Arubaini ya Imam Husain AS 1437 Hijria
(last modified Wed, 08 Nov 2017 05:27:38 GMT )
Nov 08, 2017 05:27 UTC
  • Arubaini ya Imam Husain AS 1437 Hijria

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Takribani miaka 1376 iliyopita, ilifanyika majlisi ya kwanza ya siku ya Arubaini tangu kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) Imam Husain bin Ali (AS) akiwa na watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume ambao waliuawa shahidi tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijria.

Majlisi za siku ya Arubaini hufanyika kila mwaka baada ya kupita siku Arubaini tangu tarehe 10 mwezi wa Muharram kwa ajili ya kukumbuka mauaji ya kikatili ya mjukuu wa Mtume Imam Husain AS na masahaba zake ambao walijitolea roho zao kwa ajili ya kuhuisha dini ya Mwenyezi Mungu katika jangwa la Karbala. 

Naam, mwezi 20 Mfunguo Tano Safar inasadifiana na siku ya Arubaini tangu alipouawa shahidi Imam Husain AS na wafuasi wake waaminifu 72. Siku ya Arubaini baada ya tukio la Karbala mwaka 61 Hijria ndipo mateka wa Karbala kutoka kizazi cha Bwana Mtume SAW walifika kwenye eneo hilo kutoka Sham wakiwa njiani kurejea Madina. Vile vile mwezi 20 Mfunguo Tano Safar mwaka 61 Hijria ndipo sahaba mkubwa wa Bwana Mtume Muhammad SAW, Jabir bin Abdullah al Answari alipofanya ziara katika kaburi la Imam Husain AS.

 

Wapenzi wa Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad SAW hivi sasa wako katika kilele cha kumbukumbu ya Arubaini ya Husain AS ambayo ilifanyika kwa mara ya kwanza baada ya kupita siku arubaini tokea lilipojiri tukio la Ashura. Hii ni Arubaini ya Ashuraa ya damu na mwamko, ni Arubaini ya Ashuraa ya vichwa vilivyochinjwa ni Arubaini ya Ashuraa ya viwiliwili ya watu wa nyumba tukufu ya Bwana Mtume Muhammad vilivyodungwa mishale na watoto walioadhibiwa! Ni Arubaini inayosimulia namna mahema yalivyoteketezwa moto na makatili walivyowaua shahidi watu wasio na hatia. Ni siku ya Arubaini ambayo wana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW walikuwa wakihangaika katika jangwa lenye masaibu mengi wakiwa na majeraha na uchofu mkubwa wa safari, njaa na kiu.

Mtawala wa zama hizo, Yazid ibn Muawiya alifurahia hali hiyo akiwa na dhana potofu kuwa ametekeleza haki. Hata hivyo, kusimama kidete na ushujaa wa Bibi Zainab SA na Imam Sajjad AS ulisambaratisha njama chafu ya Yazid na vibaraka wake. Hivi sasa walimwengu wote wanakiri kuwa Imam Husain AS, Bwana wa Mashahidi ndiye aliyepata ushindi wa milele. Ahlul Bayt wa Mtume SAW ni kati ya vizito viwili ambavyo Mtume Muhammad SAW aliuachia Umma wa Kiislamu ili viwe kinga ya kutotumbukia katika mkondo potofu.

Mtume SAW amenukuliwa akisema: Anawaachia Waislamu vizito viwili vyenye thamani ambavyo iwapo watashikamana navyo kamwe hawatapotea; navyo ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Itrah yake yaani Ahul Bayt au Watu wa Nyumba yake."

Wakati bendera ya mwamko wa Aba Abdillahil Husain AS ilipoanguka ikiwa mikononi mwa mbeba bendera wake yaani Abul Fadhl al Abbas bin Ali AS na kichwa kitukufu cha Imam Husain AS kikaanguka chini mbele ya Ahlu Bayt wake kikiwa kimedungwa mishale, Yazid na vibaraka wake walidhani kuwa wamefanikiwa kuwapokonya Waislamu moja kati ya vitu viwili vyenye thamani na kwamba kwa hatua yao hiyo wangeweza kupotosha Qu'rani ambayo ni kati ya vizito viwili tulivyoachiwa na Mtume SAW.

