Kuaga dunia Farajollah Salahshoor, muongozaji wa filamu za kidini
https://parstoday.ir/sw/radio/uncategorised-i2734-kuaga_dunia_farajollah_salahshoor_muongozaji_wa_filamu_za_kidini
Assalamu alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika kipindi hiki cha Makala ya Wiki ambacho katika jumla hili kitamzungumzia mwongozaji filamu mashuhuri wa filamu za kidini Farajollah Salahshoor, pamoja na athari za tasnia ya filamu zilizoachwa na msanii huyo aliyeaga dunia wiki mbili zilizopita. Ni matumaini yangu kuwa mtaendelea kuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 09, 2016 11:57 UTC
  • Kuaga dunia Farajollah Salahshoor, muongozaji wa filamu za kidini

Assalamu alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika kipindi hiki cha Makala ya Wiki ambacho katika jumla hili kitamzungumzia mwongozaji filamu mashuhuri wa filamu za kidini Farajollah Salahshoor, pamoja na athari za tasnia ya filamu zilizoachwa na msanii huyo aliyeaga dunia wiki mbili zilizopita. Ni matumaini yangu kuwa mtaendelea kuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Farajollah Salahshoor, alizaliwa mwaka 1953 katika mji wa Qazvin hapa nchini Iran. Alianza kujishughulisha na sanaa ya filamu kwa kuanzia katika uigizaji wa filamu za sinema katika kipindi cha baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, yaani cha baada ya mwaka 1979. 

Baadaye alijitosa kwenye uga wa filamu na michezo ya televisheni na kuanza kazi ya utungaji na uongozaji michezo ya mfuatano ya televisheni ya kihistoria na kidini.

Michezo hiyo ya televisheni ni "Nabii Ayoub", "As-habul Kahf" (The Men of Angelos) na "Nabii Yusuf", ambayo imeonyeshwa kwa miaka kadhaa katika kanali mbalimbali za televisheni ndani na nje ya Iran.

Baada ya kuugua kwa muda, Farajollah Salahshoor aliaga dunia tarehe 27 Februari mwaka huu akiwa na umri wa miaka 63.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alituma ujumbe wa salamu za rambirambi kwa mnasaba wa kuaga dunia msanii na muongozaji filamu huyo mashuhuri. Katika ujumbe huo wa salamu za mkono wa pole, Ayatullah Khamenei amesema:" Athari maarufu na za kudumu za mwanasanaa huyu muumini, ambazo zimevuka mipaka ya nchi na kuiletea heshima na itibari tasnia ya filamu ya Iran mbele ya macho ya watu wa mataifa mengine, bila ya shaka zitaingia kwenye hisabu ya mema aliyoyabakisha; na inshaa Allah zitampatia malipo ya thawabu kwa Mwenyezi Mungu na kukumbukwa kwa wema na watu".

***********

Moja ya michezo ya televisheni ya Kiirani iliyopendwa mno ni mchezo wa filamu ya "Nabii Yusuf" unaohusu maisha ya Nabii Yuisuf (AS) ambao ulitungwa na kuongozwa na marehemu Farajollah Salahshoor. Mchezo huo ulianza kuonyeshwa kwa mara ya kwanza mwaka 2009 katika kanali ya kwanza ya televisheni ya Iran na kisha baadaye kuonyeshwa kwenye kanali nyengine za televisheni za matangazo ya ng'ambo na kanali nyengine kadhaa za nje ya nchi. Kutokana na muhtasari wa majimui nzima ya mchezo huo imetengenezwa filamu ya sinema ambayo imeonyeshwa kwenye matamasha kadhaa ya filamu ya ndani na nje ya Iran. Waigizaji wakuu 45 na zaidi ya 150 wa nyongeza wameshiriki katika uigizaji wa mchezo wa maisha ya Nabii Yusuf (AS).

