Sep 20, 2017 07:48 UTC
  • Muharram, Mwezi wa Kujisabilia na Kuuliwa Shahidi

Tunaingia katika siku ya kwanza ya mwezi wa Muharram mwaka 1439 Hijria Qamariya.

Muharram ni mwezi wa kwanza wa kalenda ya mwaka wa Hijria na mwezi huo uliheshimiwa na Waarabu hata kabla ya kudhihiri dini ya Uislamu. Katika mwezi huo Waarabu walikuwa wakiharamisha vita na umwagaji wa damu. Kuharamishwa vita katika mwezi wa Muharram ilikuwa moja kati ya njia za kukomesha mapigano ya muda mrefu kati ya makabila ya Kiarabu na wenzo wa kurejesha amani na utulivu. Ada hiyo nzuri iliendelea kuheshimiwa katika zama za ujahilia na ushirikina hadi kipindi cha kudhihiri Uislamu. Dini hiyo pia ilipasisha suna na ada hiyo na kuifanya sheria kwa Waislamu wote. Hata hivyo katika mwaka wa 61 Hijria watawala madhalimu na majahili wa Bani Umayyah waliivunjia heshima Nyumba tukufu ya Mtume wa Mwenyezi Mungu katika mwezi huo kwa kumuua shahidi na kumkata kichwa mjukuu wa Mtume wetu Muhammad (saw) Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as), watoto, ndugu na masahaba zake wema katika ardhi ya Karbala. Tangu wakati huo mwezi wa Muharram ulifungamana na jina la Imam Hussein (as) na daima unakumbusha ushujaa na kujisabilia kwa wanadamu waliosimama kuamrisha mema na kukataza maovu na vilevile kuhuisha thamani na maadili ya dini aliyokuja nayo Mtume Muhammad (saw). Tarehe 10 ya mwezi wa Muharram historia ya mwanadamu ilishuhudia tukio lililovunja kuta za mahala na zama na kuvuka mipaka ya kijiografia na kihistoria na kutoa ilhamu na somo kwa ajili ya vipindi na zama zote.   

Tunapotazama kwa haraka mwenendo wa harakati ya Imam Hussein (as) katika mwezi wa Muharram mwaka 61 Hijria, inatubainikia hakika kwamba, lengo la kimsingi kabisa la fikra ya mtukufu huyo lilikuwa kutekeleza wajibu na amri ya Mwenyezi Mungu na kutafuta radhi zake Mola Muumba. Jambo lililomfanya Imam kusimama kwa ajili ya kukabiliana na uovu wa zama hizo ni upotofu wa utawala wa Bani Umayyah na baadaye jamii nzima ya Kiislamu kutoka kwenye vigezo halisi na sahihi vya Uislamu. Hali hiyo ilikuwa matokeo ya uhakika mchungu ulioumbika na kujitokeza taratibu na hatua kwa hatua katika kipindi cha miaka 50 ya baada ya kuaga dunia Mtume Muhammad (saw). 

Kusahaulika wasia wa Mtume Muhammad (saw), kutengwa Ahlubaiti wake (as), kutoweka masuala ya kiroho katika jamii, kukita mizizi tabia na uchu wa kujilimbikizia mali na utajiri baina ya watawala na wenye mamlaka, kuenea kwa bidaa, uzushi na opotofu ni miongoni mwa sababu zilizotayarisha uwanja wa kurejea jamii katika zama za ujahilia. Kipindi hicho mwenendo wa kuporomoka jamii ya Kiislamu ulikuwa ukienda kwa kasi kiasi kwamba, hatamu za Umma wa Kiislamu zilishikwa na mtawala fasiki na muovu kama Yazid bin Muawiyya. Jamii ya Kiislamu iliyokuwa na tajiriba ya kuongozwa na shakhsia adhimu kama ya Mtume Muhammad (saw), ilishuhudia mtu muovu na habithi kama Yazid akishika madaraka. Mtawala huyo alipuuza na kukanyaga misingi yote ya Uislamu na kujishughulisha na ufuska, maovu na maasi ya aina mbalimbali.

