Dec 11, 2016 10:50 UTC
  • Maana ya Umoja na Mshikamano Baina ya Waislamu

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Hamjambo na karibuni kuwa nami katika kipindi cha kwanza cha mfululizo wa makala maalumu za Wiki ya Umoja wa Kiislamu zinazokujieni kwa mnasaba wa sherehe za Maulidi na tukio muhimu la kuzaliwa Mtume wa rehma na upendo, Muhammad (saw) katika mwezi huu wa Mfunguo Sita .

Kuzaliwa kwa Muhammad bin Abdullah (saw) kulikuwa mithili na jua lililochomoza katika zama za giza totoro na kukunja jamvi na ujinga na ujahilia. Tukio hilo lilitoa bishara njema ya kumkomboa mwandamu katika minyororo ya utumwa wa aina mbalimbali, dhulma na matamanio ya nafsi. Ilikuwa kengele ya wito wa Tauhidi na kumwabudu Mungu Mmoja kote duniani na kuwaunganisha wanadamu wote katika kwamba moja iliyonyooka. 

Kwa sasa na baada ya kupita zaidi ya miaka 1400 tangu kuzaliwa kwake, bado tukio hilo la aina yake katika historia ya mwanadamu linazivuta nyoyo za maashiki na wapenzi wa haki, kweli yote, uungwana, na uadilifu. Japokuwa wanazuoni na Waislamu kwa ujumla hususan Shia na Suni wanatofautiana juu ya siku ya kuzaliwa kwake, lakini wote wanaafikiana juu ya mwaka na mwezi aliozaliwa ndani yake. Waislamu wa madhehebu ya Suni wanasema, alizaliwa tarehe 12 Mfunguo Sita (Rabiul Awwal) Mwaka wa Tembo (570 Miladia) na Waislamu wa madhehebu ya Shia wanasema, alizaliwa tarehe 17 Mfunguo Sita mwaka huo huo. Kwa msingi huo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imezitangaza siku za baina ya tarehe 12 hadi 17 Mfunguo Sita kuwa ni Wiki ya Umoja Baina ya Waislamu. 

 

Umoja na mshikamano ni miongoni mwa mafundisho muhimu ya dini ya Uislamu. Japokuwa neno "Wahda" lenye maana ya umoja halikutumiwa katika aya za Qur'ani, lakini maana yake imetajwa katika aya nyingi za kitabu hicho. Kwa mfano tu katika aya ya 103 ya Suratu Aal Imran, Mwenyezi Mungu SW anasema: Na shikamaneni na Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu: vile mlivyokuwa nyinyi kwa nyinyi maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu, kwa neema yake mkawa ndugu. Na mlikuwa ukingoni mwa shimo la Moto, naye akakuokoeni nalo...

Kwa hakika njia na Mwenyezi Mungu ni kuwaita watu katika elimu, maarifa na ufanisi wa milele na kuwatahadharisha na ujinga, uadui na mifarakano. Kwa msingi huo dini ya Uislamu daima inawataka waumini na wafuasi wake kuwa ndugu kama walivyo ndugu wa baba na mama au hata zaidi. Si hayo tu bali Qur'ani baada ya kutilia mkazo umoja na mshikamano baina ya Waislamu inawataka wafuasi wa dini hiyo pia kuungana na wafuasi wa dini nyingine za mbinguni kwa msingi wa Tauhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu. Aya ya 64 ya Suratu Aal Imran inasema: Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno lilio sawa baina yetu na nyinyi: Ya kwamba, tusimuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na chochote; wala tusifanyane sisi kwa sisi kuwa miungu badala ya Mwenyezi Mungu. Na wakigeuka basi semeni: Shuhudieni ya kwamba sisi ni Waislamu.

Kwa msingi huo, hitilafu ndogo ndogo hazipasi kuwa kikwazo cha mshikamano na udugu baina ya Waislamu. Waislamu wana utamaduni wa aina moja na wanashirikiana katika itikadi kuu na muhimu. Wote wanamwamini na kumwabudu Mwenyezi Mungu Mmoja asiye na mshirika, na wanaamini utume wa Nabii Muhammad (saw) na kwamba yeye ndiye Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu. Kitabu chao wote ni Qur'ani Tukufu na kibla chao ni al Kaaba takatifu iliyoko katika ardhi iliyotakasika ya Makka. Waislamu wote wanafanya pamoja ibada ya Hija na kuswali Swala tano kwa siku. Wote wanafunga mwezi mtukufu wa Ramadhani na wanashirikiana katika taratibu na sheria za ndoa, biashara kuzika na kadhalika bila ya kujali tofauti ndogondogo zinazosababishwa na tofauti za kimitazamo na ufahamu wa aya au hadithi baina ya wasomi na wanazuoni wa Kiislamu.  

Hapa linajitokeza swali kwamba, ni nini maana ya umoja wa Kiislamu?

Umoja baina ya Waislamu si umoja wa kimkakati na mbinu ya kutimiza maslahi ya kisiasa. Umoja huo si kama umoja unaofanyika baina ya vyama viwili vya siasa na kadhalika kwa ajili ya kufikia lengo moja kwa muda maalumu. Kwa mfano, iwapo katika jamii ya Waislamu kutakuwepo makundi mawili ya kisiasa, moja likawa la watu wasiokuwa na dini na walahidi na jingine likawa na Waislamu wanaompwekesha Mwenyezi Mungu, haijuzu na haipasi kuwepo umoja na mshikamano baina ya makundi hayo mawili. Hivi ndivyo alivyoamiliana hayati Imam Ruhullah Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wakomunisti wa Iran ambao pia walikuwa wakipambana na utawala wa Shah. Imam Khomeini hakuwanyooshea mkono wa udugu wakomuinisti waliokuwa wakikana itikadi ya Tauhidi na kupiga vita dini na masuala ya kiroho, wala hakuwatambua kuwa ni washirika katika mapambano ya wananchi dhidi ya utawala dhalimu wa Shah. Miezi kadhaa kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Imam Khomeini aliulizwa kwamba: Je utashirikiana na watu wenye fikra na itikadi za kimarxi? Alisema: Malengo yetu yanatofautiana. Sisi tunategemea Uislamu na itikadi ya Tauhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu, ilhali wao wanapinga yote mawili. Sheria zetu ni za Uislamu, na wao hawaukubali Uislamu; hivyo hatutashirikiana nao. Hatushirikiani nao na wala hatutashirikiana nao. (Sahifeye Nour 4:37) 