Kuhusu mchezo wa filamu ya televisheni wa maisha ya Nabii Yusuf ni kwamba sehemu zote za mchezo huo ambao umetarjumiwa katika lugha mbalimbali zinapatikana kwenye mtandao wa kijamii wa YouTube. Wakati unapotafuta neno la Kiarabu "Yusufu-Ssiddiq"ambalo ndilo jina la mchezo huo kwa Kiarabu unakuta idadi ya watu walioangalia sehemu mbalimbali za mchezo huo imeanzia laki tatu hadi milioni moja na nusu. Tab'an idadi hiyo ni kwa upande wa watazamaji wa lugha ya Kiarabu, na bila ya shaka ni kubwa zaidi mara kadhaa ikijumuishwa na watazamaji wa lugha nyenginezo.

Kanali nyingi za televisheni na za satalaiti zimeonyesha mchezo wa televisheni wa kisa cha maisha ya Nabii Yusuf (AS). Miongoni mwa hizo ni pamoja na kanali ya Al-Kawthar, Al- Wilayah, Al-Manar, Drama Al Misriyyah, Oscar Drama, Kanali ya Melody, Time Mix, Kariv Drama, Dunyal-Fadhaiyyah, Nasma TV, Al-Furat, Diyali na Iraq- Al Mustaqbal.

Mchezo mwengine wa televisheni ulioongozwa na marehemu Farajollah Salahshoor, ni wa Maisha ya Nabii Ayoub (AS).

Ayoub (AS) ni Mtume ambaye jina lake lililobarikiwa limetajwa mara kadhaa ndani ya Qur'ani tukufu na kusifiwa mno kwa subira na ustahamilivu wake. Katika mchezo huo ambao umetengenezwa kulingana na simulizi za Qur'ani anaonekana shetani aliyejawa na husuda na hasira kwa sababu ya hadhi na daraja aliyokuwa nayo Nabii Ayoub mbele ya Mwenyezi Mungu. Takdiri ya Allah ikawa ni kumtahini mja wake huyo kwa tabu na masaibu makubwa, kwa sababu shetani hakuwa akiamini kama Mtume huyo alikuwa na imani ya kiwango cha juu mno. Mwenyezi Mungu akamtahini Nabii Ayoub kwa majaribu mengi na makubwa; lakini yote hayo hayakumrudisha nyuma Nabii Ayoub katika kumwabudu Mola wake na hatimaye Mwenyezi Mungu akamrejeshea tena neema zake maradufu zaidi ya zile alizokuwa amemjaalia hapo kabla.

***********

Kisa cha As-habul Kahf, ni mchezo mwengine wa televisheni ambao utengenezaji wake uliongozwa na marehemu Farajollah Salahshoor. Kisa cha mchezo huo ni waumini kadhaa wa zama za kipindi kifupi cha baada ya kuzaliwa Nabii Isa (AS) na kabla ya kuanza kuenea Ukristo, katika zama za utawala wa Mfalme mmoja wa Rumi ya kale aliyekuwa akiitwa Diqyanus. Waumini hao wote ghairi ya mmoja tu kati yao walikuwa katika kizazi cha maashrafu na wakubwa wa ufalme huo, hivyo walikuwa wameficha imani zao. Wakati Mfalme alipowagundua kuwa ni waumini aliwatia gerezani. Vijana hao walitoroka jela wakati wa usiku na kukimbilia nje ya mji hadi eneo la mlimani. Walimlingania dini yao ya tauhidi mchungaji mmoja waliyekutana naye na kumwomba awapatie hifadhi. Mchungaji huyo aliiamini dini yao na kuandamana nao kwenda kujificha kwenye pango moja la mlimani huko. Huko walilala usingizi mzito uliochukua muda wa miaka 309 ndipo wakaamka. Matukio yaliyojiri baada hapo ndiyo maudhui kuu ya kisa cha mchezo huo wa televisheni wa kisa cha As-habul Kahf ambao wakati ulipoonyeshwa uliwavutia watazamaji wengi.

