2025 06:31 UTC
  • Ramadhani, Mwezi wa Dhifa ya Mwenyezi Mungu (25)

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Ni furaha iliyoje kuwa nanyi tena wapenzi wasikilizaji katika mfululizo mwengine wa Ramadhani, Mwezi wa Dhifa ya Mwenyezi Mungu.

Hakika Ramadhani, ni mwezi wa kufunguliwa milango ya rehma za Allah; mwezi unaozinawirisha nyoyo zetu kwa mwanga wa Aya za Qur’ani na pepo mwanana za dua na munajati na kutukurubisha zaidi kwa Mola wetu Rahimu na Mrehemevu. 

Mwezi huu ni mithili ya hidaya ya mbinguni; ni fursa ya kutuwezesha kuzitambua vizuri zaidi nafsi zetu, kuzisafisha nyoyo zetu na vumbi la mambo ya mazoea ya kila siku na kuyaangalia kwa jicho jengine jipya maisha na walioko kando yetu.

Katika mfululizo wetu wa leo tumekusudia kuzungumza machache kuhusu kumpenda Bwana Mtume Muhammad SAW na Ahlu-Baiti zake na dua za kuziunganisha nyoyo zetu na ulimwengu wa mbinguni. Tuweni pamoja basi katika dhifa hii ya leo, ya kuzipamba na kuzinawirisha nyoyo zetu kwa nuru ya Qur’ani na mapenzi ya Ahlu-Baiti (AS).

*********

Kumpenda Mtume wa Allah, Nabii Muhammad SAW na watu watoharifu wa Nyumba yake, yaani Ahlu-Baiti (AS) si kitu cha hisia nyepesi tu na cha kumalizika haraka; ni jambo linalojikita ndani kabisa ya nafsi, ambalo ni mithili ya chemchemi safi kabisa inayosafisha na kuyapa maisha yetu maana yake halisi. Mapenzi na mahaba hayo hayaishii ndani ya nyoyo zetu tu, bali yanajiakisi pia katika tabia zetu, maono yetu na katika kila hatua tunayopiga katika maisha yetu. Qur’ani Tukufu, Kitabu cha mbinguni kilichoteremshwa kwenye moyo wa Bwana Mtume SAW ndani ya mwezi huu mtukufu wa Ramadhani kinatukumbusha mara kadha wa kadha kwamba, kumpenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake ndiyo mihimili mikuu ya imani.

Katika Aya ya 24 ya Suratu-Tawbah Mwenyezi Mungu Mtukufu anatueleza kwamba, mapenzi yetu kwake Yeye na kwa Mtume wake, inapasa yawe makubwa zaidi kuliko chochote kile katika maisha yetu; kuanzia wazazi wetu, watoto wetu, mali zetu na kila tukipendacho. Aya hiyo inatuhutubu kama ifuatavyo: “Sema: Ikiwa baba zenu, na wenenu, na ndugu zenu, na wake zenu, na jamaa zenu, na mali mlizochuma, na biashara mnazo ogopa kuharibika, na majumba mnayo yapenda, ni vipenzi zaidi kwenu kuliko Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Jihadi katika Njia yake, basi ngojeni mpaka Mwenyezi Mungu alete amri yake. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wapotovu.”

Naye Bwana Mtume SAW ametuambia katika maneno yake matukufu: “Haifikii imani iliyokamilika yeyote yule kati yenu, mpaka awe ananipenda mimi zaidi kuliko nafsi yake, ahli zake na kila kilicho chake”.

Maana halisi ya kumpenda Mtume ni nini? Ni kutamka tu kwa ulimi “nampenda Mtume?” La hasha! Mapenzi ya kweli ya kumpenda Mtume, ni kujitahidi kuwa kama yeye; kuishi kwa moyo wa huruma, ukweli na uadilifu; na muda wote kumuweka Allah mbele ya macho yetu. Na hivyo ndivyo yanavyopasa kuwa pia mapenzi yetu kwa Ahlu-Baiti zake. Wateule hao ndio walioendeleza njia ya Bwana Mtume, wakatufunza kwa maisha yao, vipi tujitolee katika njia ya Mwenyezi Mungu na kuwa thabiti kiimani hata katika hali ya mitihani na misukosuko mikubwa kabisa. Imam Ali (AS) kwa ushujaa na hekima, Bibi Fatima (SA) kwa utakasifu na istiqama, Imam Hassan (AS) kwa subira yake na Imam Hussein (AS) kwa mapambano yake, ni nuru zinazoangazia njia ya haki na uongofu.

