Dec 17, 2016 09:22 UTC
  • Sira ya Bwana Mtume Muhammad SAW Katika Kuleta Umoja

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Karibuni wapenzi wasikilizaji katika kipindi hiki maalumu kinachokujieni kwa mnasaba wa kuadhimisha Maulidi ya Bwana Mtume Muhammad SAW na Wiki ya Umoja.

Tunakifungua kipindi chetu hiki kwa aya ya 128 ya Suratu-Tawba isemayo: "Hakika amekwisha kujieni Mtume kutokana na nyinyi wenyewe; yanamhuzunisha yanayo kutaabisheni; anakuhangaikieni sana. Kwa Waumini ni mpole na mwenye huruma."

Aya hii ya Qur'ani tukufu ilikuwa imetoa bishara kwa watu walioko kwenye giza la ardhi wanaotafuta mwanga wa saada na uongofu, wakiwa na matarajio ya kuzaliwa mjumbe wa mwisho wa Mwenyezi Mungu. Na hii ni bishara njema kwa watu wote katika zama zote. Bishara ya kuja Mtume wa rehma na uraufu ambaye nuru ya ujudi wake imeangazia daima dawamu njia ya uongofu wa mwanadamu. 

Amani ya Allah iwe juu ya Muhammad! Amani ya Allah iwe juu ya mwenendo na sira yake inayoongoza kwenye njia iliyonyooka ya kuwa mja halisi wa Mwenyezi Mungu! Amani ya Allah iwe juu ya kifua chake kilicho takasika kinacho zivuta nyoyo za walimwengu kwenye rehma na huruma zake! Amani ya Allah iwe juu ya unyoofu wa maneno yake ambayo yanazigeuza nyoyo ngumu na katili kuwa laini na za huruma! Amani ya Allah iwe juu ya dhihirisho la uja wake wa halisi, ambao unazijaza mapenzi na kuzifikisha kwenye Arshi ya Mwenyezi Mungu nyoyo za umati usiokadirika wa watu! Amani ya Allah iwe juu ya uadilifu wake ulioziunganisha nyoyo za Waarabu na Waajemi, weupe na weusi, masikini na matajiri, mabwana na watumwa na kuwaonyesha kwamba hakuna kipimo kingine cha ubora wa mmoja kwa mwengine ghairi ya taqwa na uchamungu! Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu ya Mtume wa mwisho wa Allah, Muhammad SAW. Tunatoa mkono wa kheri, baraka na fanaka kwa umma wote wa Mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu, kwa mnasaba wa kuadhimisha kuzaliwa kwa nabii huyo wa rehma na mbora huyo wa viumbe.

Jamii ya umma wa Waislamu duniani leo inasherehekea uzawa wa mbora wa viumbe, Nabii Muhammad SAW huku majeraha ya mifarakano yakiwa yametapakaa kwenye mwili wa umma huo. Huo ni umma wa Mtume ambaye amesema: "Mfano wa waumini katika kupendana kwao na kuhurumiana kwao ni mithili ya kiwiliwili kimoja cha mtu ambapo kinapopata maumivu kiungo kimoja, mwili mzima huungulika kwa machungu na maumivu".

Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika aya ya 21 ya Suratul-Ahzab ya kwamba: "Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anaye mtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu sana." 

Kwa mujibu wa aya hii, mwenendo, matendo na sira ya Bwana Mtume Muhammad SAW ni kigezo bora cha kuigwa na kufuatwa na waumini. Ni ubora ulioje kwa jamii ya Waislamu duniani kutumia mwenendo na sira ya mtukufu huyo kwa ajili ya kutibu majeraha na machungu thakili iliyonayo jamii hiyo hii leo. Kwa mnasaba wa kuadhimisha Maulidi ya Nabii wa rehma Muhammad SAW, tumekusudia katika kipindi chetu hiki cha leo kuzungumzia kwa muhtasari sira ya mtukufu huyo katika kuleta umoja wakati wa kuasisi na kujenga jamii ya umma mmoja wa Kiislamu.