Je, rafiki haitikii ombi la rafiki yake

 

Hata hivyo, kwa irada na mapenzi ya ya Mwenyezi Mungu, damu ya Husain AS daima inachemka katika mishipa ya Waislamu wanaofuata haki na wapenda uadilifu kote duniani Arubaini ya Imam Husain AS daima imekuwa ikikumbukwa na Waislamu hasa wa madhehebu ya Shia. Wapenzi wa Ahlul Bayt wa Mtume SAW, tokea mwaka wa kwanza wa kuuawa Shahidi Imam Husain AS wamekuwa wakifanya ziara katika Haram yake takatifu. Sunna hii ingali inaendelezwa na hadi leo tunashuhudia mamilioni kwa mamilioni ya Waislamu kutoka pembe zote za dunia wakijumuika katika Haram Takatifu ya Imam Husain AS huko Karbala Iraq na kutangaza utiifu na kushikamana kwao na njia ya Imam Husain AS na jinsi walivyo chini ya kivuli cha Wilaya yake. Wapenzi hao wa Bwana Mtume Muhammad SAW wanatumia fursa hiyo kutangaza kwamba kamwe hawatosalimu amri mbele ya dhulma na kwamba watajitolea muhanga katika njia hiyo ya kuutetea Uislamu.

Jabir bin Abdullah Ansari, Sahaba mkubwa wa Bwana Mtume alikuwa mfanya ziara wa kwanza aliyefika Karbala katika siku ya Arubaini tangu alipouawa shihidi kidhulma Imam Husain AS katika jangwa la Karbala mwaka 61 Hijria. Pamoja na kwamba Sahaba Jabir al Answari alikuwa kipofu, lakini alifika katika maziara hayo ya Imam Husain AS akiwa ameandamana na Atiya Bin Saeed Al-Kufi ambaye anajulikana pia kwa lakabu za al Ufi, Jadali na Qeysi. Akiwa pamoja na mwanazuoni mkubwa wa fikhi na mfasiri wa Qur'ani, Sahaba Jabir al Ansari walifanya ziara kwa pamoja katika kaburi takatifu la Imam Husain AS. Attiya Al-Kufi amenukuliwa akisema: "Tuliwasili Karbala na Jabir kwa lengo la kuzuru kaburi la Imam Husain AS... Punde baada ya kuwasili Jabir aliniambia hivi: 'Nipeleke katika kaburi la Husain.' Mimi niliushika mkono wake na kuuweka juu ya kaburi la Imam Husain AS. Hapo Jabir alianguka juu ya Kaburi na kuzimia. Nilimwaga maji kwenye uso wake na alipopata fahamu alisema mara tatu mfululizo..: Ya Husain! Ya Husain! Ya Husain! Kisha akaendelea kusema: 'Ewe Husain mbona hunijibu?" Kisha akasema: 'Ni vipi utaweza kunijibu wakati mishipa ya koo lako imekatwa na kichwa chako kimetenganishwa na mwili wako?' Nashuhudia kuwa wewe ni mwana wa Mtume wa Mwisho na Bwana wa Waumini... Sala, Salamu na Radhi za Allah ziwe juu yako."

 

Kumbukumbu za kale kabisa za historia ya Uislamu zimetaja suala la kumbukumbu ya Arubaini ya Imam Husain na kwamba watu wakubwa wakiwemo maswahaba na tabiina walivyokuwa wanamzuri Imam Husain na kukumbuka Arubaini yake. Ushahidi muhimu zaidi kuhusu hili ni Riwaya ya Imam Askari AS ambaye amenukuliwa akisema: "Ishara za muumini wa kweli wa Ahlul Bayt wa Bwana Mtume Muhammad SAW ni katika vitu vitano: Kusali rakaa 50 kila siku ambazo zinajumuisha sala za faradhi na sunna, Ziara ya Arubaini, kuvaa pete katika mkono wa kulia, kusujudu katika udongo na kusema Bismillahir Rahmanir Rahim kwa sauti katika sala."

Katika riwaya nyingine imenasihiwa kuwa, watu ambao katika siku ya Arubaini hawawezi wao binafsi kufika Karbala, wasome Ziara ya Arubaini wakiwa mbali. Jambo hili linaashiria umuhimu wa kumbukumbu ya Arubaini ya Imam Husain AS ambayo pia ni kumbukumbu katika Kamusi ya Kiislamu kuhusu utamaduni wa kupinga dhulma. Kutoka Siku ya Ashura alipouawa shahidi Imam Husain AS na wafuasi wake 72 hadi Arubaini ya mtukufu huyo, kuna kipindi cha mwezi mmoja na siku kumi. Katika siku hizo arubaini ni Bibi Zainab SA ambaye kwa busara na ujasiri sawa na wa Imam Ali AS ndiye aliyefelisha kikamilifu njama na ndoto za Yazid za kufuta utajo na kumbukumbu za Bwana Mtume na Ahlul Bayt wake watoharifu.