Kwa msingi huo umoja wa Kiislamu unaokusudiwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran si umoja wa kitaktiki, kimbinu na wa muda tu, bali ni umoja wa kina na wa kudumu unaojenga mshikamano wa kweli na kutayarisha mazingira na uwanja mzuri wa ustawi na kuchanua vipawa vya Waislamu, na kueneza mafundisho ya dini katika jamii ya wanadamu kwa kuwapa watu uhuru wa kuchagua. Hii ni pamoja na kuwa suala la kuanzisha na kujenga umoja baina ya Waislamu ni amri ya Qur'ani tukufu inayowawajibisha Waislamu kushikamana kwa kusema: Na shikamaneni na Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. (Aal Imran:103)  

Umoja na mshikamano wa Kiislamu hauna maana ya kila madhehebu kutupilia mbali itikadi zake. Hakuna anayetatajia kuwa, madhehebu zote za Waislamu zinapaswa kutupiliwa mbali na kuchagua madhehebu moja tu au kuchukua masuala yanayowashirikisha wafuasi wa madhehebu zote na kutupilia mbali mengine na hivyo kuanzisha madhehebu mpya na Waislamu wote. La hasha, maana ya umoja kati ya Waislamu wa Shia na Suni ni kuweka kando masuala waliyohitilafiana juu yake na kusisitiza yale yanayowakutanisha pamoja katika kuamiliana baina yao na katika masuala yanayohusiana na ulimwengu wa Kiislamu na medani ya kimataifa. Kwa kadiri kwamba, Waislamu wote watakuwa na mshikamano na mwelekeo mmoja bila ya kujali hitilafu za kimitazamo na tofauti zao.

Sheikh Muhammad A'shur ambaye ni Naibu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Azhar nchini Misri na Mwenyekiti wa Kamati ya Mazungumzo Baina ya Madhehebu za Kiislamu anasema: Lengo letu si kuunda madhehebu moja na kutupilia mbali madhehebu nyingine za Waislamu; jambo hilo linapotosha fikra ya kukurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu. Mwelekeo wa pamoja wa Waislamu unapaswa kuandamana na mjadala wa kielimu na kutumia silaha hilo kukabiliana na hurafa. Wanazuoni wa kila madhehebu wanapaswa kufanya mijadala ya kielimu na kuelimishana, kukumbushana na kufikia natija.

Umoja baina ya Waislamu wa Shia na Shuni

Umoja kati ya madhehebu za Waislamu ni fursa nzuri kwa pande mbili kujadiliana na kubadilishana mawazo katika anga ya utulivu na kwa kutegemea mantiki na hoja za kielimu. Kwa msingi huo umoja na mshikamano baina ya Waislamu haupingani na kueleza au kuweka bayana ukweli na lililo sahihi.

Kiongozi  Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei ametilia mkazo sana suala la kuwepo umoja na mshikamano baina ya Waislamu akisema: Tumeazimia haswa katika suala hili la umoja baina ya Waislamu na tumeweka bayana nini maana ya umoja huo. Anaendelea kusema kuwa: "Umoja baina ya Waislamu hauna maana ya Waislamu na madhehebu mbalimbali kutupilia mbali na kuachana na itikadi zao makhsusi za kiteolojia na kifiqhi; bali umoja wa Waislamu una maana mbili ambazo zote zinapaswa kutimizwa: Kwanza ni kuwa, makundi mbalimbali ya Waislamu wa Shia na Suni yashirikiane haswa na kwa dhati katika kukabiliana na adui wa Waislamu. Na pili ni kuwa, makundi na madhehebu za Waislamu zifanye jitihada za kukurubiana zaidi, kuelewana, kujuana na kufanya ulinganisho baina ya madhehebu zao za kifiqhi na kisheria. Ayatullah Khamenei anaendelea kusema kuwa: "Kuna fatwa nyingi za maulama na wanazuoni wa fiqhi ambazo iwapo zitachunguzwa kwa kina na kielimu inawezekana zikafanyiwa marekebisho madogo na hivyo kukurubisha zaidi fatwa za madhehebu mbili tofauti. Kauli yetu katika Wiki ya Umoja wa Kiislamu na ujumbe wetu ni kwamba, Waislamu wanapaswa kuungana na kushikamana, waache uhasama na uadui baina yao, na waweke mbele Kitabu cha Mwenyezi Mungu, Suna za Mtume mtukufu (saw) na sheria za Kiislamu." 

Tunamalizia kwa kusisitiza kuwa, maadui wa Uislamu wanaogopa sana umoja na mshikamano wa Waislamu, na wanafanya njama zao baina ya Waislamu kwa kutumia kaulimbiu yao maarufu inayosema"tenganisha upate kutawala". Hivyo ni jambo la dharura kwa Waislamu wote kushikamana na misingi ya dini hiyo inayowakutanisha na kuwaunganisha na kujiepusha na kila kitu kinachozusha mifarakano na kuurudisha nyuma Umma wa Kiislamu.  

اینفوگرافی وحدت: شاهراه اسلام 

       

Tags