Dec 12, 2016 10:43 UTC
  • Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na Fikra ya Umoja wa Kiislamu

Assalamu Alaykum Wapenzi wasikilizaji na karibuni kuwa nami tena katika sehemu nyingine ya makala hizo zinazokujieni kwa mnasaba wa maadhimisho ya Wiki ya Umoja na Maulidi ya Mtume Muhammad (saw). Kipindi chetu leo kitazungumzia Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na fikra ya umoja baina ya Waislamu.

Umoja na mshikamano baina ya Waislamu ni miongoni mwa masuala muhumu sana yaliyosisitizwa na kutiliwa mkazo na Qur'ani tukufu, Mtume (saw) na Maimamu watoharifu katika kizazi chake. Qur'ani tukufu imesifu na kupongeza jambo lolote linalohimiza umoja na mashikamano na kukemea migawanyiko na mifarakano. Kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu kimezungumzia suala la umoja na mshikamano katika aya zake nyingi na kuwataka wanadamu washikamane na kamba ya Mwenyezi wote kwa pamoja na kujiepusha na migawanyiko na hitilafu. Sehemu moja ya Aya ya 103 ya Suratu Aal Imran inasema: Na shikamaneni na Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu: mlivyokuwa nyinyi kwa nyinyi maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu...

Umoja wa Kiislamu ni miongoni mwa fikra na thamani muhimu zaidi ambazo kila Mwislamu tangu zama za awali hadi hii leo, anaihubiri na kuitangaza. Mtume (saw) na viongozi wa Uislamu katu hawakuacha kusisitiza umoja na mshikamano kati ya Waislamu na wameutaja umoja huo kuwa ndiyo siri ya mafanikio na ufanisi wa jamii ya Kiislamu. Mtume Muhammad (saw) amesema: Shikamana daima na jamaa, kwani mbwa mwitu humla mbuzi aliyejitenga na wenzake". Vile amesema katika hadithi nyingine kwamba: Mkono wa Mwenyezi Mungu uko pamoja na umoja na mshikamano, na Shetani huwa pamoja na wale wanaopinga umoja". Vilevile Imam Ali bin Abi Twalib (as) na Maimamu wengine maasumu walinyamazia kimya na kufumbia macho dhulma zilizowapata wao binafsi kwa shabaha ya kulinda umoja na mshikamano wa Kiislamu na walikuwa daima wakisisitiza udharura wa Waislamu wote kushikamana kwa msingi wa itikadi ya Tauhidi, Qur'ani, al Kaaba na kadhalika. Ni kutokana na mafundisho hayo ya Uislamu ndiyo maana Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yakalipa umuhimu mkubwa suala la umoja na mshikamano baina ya Waislamu.

Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran mwaka 1979, hayati Imamu Ruhullah Khomeini aliutangaza umoja baina ya Waislamu kuwa ni kaulimbiu ya kistratijia inayotokana na itikadi na mafundisho ya Kiislamu. Mbali na hayo katiba ya Jamhuri ya Kiislamu pia imewapa wafuasi wa madhehebu zote za Kiislamu uhuru kamili wa kufuata na kushikamana mafundisho na itikadi za madhehebu zao kwa kadiri kwamba, wana haki ya kurejea katika mahakama zinazohukumu kwa mujibu wa fiqhi na sheria za madhehebu zao.  

Hayati Imamu Ruhullah Khomeini

Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika harakati zake za kuimarisha umoja na mshikamano wa Kiislamu ni kuzitangaza siku za kuzaliwa Mtume wa rehma, Muhammad (saw) kuwa ni wiki ya umoja na mshikamno baina ya Waislamu na kuasisi Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu.

Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran daima yamekuwa yakitilia mkazo udharura wa kuwepo umoja baina ya Waislamu na kulitaja suala hilo kuwa ni siri ya izza, heshima na nguvu ya Waislamu. Kwa kutegemea aya ya 46 ya Suratul Anfal inayosema: Wala msizozane msije mkaharibikiwa na kupoteza nguvu zenu. Na subirini, hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanaosubiri, Iran ya Kiislamu imekuwa ikinadi kwa sauti kubwa kwamba, nguvu hiyo inayotokana na umoja na mshikamano wa Waislamu ndiyo itakayouwezesha Umma kusimama kidete na kupambana na maadui zake bila ya woga wowote. Hii leo Wazayuni ambao ndio maadui wakubwa zaidi wa Umma wa Kiislamu wanaikalia kwa mabavu Palestina na kibla cha kwanza cha Waislamu na wanaendelea kuua ndugu zetu wa Palestina kutokana na Waislamu kutoshikamana barabara na aya hiyo na mafundisho ya dini yao. Kwa kutilia maanani suala hilo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliitangaza Ijumaa ya mwisho ya kila mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Quds ili kuwakumbusha Waislamu wajibu wao wa kushikamana kwa ajili ya kuwatetea ndugu zao wa Palestina na kukomboa kibla chao cha kwanza kutoka kwenye makucha ya Wazayuni maghasibu huko Israel. 

Haya yote yanaonesha jinsi Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran yanavyotilia mkazo suala la umoja, udugu na mshikamano baina ya Waislamu bila ya kujali madhehebu wala utaifa wao. Umoja na mshikamano huu wa Kiislamu ndio utakaowatia hofu na woga maadui na kuwazuia kupora mali na utajiri wao ambao unaweza kutumiwa kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa Waislamu na wanadamu wote kwa ujumla.    