Hii ni kwa sababu Bibi Zainab SA aliendelea kuinua bendera ya harakati ya Imam Husain AS na ndio sababu hadi leo bendera hiyo ingali inapepea kwa nguvu. Ni machozi ya simanzi, majonzi na huzuni kubwa ya Bibi Zainab SA tangu Ashura hadi Arubaini ndiyo yaliyoweza kusambaza ujumbe wa kudhulumiwa na wa kup[igania haki wa Imam Husain AS. Hotuba kali alizotoa Bibi Zainab zilitikisa kasri ya kila dhalimu na kuvutia wimbi kubwa la watu kila mwaka kuelekea katika jangwa la Karbala. Mbali na sifa zake za kipekee pamoja na cheo na utukufu aliokuwa nao Bibi Zainab SA kutokana na kuzaliwa katika familia ya Wahyi, pia alikuwa na nafasi muhimu sana katika kufanikisha Harakati ya Ashura na mwamko wa Imam Husain AS.

Baada ya tukio chungu la Ashura, Bibi Zainab AS alichukua nafasi ya mlezi wa mateka na mlinzi wa Imam Sajjad AS ili asikumbwe na hatari. Kutokana na kustahamili kwake masaibu, bibi huyo mtukufu aliweza kuipa ushindi kamili harakati ya kimapinmduzi ya Imam Husain AS. Katika kutekelelza majukumu yake, Bibi Zainab SA alisimama kidete na kwa ushujaa mkubwa kuhakikisha kuwa hakuna upotofu wowote utakaozima nuru ya Uislamu na Sunna za Mtume SAW na mapambano ya Imam Husain AS huko Karbala.

 

Wakati msafara wa mateka wa Karbala ulipowasili Kufa, kundi la kwanza la watu waliokuwa na furaha walienda kuwapokea mateka hao ambao walijumuisha wanawake, watoto na askari. Lakini Bibi Zainab SA alitoa hotuba kali na nzito iliyobainisha ukweli na ukubwa wa dhulma na usaliti waliofanyiwa Ahlul Bayt wa Mtume SAW. Baada tu ya kusikia hotuba hiyo, nyoyo zilizokuwa zimejaa mghafala za watu wa Kufa zilizama katika majonzi na maombolezo. Katika sehemu moja ya hotuba yake hiyo, Bibi Zainab SA alisema: 'Enyi watu waovu, wasaliti wenye hadaa na msioaminika....! Ni vipi mumemuua kipenzi cha Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW na Bwana wa Vijana wa Peponi? Yeye ndiye yule yule ambaye aliwapa hifadhi wakati wa vita na alikuwa chanzo cha utulivu wenu wakati wa amani. Je, mnajua ni vipi mlivyomuumiza roho Mtume wa Mwenyezi Mungu na ni vipi mlivyovunja ahadi?" Kwa maneneo mazito ya Bibi Zainab SA idadi kubwa ya watu wa Kufa walitambua ukubwa wa dhambi zao.

Aidha Bibi Zainab SA alipofika katika Kasri ya liwali Obaidullah ibn Ziad huko Kufa, liwali huyo alimkejeli sana bibi huyo mtukufu na msafara wake. Hapo Bibi Zainab alitoa hotuba ambayo ilipelekea kusambaratika njama za Obaidullah ambaye alikuwa na nia chafu ya kupotosha ukweli wa mapambano ya Imam Husain AS. Liwali huyo wa Kufa alidhalilika kutokana na hotuba nzito iliyotolewa na Bibi Zainab SA na hivyo akaona kuwepo mateka hao hapo Kufa ni tishio kwake. Kwa hivyo aliamuru wapelekwe haraka iwezekanavyo katika makao makuu ya Khalifa wa zama hizo huko Sham. Wakati msafara wa mateka wa Karbala ulipowasili Sham, wakaazi wa mji huo nao walikuwa na furaha tele kutokana na propaganda sumu za Yazid ambazo ziliwafanya watu hao wawe na mtazamo potofu kuhusu Bibi Zainab SA na wenzake. Yazid alikuwa ameeneza propaganda kuwa eti Bibi Zainab SA alitoka chini ya amri ya mtawala wa zama zake, hivyo watu wa Shama nao walisema ni haki yao watukufu hao kuwa mateka.