Kwa mtazamo wa Qurani tukufu, ubaguzi wa rangi na hisia za ukabila na ukaumu ni mojawapo ya vizuizi vikubwa vya kujenga umma mmoja. Historia inaonyesha kuwa taasubi za rangi na ukaumu zilikuwa zimeirarua vipande vipande jamii ya watu katika zama za kubaathiwa na kupewa Utume Nabii Muhammad SAW. Ubaguzi na upendeleo mkubwa uliotokana na misingi hiyo ulikuwa umetawala na kuzijaza hasadi na chuki nyoyo za watu. Kuiunganisha jamii hiyo iliyogawika vipande vipande ndiyo kazi aliyopaswa kuifanya Bwana Mtume SAW. Kwa amri ya Allah SW, mtukufu huyo aliasisi jamii yenye msingi wa usawa na kuwatangazia watu kwamba kwa mtazamo wa Qur’ani tukufu, taqwa na uchamungu ndicho kitu pekee kinachomfanya mmoja awe mbora zaidi ya mwenzake. Nabii Muhammad SAW hakutofautisha kati ya watumwa na mabwana zao; na kwa tabia na mwenendo wake, aliwaonjesha watu ladha tamu ya usawa, kiasi kwamba wakati alipokuwa akiketi kwenye mkusanyiko wa watu, mtu aliyekuwa hamjui, hakuweza kumpambanua Mtume ni yupi miongoni mwa masahaba zake. Na sababu ni kuwa Nabii Muhammad SAW aliwaenzi na kuwaheshimu kwa usawa waja wote wa Mwenyezi Mungu, awe mtumwa au mtu huru, Mwarabu au Mwajemi na masikini au tajiri; na akikaa na kuchanganyika nao na kuonekana kuwa ni mmoja tu miongoni mwao. Bwana Mtume Muhammad SAW alimfanya kuwa mwanawe wa kulea, Zaid bin Haritha ambaye alikuwa mtumwa wa mkewe Bibi Khadija (sa); na baada ya kuleleka kwenye mafundisho ya Kiislamu akampa ujemadari wa kuongoza jeshi la Waislamu. Kama ambavyo Bilal Mhabeshi, ambaye hapo kabla alikuwa mtumwa mweusi aliyenyongeshwa, ndiye aliyekuwa mwadhini wa kwanza wa Uislamu. Bwana Mtume SAW alitamka pia kuhusu Salman Al-Farsy ambaye hakuwa Mwarabu ya kwamba: “Salman ni katika sisi Ahlul Bayt”. Ni kwa namna hiyo, Nabii huyo wa rehma aliifutilia mbali mipaka bandia ya ubaguzi wa rangi na wa kikaumu ili kuondoa moja ya sababu kuu za kuzusha mpasuko na mfarakano ndani ya umma mmoja wa Kiislamu.

Wakati Bwana Mtume Muhammad SAW alipowasili mjini Madina akiwa na nia ya kuasisi utawala wa Kiislamu, jamii ya mji huo ilikuwa na mchanganyiko wa Waislamu na Mayahudi pamoja na makabila mengine tofauti ambapo baadhi yao kama Aus na Khazraj yalikuwa na visasi na uadui wa zaidi ya karne moja. Muhajirina waliotoka Makka, waliokuwa wameandamana na Bwana Mtume huko Madina na ambao walikuwa wamejitenga na watu wa kaumu na makabila yao kwa sababu ya kulinda dini na imani yao, nao pia walikuwa kundi la jamii nyingine ya watu waliohamia katika mji huo bila ya kuwa na masurufu yoyote ya kuanzia maisha, wakiwa na utamaduni tofauti na wa wenyeji wao. Katika hatua ya kwanza aliyochukua kuiunganisha jamii, Nabii wa rehma Muhammad SAW aliweka kanuni na taratibu kwa ajili ya watu wa Madina na kufungiana mikataba mbalimbali ya ahadi na makabila tofauti ya mji huo. Mayahudi wa Madina walifungiana ahadi na Bwana Mtume SAW ya kuishi pamoja kwa amani na kuahidi kushirikiana na Waislamu kuuhami mji wa Madina endapo utashambuliwa na maadui. Aidha wakatoa ahadi kuwa hawatowasaidia kwa hali na mali makafiri wa Kikureishi wala kufanya nao miamala ya biashara. Ukiutafakari mkataba huo wa kihistoria utabaini jinsi wanadamu walivyopewa heshima katika utamaduni wa kubaathiwa na kupewa Utume Nabii Muhammad SAW. Uhuru wa mtu ulizingatiwa, na ubabe na unyongeshaji watu haukuwa na nafasi yoyote. Katika mikataba hiyo si haki za wahajiri wa Kikureishi na za makabila ya Aus na Khazraj pekee zilizotiliwa mkazo, bali Mayahudi wa kila kabila pia waliandaliwa mazingira ya kuishi kwa amani na Waislamu kwa sharti tu kwamba wasianzishae chokochoko na uadui dhidi yao.

