Dec 12, 2016 08:00 UTC
  • Umoja katika mtazamo wa wanazuoni wa Kisuni

Wanazuoni wengi wa Kisuni sambamba na wenzao wa Kishia wamekuwa wakitoa wito wa kuwepo umoja katika Umma wa Kiislamu na kutahadharisha dhidi ya madhara ya mifarakano katika umma wa huu. Katika kipindi hiki na kwa mnasaba wa kuwadia Wiki ya Umoja wa Kiislamu tutachunguza baadhi ya mitazamo ya wanazuoni wa Kisuni kuhusiana na suala zima la umoja wa madhehebu ya Kiislamu.

Miladu an-Nabii, yaani siku ya kuzaliwa Mtume Muhammad (saw) ambaye ni mbora wa viumbe vyote ni fursa bora  ya kuwaza na kuchunguza suala la Umoja wa Kiislamu. Nuru ya Mtume huyu ambaye kwa hakika ni rehema ya Mwenyezi Mungu kwa walimwengu, ingali inaangaza ulimwenguni hata baada ya kupita karne 14, na joto la rehema na mahaba yake lingali linazipa uhai mpya nyoyo zilizoganda kwa baridi kali. Mapenzi na mahaba kwa Muhammad (saw) ni moja ya rasilimali za pamoja za Waislamu wapatao bilioni moja na nusu duniani. Miaka 35 iliyopita kipindi cha kati ya tarehe 12 na 17 Rabiul Awwal kilitangazwa katika Jamhuri ya Kiislamu  ya Iran kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu ili kwa njia hiyo Mtume Mtukufu (saw) na Sunna zake ziweze kuenziwa na kutumika nchini kama msingi wa umoja kati ya madhehebu mbalimbali za Kiislamu nchini. Ni vyema kuashiria hapa kwamba Masuni wanachukulia tarehe 12 na Mashia tarehe 17 Rabiul Awwwal kuwa tarehe aliyozaliwa Mtume Mtukufu (saw). Pendekezo la kutangazwa kipindi hiki kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu lilikaribishwa na kupokelewa vyema na Waislamu kote duniani na hasa wanazuoni na maulamaa wa madhehebu ya Suni.

Leo maadui wa Uislamu wanafanya njama za kuzua fitina na mifarakano kati ya madhehebu tofauti za Kiislamu kuliko wakati mwingine wowote ule. Tunaweza kusema kuwa katika kipindi chote cha historia ya Kiislamu hakuna wakati ambao Umma wa Kiislamu uliwahi kugawanyika kama ilivyo hivi sasa. Bila shaka kama ambavyo mikono ya chuki na fitina za wageni imekuwa na nafasi muhimu katika kuzua mifarakano hiyo, ujahili na ujinga wa baadhi ya makundi ya Kiislamu pia umekuwa na mchango mkubwa na kuchukuliwa kuwa kuni za kuendeleza moto wa mifarakano hiyo. Kwa masikitiko makubwa kutokuwa na elimu ya kutosha baadhi ya makundi kuhusiana na hakika na uhalisi wa mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu pamoja na historia yake ni moja ya sababu zinazopelekea wafuasi wa baadhi ya makudi ya Kiislamu kutekeleza unyama na jinai dhidi ya wenzao. Hii ni katika hali ambayo kadiri elimu ya watu inavyozidi kuongezeka kuhusiana na mafundisho ya Kiislamu ndivyo wanavyozidi kuwa na hamu ya kuhubiri umoja na udugu kati ya wenzao. Hii ni kwa sababu licha ya kuwa wanazuoni wa madhehebu tofauti za Kiislamu wanaelewa vyema kuwepo kwa tofauti ndogondogo kwenye matawi ya dini lakini pia wana ufahamu wa kutosha kuhusiana na masuala mengi ya kimsingi yanayokutanisha pamoja madhehebu zao. Ni viongozi wa Kiwahabu tu ndio wasioafikiana na suala hili. Ni wazi kuwa uwahabi uko nje kabisa ya madhehebu za Kiislamu na hata wanazuoni wa Kisuni wanaamini kuwa uwahabi ni kundi bandia lililo mbali na hakika ya Uislamu. Mashekhe wa Kiwahabi daima hupiga ngoma ya fitina na migawanyiko miongoni mwa Waislamu na hivyo kuuletea Umma wa Kiislamu machungu na mashaka yasiyokuwa na mwisho. Amma maulama wengi wakubwa wa Kisuni na Kishia kwa kushikamana kikamilifu na aya ya 103 ya Surat Aal Imran katika Quráni Tukufu inayosema: Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane, wamekuwa wakifanya juhudi kubwa za kutibu maradhi haya sugu ya Umma wa Kiislamu kwa kutumia dawa mujarabu ya umoja.