Katika upande mwingine, Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran yanataka kuwepo umoja na udugu wa kweli baina ya Waislamu kwa ajili ya maendeleo halisi ya Waislamu wote. Kwa mfano tu, Iran inasisitiza kuwa ustawi wa elimu na teknolojia katika nchi moja ya Kiislamu haupaswi kubakia katika nchi hiyo peke yake, bali zinapaswa kufanyika jitihada za kuhakikisha kwamba, wasomi na wataalamu wa nchi nyingine za Waislamu wanapata elimu na teknolojia hiyo na kueneza maendeleo na ustawi katika nchi zote za Waislamu. Kwa mtazamo huo wa Kiislamu wa Mapinduzi ya Kiislamu unaosisitizwa na aya ya 2 ya Suratul Maida inayosema: Na saidianeni katika wema na uchamungu, wala msisaidiane katika dhambi na uadui... , ushindani unageuka na kuwa urafiki, na Waislamu wote wanashikamana kwa ajili ya maendeleo ya Umma mmoja wa Kiislamu.

Hata hivyo inatupasa kukumbusha hapa kwamba, Mapinduzi ya Kiislamu yanasisitiza umoja na mshikamano baina ya wafuasi wa madhehebu za Kiislamu kama Shia na Suni na kamwe si umoja na mshikamano na makundi anayowakufurisha Waislamu na kuzusha mifarakano na fitna kama yale ya kiwahabi na kisalafi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, msingi wa makundi hayo ni kukufurisha Waislamu, kuzusha mtengano na hitilafu na kumwaga damu za Waislamu wanaoamini kalima ya Tauhidi. Mfano mzuri zaidi wa makundi kama hayo katika kipindi cha sasa na kundi la Daesh linalofanya jinai za kutisha katika maeneo mbalimbali ya dunia, kundi la al Shabab huko Somalia na lile la Boko Haram katika maeneo ya magharibi mwa Afrika. La kusikitisha zaidi ni kuona kwamba, makundi hayo ya kiwahabi yanafanya mauaji ya kutisha kwa kutumia jina la Mwenyezi Mungu, Mtume Wake na Uislamu!

Wapenzi wasikiliza, suala la umoja baina ya Waislamu katika mtazamo wa fikra ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, ni miongoni mwa ajenda muhimu zinazotekelezwa tangu baada tu ya ushindi wa mapinduzi hayo. Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu hayati Imam Khomeini alilitazama suala hilo kwa mtazamo wa kiistratijia. Daima alikuwa akisisitiza kuwa umoja wa kitaifa ni muhimu kwa ajili ya kulinda nchi na uwezo wa kitaifa na vilevile kuzuia uporaji ya maliasili na utajiri wa taifa, na katika upande mwingine alikuwa akitilia mkazo umoja na mshikamano wa Kiislamu ambao anasema, ndiyo nguzo ya izza, heshima ya nguvu ya Umma wa Kiislamu inayozuia kushambuliwa dini, Qur'ani, umoja wao na kuwapa uwezo wa kukabiliana na mustakbirina na mabeberu. Imam Khomeini alikuwa akisema, umoja na mshikamano wa Waislamu ni mti imara ambao matunda yake yatakuwa ushindi wa Waislamu, kuangamizwa maadui na kuchanua vipawa vya Umma wa Kiislamu. Alisisitiza kwamba, umoja na mshikamano huo ndiyo siri ya kubakia hai Waislamu.  

Imam Ruhullah Khomeini daima alikuwa akisema kuwa, kustahamili maneno ya upande wa pili unaotofautiana na wewe katika fikra na mitazamo ni miongoni mwa nguzo muhimu za umoja. Alisisitiza kuwa, wale wanaoeneza hitilafu na mifarakano baina ya Waislamu hawana uchungu na Uislamu bali wanachojali ni maslahi yao binafsi. 

Hayati Imam Khomeini amesema: Siri ya ushindi wa Waislamu katika zama za awali ni umoja na nguvu ya imani vilivyoliwezesha jeshi dhaifu kupambana na kuzishinda tawala kubwa za dunia ya kipindi hicho. Enyi Waislami kote duniani! Enyi wafuasi wa dini ya Tauhidi! Eleweni kwamba, sababu ya mashaka na matatizo ya nchi za Kiislamu ni hitilafu na ukosefu wa umoja na mshikamano, na siri ya ushindi ni umoja na mshikamano. .. Sisi sote tunapaswa kufanya jitihada kwa ajili ya Uislamu na maslahi ya Waislamu na kujiepusha na mifarakano, mtengano na sera za kimakundi ambavyo ndiyo msingi wa matatizo na kubalia nyuma .." Mwisho wa kunukuu.

Kiongozi wa sasa wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei pia kama alivyokuwa hayati Imam Khomeini, analiangalia suala la umoja baina ya Waislamu kwa mtazamo wa kistratijia. Ameutaja umoja wa Waislamu kuwa ni miongoni mwa masuala muhimu sana ya ulimwengu wa Kiislamu na kusisitiza kuwa, lengo la kuwepo umoja si kuwataka Waisalmu wote kuwa na mtazamo wa aina moja, bali ni kwamba mitazamo na mieleleko yao yote iwekwe kwenye kalibu moja na maslahi ya Waislamu yatangulizwe mbele ya masuala mengine. Ayatullah Khameni anasema: Mambo yanayowakutanisha pamoja Waislamu wa madhehebu mbalimbali ni mengi na muhimu zaidi kuliko yale waliyohitilafiana juu yake na kwamba, maadui wanasisitiza sana juu ya mambo ya hitilafu, hivyo Waislamu wa madhehebu tofauti wanapaswa kwenda kinyume chake na kuimarisha masuala yanayowaunganisha. 

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu anasema: Nchi za Magharibi hususan Marekani zinafanya njama za kuzusha hitilafu na mifarakno kati ya Waislamu kwa kutumia majina kama Shia, Suni, au ukabila na utaifa; hivyo, ni wajibu kwa Waislamu wote kuwa macho na kuchukua misimamo imara mbele ya njama kama hizo. 

Tags