**********

Wakati alipokuwa akizungumzia jinsi mchezo wa filamu ya maisha ya Nabii Yusuf ulivyovutia watazamaji wengi, wakiwemo Waislamu na hata wasio Waislamu, marehemu Salahshoor alisema:”Filamu ya “Nabii Yusuf” inajenga mawasiliano na fitra na maumbile ya watu. Fitra ni nguvu ya kubaini na kupambanua jambo kiinsafu na kiadilifu ambayo Mwenyezi Mungu ameijaalia ndani ya nafsi ya mtu, na hivyo kuwafanya watu walikubali jambo zuri bila kujali kama mtu ni Muislamu au si Muislamu. Kisa cha Nabii Yusuf ni hakika si uongo. Hakika na ukweli ni mambo yanayowafikiana na fitra na maumbile ya mtu. Kama ambavyo wanadamu wanachukizwa na uongo ndivyo vivyo hivyo wanaikubali haki. Kwa masikitiko ni kwamba aghalabu ya filamu zilizopo duniani leo hii ni za uongo, isipokuwa zile zinazotengenezwa kwa kuzingatia matukio ya kweli. Isitoshe ni kwamba filamu ya Nabii Yusuf ina kisa kizuri sana; na watu huwa wanapenda kisa kizuri na cha kuvutia. Nukta nyengine ni kwamba kisa hiki kina mafunzo ya kuzingatia. Kwa kawaida filamu ambazo ndani yake zina mafunzo ya kuzingatia huwa zinapendwa zaidi na nukta hii imetiliwa mkazo na Qur’ani pia. Sifa nyengine maalumu iliyonayo filamu ya mfululizo ya Nabii Yusuf ni kuwa kwake na muhtawa maudhui iliyokamilika. Ibada, mapenzi, kujitolea, kusamehe, imani n.k ni miongoni mwa maudhui zinazojenga muhtawa wa majimui hiyo.

Farajollah Salahshoor, alikuwa mmoja wa wanasanaa wachache walioingia kwenye tasnia ya filamu wakiwa na dukuduku la Qur’ani; na kwa sababu hiyo tunaweza kusema yeye ni mmoja wa wasanii walioweza kuioanisha tasnia ya filamu na Qur’ani tukufu. Marehemu Salahshoor aliweza kubuni maigizo ya kuvutia katika tamthilia pamoja na filamu za sinema na michezo ya televisheni na kulifanya jina lake libakie milele katika uga wa sanaa hapa nchini. Nukta ya kutaamali na kuzingatia kuhusu njia ambayo alichagua kuifuata mwanasanaa huyu ni kwamba kwa maoni ya wadau wengi wa tasnia ya sinema, kufuata njia hiyo ya utengenezaji filamu kiqur’ani ni jambo lisiloweza kutekelezeka; lakini kwa hima, bidii na jitihada zake aliweza kulifanikisha suala hilo muhimu, ambalo linashuhudiwa vyema zaidi katika athari ya mwisho kabisa ya sanaa iliyotengenezwa na marehemu Salahshoor ya filamu ya “Nabii Yususf”. Na sababu ni kwamba kazi na athari hiyo muhimu iliwavutia watazamaji wengi mno, si wa nchini Iran pekee bali pia wa nchi nyengine nyingi za Kiislamu.

Nukta ya mwisho inayopasa kuiashiria hapa ni kwamba marehemu Farajollah Salahshoor, alikuwa ameshakamilisha kuandaa matini ya filamu mpya ya mfululizo wa televisheni ya “Kalimullahi Musa” kuhusu kisa cha maisha ya Nabii Musa (AS), lakini mauti hayakumpa fursa ya kuianza kazi ya uchukuaji filamu wa mchezo huo. Mchezo wa televisheni ambao kwa kutoa picha ya maisha na mafundisho sahihi ya Mtume huyo wa Allah ungeweza kufichua na kuanika mengi ya uongo na ghilba yanayofanywa na Wazayuni kupitia utawala wao bandia na haramu wa Israel.

Wapenzi wasikilizaji, kipindi chetu cha juma hili cha Makala ya Wiki kimefikia tamati. La ziada sina ghairi ya kukuageni na kukutakieni kheri na fanaka maishani