Shahid Hassan al-Banna, mwasisi wa Harakati ya Kimataifa ya Ikhwanul Muslimeen ambayo ilikuwa na athari kubwa na ya kina kwa fikra za Kiislamu katika karne iliyopita ya 20, alikuwa mmoja wa waanzilishi wa fikra ya kuwepo umoja miongoni mwa Mashia na Masuni. Yeye na kundi la wanazuoni wa Kisuni na Kishia waliafikiana kwamba Waislamu wote Mashia kwa Masuni wazingatie misingi ya pamoja na kujiepusha na masuala madogomadogo ambayo si katika misingi ya dini na ambayo kuyapinga hakumtoi Mwislamu katika dini. Wanazuoni hao waliokuwa mashuhuri na kuheshimiwa sana katika madhehebu za Shia na Suni walisisitiza kwamba Mwislamu ni yule anayemwamini Mwenyezi Mungu mmoja yaani Allah, na kwamba Mtume Muhammad (saw) ni Mtume wake wa mwisho na pia kukiamini kitabu kitakatifu cha Quráni, al-Kaaba kuwa kibla na Nyumba ya Mwenyezi Mungu, Siku ya Kiama na kutekeleza mambo yote ya kimsingi katika dini.

Hassan al-Banna

Huku akisema kuwa hitilafu kati ya Shia na Suni si za msingi, Sheikh Muhammad Ghazali mwanafikra wa zama hizi wa Kisuni anasema: ''Itikadi pia imeathirika na siasa na utawala kwa sababu umashuhuri na kutafuta ubora na utumiaji mabavu umeingiza humo mambo ambayo hayako kwenye itikadi hiyo na tokea wakati huo Waislamu wamegawanyika katika makundi mawili makubwa ya Shia na Suni pamoja na kuwa makundi mawili haya yote yanamwamini Mwenyezi Mungu mmoja na ujumbe wa Muhammad (saw).' Anaendelea kusema: 'Licha ya kuwa mimi nina mtazamo tofauti na Mashia katika masuala mengi ya kisheria (fiqhi) lakini siamini kwamba kila mtu anayetofautiana na mimi kimtazamo ni mtenda dhambi. Msimamo wangu ni hivyohivyo kuhuhusiana na baadhi ya mitazamo mashuhuri ya kifik'hi kati ya Masuni.' Sheikh Muhammad Ghazali ambaye anaamini kikweli kwamba uchochezi wa hitilafu kati ya Suni na Shia ni njama zinzazofanywa na maadui wa Uislamu anaandika: 'Hatimaye (maadui wa dini) wamefungamanisha pengo lililopo kati ya Shia na Suni na misingi ya kiitikadi! Ili dini ambayo ni moja igawanyike katika makundi mawili na umma ambao ni mmoja ugawanyike katika matawi mawili na kila moja kulenga la pili bali kulitakia mauti! Kila mtu anayesaidia mgawanyiko huo hata kama itakuwa ni kwa neno moja tu basi atakuwa amejumuishwa kwenye aya ifuatayo: Hakika walioigawa Dini yao na wakawa makundi makundi, huna ukhusiano nao wowote. Bila ya shaka shauri yao iko kwa Mwenyezi Mungu; kisha atawaambia yale waliyokuwa wakiyatenda (6:159).

Sheikh Ghazali anaendelea kusema: 'Katika uwanja wa fik'hi ya mlingano, tunapochunguza matatizo na hitilafu za kifik'hi zilizopo kati ya fikra hii na ile tunaona kwamba tofauti iliyopo baina ya Shia na Suni ni ileile iliyopo baina ya mitazamo ya kifik'hi ya Abu Hanifa na Malik au Shafi'.....Sisi tunawachukulia wote hao kuwa wanatafuta hakika, hata kama mbinu zao zitakuwa zinatofautiana.'