Kufunga “Ahadi ya Udugu” ni tadbiri na hatua nyingine makini aliyochukua Bwana Mtume Muhammad SAW na ambayo ilizidisha mshikamano na kuifanya jamii ya Kiislamu iwe imara zaidi. Bwana Mtume SAW alimuamuru kila Muislamu afunge ahadi ya udugu na Muislamu mwenzake. Uzuri wa mkataba huo unabainika tunapozingatia kwamba baada ya kudhihiri Uislamu, kwa amri ya Mwenyezi Mungu, mafungamano yote ya kikabila na kikaumu hayakuwa na thamani tena, na sasa ahadi na mkataba wa udugu ukawa umefungwa baina ya watu wa makabila na asili tofauti. Wale watu ambao hapo kabla walikuwa watumwa, sasa wakawa ndugu wa wenzao matajiri na wenye umakinifu wa maisha. Mipaka ya kijahilia iliyokuwa ikinyemelea kuipasua vipande vipande jamii ya Waislamu ilitokomezwa, na misingi ya jamii hiyo ikaimarishwa zaidi. Baadhi ya wahakiki wa historia wanaitakidi kuwa mkataba huo wa udugu na usawa wa kidini ulikuwa wenzo imara zaidi wa kuziunganisha nyoyo katika jamii na kielelezo cha wazi cha juhudi za Bwana Mtume SAW za kupanda mbegu za umoja kwa msingi wa imani juu ya Allah. Hivi sasa Waislamu duniani wanahitaji kwa mara nyingine kuuhuisha tena mkataba huo wa udugu baina yao.

Sira ya Nabii Muhammad SAW katika kujenga umoja wa umma mchanga wa Kiislamu ni kigezo bora cha kufuata kwa ajili ya kuunganisha Umma wa Kiislamu katika zama zote. Hivi sasa sio tu tunayo mbele yetu sira ya mtukufu huyo kwa ajili ya kujaza upendo ndani ya nyoyo za Waislamu, bali mapenzi na mahaba yetu kwa Bwana Mtume ni mtaji na rasilimali adhimu iliyomo ndani ya nyoyo za Waislamu bilioni moja na nusu walioko duniani. Shakhsia ya Nabii huyo wa rehma ni mhimili mkuu wa mapenzi na itikadi za Waislamu wote na nguzo kuu ya kuwaunganisha na kuleta umoja baina yao. Katika mafunzo na mafundisho ya Kiislamu hakuna kitu kinachoziunganisha kimapenzi juu yake nyoyo za Waislamu na kuwafanya wawe na rai na itikadi moja kama ujudi na nafsi ya Bwana Mtume Muhammad SAW. Kwa sababu si itikadi za pamoja tu walizonazo Waislamu kuhusiana na Bwana Mtume lakini mapenzi na nyoyo zao pia ziko kitu kimoja juu ya suala hilo. Ndiyo kusema kwamba ujudi na shakhsia ya mtukufu huyo inaweza kuwa mhimili mkuu wa umoja. Na ni sababu hiyo hasa inayowafanya maadui wa Uislamu waamue, mbali na njama zao za kuulenga umoja wa Waislamu, wawe kila mara wanaiandama shakhsia takatifu ya Nabii wa rehma Muhammad SAW ili kuwawekea watu kizuizi cha kushindwa kuwa na ufahamu sahihi kuhusu mtukufu huyo.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu anasema hivi kuhusu suala hilo: “Qur’ani na Al-Kaaba, masuala ya faradhi na itikadi, ni masuala ya wote; lakini kila moja kati ya hayo yanauvuta upande mmoja wa shakhsia ya mtu, kama vile itikadi, mahaba, mielekeo ya kiroho, kufanana katika mambo na katika hulka za matendo. Lakini mbali na hayo, aghalabu ya vitu vyote hivyo vilivyoelezwa vina tafsiri na mitazamo tofauti miongoni mwa Waislamu; ama kile ambacho Waislamu wote wana mtazamo wa pamoja juu yake kifikra na kiitikadi – na muhimu zaidi ya hayo kihisia na kiupendo – ni nafsi takatifu ya Mtume wa mwisho na Nabii mtukufu Muhammad Ibn Abdilllah SAW.  Jambo hili linapasa kupewa uzito. Mapenzi hayo yanapasa kuzidishwa siku baada ya siku na mvuto huu wa kimaanawi na kiroho kuhusiana na shakhsia huyu mtakatifu unapaswa kushadidishwa ndani ya fikra za Waislamu na nyoyo za watu wote.”

Wapenzi wasikilizaji tunahatimisha kipindi chetu hiki kwa maneno ya kuzipa utulivu nyoyo ya Imam Ali (AS). Amirul Muuminin, ambaye katika siku ya kufunga mkataba wa ahadi ya udugu alitajwa na Bwana Mtume SAW kuwa ndiye ndugu yake wa udugu wa kidini amesema: “Nyoyo za waja wema zimejawa na mapenzi ya Mtume, na macho yote yameelekezwa kwake. Cheche cha tumaini inajengeka ndani ya nyoyo zetu hivi sasa, kwa kuwa Mwenyezi Mungu ametuneemesha kwa rehma na utukufu wake, kwa kuyajaza mahaba na mapenzi ya mtukufu huyo nyoyoni mwetu; asaa atatujaalia kuwa kwenye kundi la waja wema; na kwa fadhila zake alizotujaalia kutokana na kuzihuisha nyoyo zetu kwa mahaba ya Mtume atayanawirisha macho ya nyoyo zetu kwa jamali ya sura yake tukufu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

 

Tags