Katika upande mwingine mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam Hussein (as) alikabiliana na utawala uliokuwa ukifikiria tu maslahi yake na ulihalalisha kila kitu, kutenda dhulma na kupotosha mafundisho sahihi ya dini kwa ajili ya kufikia maslahi hayo. Imam aliona kwamba, Umma umekumbwa na hali ya mporomoko wa kimaadili ambayo imewafanya Waislamu kuwa watu wasio na irada na wasiojali lolote. Japokuwa walielewa haki na kweli, lakini aghlabu ya Waislamu hao walitilia maanani maslahi yao binafsi bila ya kujali hatima ya Umma na maslahi muhimu ya Uislamu.

Katika kipindi hiki suala lililokuwa muhimu sana kwa mtawala Yazid bin Muawiya na jamaa zake lilikuwa kupata uungaji mkono na mkono wa utiifu kutoka kwa watu adhimu na wakubwa kama Imam Hussein (as). Ilieleweka wazi kwamba, Imam Hussein (as) kamwe asingetoa mkono wa utiifu kwa mtawala fasiki na muovu kama Yazid, kwa sababu kufanya hivyo kulikuwa na maana ya kuunga mkono na kupasisha utawala muovu. Hivyo mtukufu huyo aliyeelewa vyema hatari ya madaraka na utawala kuwa mikononi mwa watu laghai na wanaojidhihirisha katika vazi la dini na uchamungu, alianzisha mikakati na wimbi la mwamko na kuzindua watu kidini, kijamii na kisiasa katika jamii ya Kiislamu. Imam alieleza wasifu wa watala kama Yazidi akisema: "Watu wa aina hii ni watumwa wa dunia, na dini ni mchezo tu katika ndimi zao. Hushikamana na dini pale inapohudumia maslahi yao na wanapopatwa na misukosuko, basi wenye kushikama barabara na dini huwa wachache". Bani Umayyah waliifanya dini ya Uislamu kuwa wenzo wa kutimizia malengo yao ya kisiasa na walipotosha au kubadili kwa ndani maana halisi ya mafundisho ya dini hiyo. Kwa kuelewa vyema harakati hiyo ya kupotosha na kuyumbisha mafundisho ya dini, Imam Hussein (as) alijifunga kibwebwe kupambana na utawala wa zama hizo na kufichua malengo ya watawala na hali ya kisiasa na kijamii ya kipindi hicho. Kwa msingi huo pia alikataa kumpa mkono wa utiifu mtawala Yazid bin Muawiya.

Hatua ya Imam ya kukataa kumpa mkono wa utiifu gavana wa Yazid katika mji mtakatifu wa Madina ilisababisha mazingira magumu sana kwa Imam na kizazi cha Mtume Muhammad (saw). Hivyo Imam alichukua uamuzi wa kuondoka Madina. Wakati huo mji mtakatifu wa Makka ulikuwa eneo zuri zaidi kwa ajili ya kudumisha mapambano ya Imam Hussein dhidi ya utawala muovu wa Yazid. Hasa kwa kutilia maanani kwamba, msimu wa ibada ya Hija ulikuwa umekaribia ambapo Waislamu kutoka maeneo mbalimbali ya dunia hukusanyika katika mji huo kwa ajili ya ibada hiyo. Suala hilo lilikuwa fursa adhimu kwa Imam kuweza kubainisha malengo ya harakati yake ya kufanya marekebisho katika Umma wa babu yake. Imam Hussein alisema wakati anaondoka Madina kwamba: Ninaondoka Madina kwa ajili ya kufanya marekebisho katika Umma wa babu yangu. Nataka kuamrisha mema na kukataza maovu na kurejesha sira na mwenendo wa babu yangu, yaani Mtume Muhammad (saw), na baba yangu, yaani Ali bin Abi Twalib (as)