Muhammad Ghazali

Sheikh Muhmoud Shaltut ni miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa Kisuni, mtafiti, mfasiri wa Quráni Tukufu, fakihi, mmoja wa viongozi mashuhuri wa zamani wa Chuo Kikuu cha kidini cha al-Azhar na mmoja wa waasisi wa Dar at-Taqrib kwa ajili ya kukurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu. Sheikh Shaltut ambaye alikuwa miongoni mwa watetezi na waungaji mkono wakubwa wa umoja wa Shia na Suni alikuwa na uhusiano mkubwa na wa kirafiki na Ayatullah Sayyid Hussein Burujerdi, Alim mkubwa na marja taklidi wa Mashia. Sheikh Shaltut anasema katika fatwa yake mashuhuri kuhusiana na madhehebu ya Shia: 'Madhehebu ya Jaafari mashuhuri kama madhehebu ya Shia Ithna Ashari ni madhehebu kama zilivyo madhehebu nyingine zote za Ahlu Sunna na kuifuata ni jambo linalojuzu na Waislamu wanapasa kulijua hili na kujiepusha na taasubi isiyofaa kuhusiana na madhehebu fulani.' Kuhusiana na moja ya vikao vilivyoandaliwa na Dar at-Taqrib kwa ajili ya kulinda umoja miongoni mwa Waislamu, Sheikh Shaltut anasema: 'Laiti lingeliweza kuzungumza kuhusiana na vikao vya Dar Taqrib, ambapo Mmisri, Muirani,  Mlebanoni, Muiraki, Mpakistan au wengineo kutoka mataifa ya Kiislamu wengeliketi pamoja na Mhanafi, Mmaliki, Mshafi' na Mhambali kuketi kwenye meza moja na Muimami na Mzeidi na kupaza sauti moja ya kujadili elimu, usufi na fik'hi, mbali na kuimarisha moyo wa udugu, ladha ya mahaba, mapenzi na ushirikiano katika uwanja wa elimu na irfani.' Sheikh Shaltut pia ameandika hivi kuhusiana na watu wasiokuwa na uelewa wa mambo waliokuwa wakipinga kuasisiwa kwa Dar at-Taqrib: 'Watu walio na mitazamo finyu wanakabiliana na fikra ya umoja kama ambavyo kundi jingine lililo na nia mbaya linapiga vita fikra hii. Hakuna umma wowote usiokuwa na watu wa aina hii. Wale wanaoona kwamba kubakia kwao na maisha yao yanadhaminiwa na migawanyiko, wanakabiliana na fikra hii na watu wenye nia mbaya, matamanio na mielekeo maalumu wanapambana na fikra ya kubuniwa Dar at-Taqrib. Makudi mawili haya yote ni ya wale watu ambao wameuza na kutumia kalamu zao kwa ajili ya kueneza siasa za mifarakano! Siasa ambazo hukabiliana kwa njia ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja na kila harakati ya marekebisho, na kusimama mbele ya kila jambo ambalo hutekelezwa kwa ajili ya kuleta umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu.'

Sheikh Mahmoud Shaltut

Katika utangulizi wa Kitabu chake alichokipa jina la 'al-Muslimun....Man Hum', yaani Waislamu ni akina nani, Ustadh Samih Atif az-Zain mmoja wa wanazuoni mashuhuri wa Kisuni anasema: 'Kilichonipelekea kuandika kitabu hiki ni mgawanyiko wa kipumbavu unaoonekana hii leo latika jamii yetu, na hasa mgawanyiko unaoonekana kati ya Waislamu wa Kishia na Kisuni, mgawanyiko ambao ulipasa kufutwa kabisa kwa kufutwa ujahili, lakini kwa bahati mbaya ungali una mizizi kwenye nyoyo zilizo na maradhi. Hii ni kwa sababu chanzo chake kinapatikana kwenye tabaka lilelile ambalo limekuwa likiutawala ulimwengu wa Kiislamu na kuwa adui wa dini kwa kuanzisha fitina.' Anaamini kwamba kamwe hitilafu kati ya Shia na Suni hazijatokana na Quráni na Suna bali zimetokana na ufahamu mbaya wa vyanzo viwili hivi vya sheria za Kiislamu. Mwishoni anasema: 'Tunapasa kufuta moyo muovu wa mifarakano na kuwafungia njia wale wote wanaoeneza chuki za kidini, ili kuweza kuwafanya Waislamu wote kuwa kundi moja linaloshirikiana na kupendana kama ilivyokuwa zamani.'


Ustadh Swabir Twahima, mmoja wa wanazuoni mashuri wa Kisuni katika zama hizi pia anasema: 'Hakuna tofauti yoyote iliyopo baina ya Shia na Suni kuhusiana na misingi mikuu...bali hitilafu zilizopo zinahusiana tu na matawi, hitilafu ambazo kwa hakika ni mfano wa hitilafu zilizopo kati ya madhehebu za kisuni zenyewe (Shafi', Hambali ......). .....Ukweli ni kwamba Suni na Shia ni madhehebu mbili miongoni mwa madhehebu za Kiislamu ambapo kila moja inatoa mafundisho yake kwenye Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna za Mtume.'

Allama Imam Sayyid Abul Hassan Ali Nadawi ni mwanafikra, alim na muhubiri mashuhuri wa Kisuni wa karne ya sasa ambaye pia alikuwa na matumaini makubwa ya kuona kwamba Shia na Suni wanakaribiana. Anasema: Iwapo ukaribu na ukuruba huu utapatikana baina ya Shia na Suni, bila shaka kutatokea mapinduzi makubwa yasiyo na mfano wake katika historia ya kuhuisha fikra ya Kiislamu.'

Mwishoni, tunatumai kwamba Waislamu kote duniani watarejea elimu na mafundisho ya wanazuoni wao wakubwa katika kila madhehebu, kushikamana kikamilifu na mafundisho ya Quráni na Mtume Mtukufu (saw) na kwa mara nyingine tena kuasisi Umma mmoja na mkubwa wa Kiislamu.

Tags