Ramadhani wapenzi wasikilizaji, ni mwezi ilioteremshwa Qur’ani, ambayo Bwana Mtume SAW ameielezea pamoja na Ahlu-Baiti zake kuwa ni vizito viwili vyenye thamani ya kipekee, alivyotuachia ili vitufikishe kwenye saada na fanaka. Mwezi huu ni fursa ya kujikurubisha kwa Allah kwa Funga, ibada na kusoma Qur’ani; lakini kujikurubisha huko hakutakamilika, bila ya kuambatana na mapenzi yetu kwa Mtume na watu wa Nyumba yake.

*********

Katika siku ya 25 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani tuisomeni kwa pamoja dua ya siku hii ili kuzikurubisha nyoyo zetu kwa Allah:

اَللّهُمَّ اجعَلْنِی فِیهِ مُحِبًّا لِأَوْلِیَائِکَ- وَمُعَادِیًا لِأَعْدَائِکَ -مُسْتَنًّا بِسُنَّةِ خَاتِمِ أَنْبِیَائِکَ- یَا عَاصِمَ قُلُوبِ النَّبِیِّینَ

Ewe Mola wangu, nijaalie ndani ya siku hii niwe mpenzi wa mawalii wako- na adui wa maadui zako-, mwenye kujipamba kwa mwenendo wa wamwisho katika Mitume wako; Ewe mlindaji wa nyoyo za Mitume. Dua hii imebeba ndani yake matarajio yote ya muumini; yaani kutaka moyo wake uwe pamoja na waja wema, uwekwe mbali na wabaya na ufuate njia ya Mtume.

Na hiki ndicho kinachoelezwa katika mafundisho ya dini kama “tawalli” na “tabarri”. Tawalli maana yake ni kuwapenda anaowapenda Mwenyezi Mungu, wanaomfurahisha Allah kwa amali zao. Na tabarri ina maana ya kujiweka mbali na maadui wa Mwenyezi Mungu, watu ambao kwa madhambi na dhulma wanazofanya wameziweka mbali nafsi zao na rehma za Mola. Misingi miwili hii ni mfano wa mbawa mbili zinaotuwezesha kuruka kwenye anga ya imani.

Katika sehemu ya kwanza ya Aya ya 22 ya Suratul-Mujaadalah Mwenyezi Mungu Mtukufu anatuambia: “Huwakuti watu wanao muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho kuwa wanawapenda wanao mpinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hata wakiwa ni baba zao, au watoto wao, au ndugu zao, au jamaa zao”….

Aya hii kwa hakika inachora mstari mwekundu kuhusu imani zetu; kwa maana kwamba, kama kweli tunampenda Mwenyezi Mungu, haziwezi nyoyo zetu kuwa na mfungamano na watu wanaomuasi Yeye Mola. Tukumbuke pia kuwa, mapenzi na uadui wetu inapasa uwe ni kwa ajili ya Allah, na si kwa ajili ya nafsi zetu. Ikiwa tunampenda au kumchukia mtu kwa sababu za binafsi au taasubi zisizo na msingi, mapenzi na chuki hizo hazitakuwa ni kwa ajili ya Allah.

Bwana Mtume SAW na Ahlu-Baiti zake wametufunza kuwa, yeyote tunayesuhubiana naye, tutakuwa pamoja naye huko Akhera. Imam Ali (AS) amesema: “Yeyote atupendaye sisi, atakuwa pamoja nasi; na kama mtu atalipenda hata jiwe, Mwenyezi Mungu atamfufua na jiwe hilo”. Imam Muhammad Baqir (AS) naye pia ametuambia: “Kama unataka kuipima nafsi yako, uangalie moyo wako. Kama utaona unawapenda wanaompenda Mwenyezi Mungu na unawachukia wafanyao madhambi, jua kwamba nafsi yako ni nzuri na Mwenyezi Mungu pia anakupenda”. Hii inamaanisha kuwa, kipimo kizuri kwetu ni mapenzi yetu. Na katika dua ya leo, tumemuomba Allah mambo mawili makubwa: atufanye tuwapende wanaompenda Yeye na atuweke mbali na maadui zake. Maombi mawili haya ni mithili ya nguzo mbili imara za kuyaelekeza maisha yetu katika mkondo sahihi.

Ninamuomba Mwenyezi Mungu atutakabalie ibada zetu na ninayahitimisha mazungumzo yetu ya leo kwa dua hii:

 اللَّهُمَّ- إِنِّی أَسْأَلُکَ خَیْرَ مَا تُسْأَلُ، فَأَعْطِنِی أَفْضَلَ مَا تُعْطِی

Ewe Mola wangu! Hakika mimi ninakuomba yaliyo mema zaidi, ya unayoombwa, na nitunuku yaliyo bora, ya unayotoa kuwatunuku waja wako”. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/