Baada ya kuwasili Makka, Imam Hussein alifanya jitihada kubwa za kutayarisha mazingira mazuri kwa ajili ya harakati ya mageuzi na mapambano dhidi ya utawala muovu. Wakati huo watu wengi wa Iraq na maeneo mengine walitaka kumpa Imam mkono wa utiifu na walimwandikia barua nyingi wakimtaka ahamie Iraq na kumuahidi kumsaidia na kuwa naye bega kwa bega katika harakati hiyo ya mageuzi na marekebisho ndani ya Umma. Hata hivyo wengi kati ya watu hao waliogopa na kughairi azma yao ya kumsaidia Imam kutokana na mazingira magumu ya mbinyo, vitisho na ukandamizaji mkubwa wa utawala wa Yazid bin Muawiya. Baadhi ya wengine walikumbwa na tamaa ya mali ya dunia, madaraka na hadaa za aina mbalimbali na wakampa mgongo Imam na kizazi cha Mtume. Watu hao ambao dunia iliziba macho na masikio yao, walielewa vyema kwamba, Hussein ni mjukuu wa Mtume na bwana wa vijana wa peponi, kama walivyofundishwa na kuambia katika mafundisho ya Uislamu. Hata hivyo walimpa mgongo na kumuacha peke yake. Imam Hussein (as) akiwa pamoja na watu wa familia ya Mtume, ndugu, watoto na msahaba wake, walikatiza safari ya Hija na kuelekea Kufa huko Iraq. Hata hivyo walizingirwa na jeshi la mtawala mal'uni Yazid katika jangwa la Karbala. Imam na wafuasi wake wachache walikataa kusalimu amri kwa utawala wa Yazid uliomtaka atoe mkono wa utiifu na kumkubali mtawala huo dhalimu. Hatimaye katika siku ya tarehe 10 mwezi wa Muharram mwaka 61 Hijria ambayo ni maarufu kwa jina la A'shuraa, mjukuu huyo wa Mtume Muhammad (saw), watoto, ndugu na masahaba zake waaminifu waliuawa shahidi kikatili na kuchinjwa wakiwa na kiu katika eneo la Karbala nchini Iraq. 

Harakati ya Imam Hussein (as) ilikuwa na matunda ya aina mbalimbali katika medani za siasa na jamii. Hii leo na baada ya kupita karne kadhaa tangu wakati wa harakati ya A'shuraa, jina la Hussein bin Ali bin Abi Twalib linazivuta kama sumaku na kuzisisimua nyoyo za wapenda haki na uadilifu kote dunia. Harakati hiyo ya marekebisho na mageuzi ilisimama juu ya misngi na mambo ambayo yanaungwa mkono na kukubaliwa na wanadamu katika zama na maeneo yote. Awamu zote za harakati hiyo ziliambatana na kumuweka mbele Mwenyezi Mungu, kupigania uadilifu, kupambana na dhulma na uaonecvu, kusisitiza heshima na utukufu wa mwanadamu na kadhalika. Harakati hiyo ilitoa darsa na somo kubwa la ubinadamu na matukufu ya kibinadamu. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana harakati ya mjukuu huyo wa Mtume Muhammad (saw) ikaendelea kutoa ilhamu, ibra na darsa kwa vizazi vyote.

Kwa hakika siku ya A'shuraa haikuwa tukio la siku moja na na la kupita, bali mwanga na mwongozo wake utaendelea kuwa tochi kwa Waislamu bali wanadamu wote wanaopinga dhulma na uonevu na kupigania haki, uadilifu na maadili ya kibinadamu. Darsa hii ya Imam Hussein na mapambano ya Ashuraa mwaka 61 Hijria itaendelea kutoa ilhamu maadamu dunian inaendelea kushuhudia mpambano baina ya haki na batili. Hivyo basi ni sahihi kabisa kusema kwamba: Kila siku ni A'shuraa, na kila ardhi ni Karbala.

Tags