Yazid aliitisha kikao cha maafisa wa utawala na kijeshi ambapo katika kikao hicho cha watu waliokuwa wamejaa ghururi, kiburi na majivuno, Yazid alichukua kijiti na kuanza kuupiga mdomo na meno ya Imam Husain AS huku akisema: 'Natamani wakuu wa kabila langu ambao waliuawa katika vita vya Badr wangekuwepo hapa ili waone namna sisi tulivyolipiza kisasi cha vita vya Badr kwa kuwaua wakuu wa Bani Hashim... Bani Hashim wamewahadaa watu ili kupata utawala kwani hakuna malaika aliyetumwa wala Wahyi ulioshuka..." Yazid alisema hayo akiwa amelewa chakari na kwa maneno yake hayo ya jeuri, alibainisha wazi kwama hakuna na imani na mafundisho ya Uislamu na wale Mtume Muhammad na wala dini ya Mwenyezi Mungu. Alisema, hakuna malaika aliyetumwa, yaani alikanusha kuwa Malaika Jibril AS alikuwa akija kwa Mtume na alisema pia kuwa hakuna wahyi ulioshushwa ikiwa ni kukanusha kuwa Qur'ani tukufu ni kitabu cha Mwenyezi Mungu. 

Hapo Bibi Zainab SA alitoa hotuba kali iliyofichua mengi na kuwafanya hadhirina wamkumbuke Imam Ali AS. Katika sehemu moja ya hotuba yake hiyo Bibi Zainab SA alisema: "Ni ukweli uliojaa yakini maneno ya Mwenyezi Mungu aliposema: Kisha ulikuwa mwisho wa waliofanya ubaya ni kuzikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu, na wakawa wanazifanyia maskhara." (Surat Ar-Rum aya ya 10.) Bibi Zainab AS akaendelea kumkhutubu Yazid bin Muawiya akimwambia: Ewe wana wa Muawiya! Ingawa hali ya mambo imetulazimisha tuzungumze katika hali hii mbele ya yako hivi sasa, lakini mimi nakuona ni mtu duni wa kuzungumza naye kwani wewe ni mtu muovu mwenye madhambi mengi na utapata adhabu ambazo hatuwezi kuzihesabu. Lakini nifanyeje? Mimi nina majonzi kutokana na vifo vya vipenzi vyangu.. .Ewe Yazid! Fanya uwezalo lakini naapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba huwezi kamwe kuzima utajo wetu na kupotosha Wahyi wetu ulioshuka kwetu....

Umati wa Waislamu wanaoshiki katika kumbukumbu ya Arubaini ya Imam Husain AS huko Karbala, Iraq kila mwaka

 

Hotuba ya Bibi Zainab ilijaa hamasa na ushujaa kiasi cha kumdhalilisha kabisa Yazid ambaye kutokana na kukosa la kusema aliona njia pekee ya kujivua na jinai hiyo, ni kudai kuwa yeye siye aliyemuuma Imam Husain AS bali ni Ibnu Ziad, liwali wa mji wa Kufa. Hotuba ya Bibi Zainab AS mbele ya baraza la wakuu wa utawala wa Yazid iliyoifuatiwa na hotuba kali na nzito ya Imam Sajjad AS zilibadilisha hali ya mambo mjini Dimishq kwani haki iliwabainikia wananchi wa Sham kwa namna ambavyo haikutarajiwa.

Uwepo wa watukufu hao huko Sham nao ulikuwa ni tishio kwa nguzo za mtawala dhalimu Yazid mwana wa Muawiya, hivyo alilazimika kuwarejesha Madina mateka hao kutoka kizazi cha Bwana Mtume Muhammad SAW. Kiujumla ni kwamba hivi ndivyo Bibi Zainab alivyotekeleza majukumu yake katika kufikisha ujumbe wa harakati ya Imam Husain AS na hatimaye aliwasili Karbala kwa ushindi na heshima katika siku ya Arubaini tangu alipouawa shahidi Imam Husain AS mwezi 10 Muharram maarufu kwa jina la Siku ya Ashura.

Sahaba Jabir aliupokea msafara wa mateka wa Karbala uliokuwa unaotokea Sham akiwa anatembea miguu chini kwa kilio na huzuni kubwa. Alipomkaribia tu Imam Sajjad AS, Imam alimuuliza, wewe ndiye Jabir? Akajibu, naam ndiye mimi ewe mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu. Hapo hapo alimkumbatia Imam na kulia vibaya sana kutokana na mauaji ya kikatili ya Imam Husain AS. Imam Sajjad akamwambia Sahaba Jabir kwamba: 

Ewe Jabir! Naapa kwa Mwenyezi Mungu, ni katika eneo hili ndipo watu wetu walipouawa shahidi, vijana wetu walipotekwa nyara, wanawake wetu walipofanywa mateka na mahema yetu walipoyachoma moto. Baada ya hapo Imam Sajjad alimuonesha Jabir sehemu moja moja waliyouawa mashahidi wanamapambano wa Karbala. Katika sehemu moja alimwambia: Hapa ndipo lilipo kaburi la Ali Akbar na hili hapa ndilo kaburi la Qassim. Hapa ndipo lilipo kaburi la baba yangu Husain na pale ndipo lilipo kaburi la ami yangu Abbas.

 

Baada ya kuonana na Jabir na Atiyyah, Imam Sajjad AS aliwaamrisha wanaume waliokuwepo hapo wasogee mbali kidogo na sehemu lilipo kaburi takatifu la Imam Husain AS. Baada ya kutendeka hilo, Bibi Zainab SA aliyekuwa amechoka kwa kiu, safari, njaa na majonzi, alikwenda kwenye kaburi la Imam Husain AS na kusema kwa sauti kubwa ya majonzi: Ewe kipenzi cha moyo wa Mtume wa Mwenyezi mungu! Ewe mwana wa Makka na Mina na ewe mwana wa Zahra na Aliyul Murtadha! Aah! Kaka yangu! Nimerejea kwako baada ya siku Arubaini! Kaka yangu! Mchana wa siku ya Ashura nilipokuja sehemu ulipouawa, mwili wako ulikuwa umejaa mishare, majambia na panga kiasi kwamba nilishindwa kukutambua! Lakini hivi sasa amka uione hali yangu baada ya siku Arubaini za kuuawa kwako! Bila ya shaka wewe nawe hutonitambua! Nywele zangu zimepiga weupe na nyonga yangu imepinda... Bila ya shaka ukiniona huwezi kunitambua!

Imam Sajjad AS alipoona hali hiyo ya shangazi yake, alihofia asije akampoteza. Alimwendea na kumwambia, sahangazi yangu kipenzi, subiri! Vumilia shangazi yangu! Bibi Zainab AS alisema: Ewe Ali, nuru ya macho yangu, niache hapa hapa Karbala nibakie na kaka yangu Husain. Imam Sajjad AS alimjibu kwa kumwambia: Shangazi yangu kipenzi! Vumilia, subiri, kwani wewe ndiye mlezi wa mayatima, usipowalea wewe alitekeleze nani juhukumu hili?  Hapo msafara wote uliripuka kwa vilio, simanzi na maombolezo yaliyohinikiza eneo lote na kila mmoja akiomboleza kwa lugha na maneno yake. 

Amma kumbukumbu za Arubaini ya Imam Husain AS katika karne zilizopita zilikuwa zinafanyika hivi hivi kwa majonzi makubwa. Maashiki wa Bwana Mtume na Imam Husain AS wanatembea wiki kadhaa kwa miguu na kuvumilia nyakati za mchana na usiku zilizojaa baridi kali jangwani na hayo yote ni kwa ajili ya mapenzi yao kwa Bwana Mtume na kwa Bwana wa Mashahidi, Imam Husain AS. Mapenzi na mahaba haya ni ya kumzuru Bwana wa Vijana wa Peponi ambaye Mtume Mtume SAW alimtaja kuwa ni 'merikebu ambayo itauokoa umma na ni mwanga wa kuwaongoza wanaadamu milele.'

Kwa hakika mjumuiko wa mamilioni ya Waislamu katika Siku ya Arubaini ya Imam Husain AS ni fursa bora kwa wapenda haki duniani ya kutangaza msimamo wao usiotetereka wa kuangamiza dhulma, upotofu na batili na kuamrisha mema ili kuhakikisha kuwa Uislamu halisi ndio unaobakia milele hata kama maadui watachukia. Msisimuko huu wa mapenzi makubwa kwa Imam Husain AS ni ishara ya wazi kuwa njama za mashetani wa zama hizi nazo zitashindwa tu, na Uislamu halisi utaenea kote duniani.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.