Oct 14, 2019 14:20 UTC
  • Upeo wa kimataifa wa Arubaini ya Imam Hussein (as) + Video

Arubaini ya Imam Hussein (as) imekuwa ni ya kimataifa na itaendelea kupanuka zaidi katika upeo huo. Hii ni damu ya Hussein bin Ali (as) ambayo licha ya kupita miaka 1400, ingali inachemka na kuendelea kuwa mpya na hai zaidi siku baada ya nyingine. Huu ndio ujumbe ule ule wa Siku ya Ashura uliopazwa kupitia koo za Aba Abdillah al-Hussein (as) na Bibi Zainab (sa) katika kipindi kigumu zaidi cha upweke wao. Pamoja na hayo, hii leo ujumbe huo umeenea na kufika katika kila pembe ya dunia.

Arubaini ni 'Siku za Mwenyezi Mungu.' Arubaini ya Imam Hussein (as) ni wakati ambao unaweza kuwa ni mwanzo wa kujua ukweli wa mambo, na Hussein (as) pia ni Imam ambaye kushikamana naye kunaweza kuufanya moyo wa mwanadamu kupanda safina ya wokovu na kufika kwenye ufuo salama na wenye utulivu wa kudumu milele. Ni taa ambayo mwangaza wake uliojaa rehema unamuwezesha mwanadamu kuondoa pazia la kiza na kumfanya aweze kutambua hakika ya mambo ya ulimwengu. Hii ndio ndio maana Mtume Mtukufu  (saw) akasema kuhusiana na utukufu wa Imam Hussein: 'Hussein ni taa ya uongofu na safina ya wokovu.' Hii ni kwa sababu Imam Hussein (as) huzivutia nyoyo na bila shaka kila mtu anayezingatia na kutii wito wa maumbile yake, humkubali Imam (as) bila kusita.
 
Hussein ni taa ya uongofu na safina ya wokovu

Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 5 ya Surat Ibrahim: Na tulimtuma Musa pamoja na miujiza yetu, tukamwambia: Watoe watu wako kwenye giza uwapeleke kwenye mwangaza. Na uwakumbushe Siku za Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anamuamrisha Nabii Musa (as) awakumbushe watu wake kuhusiana na Siku za Mwenyezi Mungu na awatoe kwenye giza na kuwapeleka kwenye nuru. Anatakiwa pia kuwakumbusha kuhusiana na neema hiyo kubwa ya Mwenyezi Mngu na kuwafanya wapate ibra kutokana na "Siku za Mwenyezi Mungu' na hasa kuhusiana na watu ambao wamejitolea na kufanya subira kubwa maishani mwao na kumshukuru Mola wao katika kila hali. Ni kutokana na ukweli huo ndipo Aya ya 7 ya Sura hiyo hiyo ya Ibrahim ikasema: 'Mkishukuru nitakuzidishieni; na mkikufuru, basi adhabu yangu ni kali.' Ni kutokana na hali hiyo ndipo dada mtukufu na mwenye subira kubwa wa Imam Hussein (as), yaani Bibi Zainab (sa), baada ya kupitia masaibu, machungu, upweke na mateso mengi makubwa kutoka kwa askari wa dhalimu Yazid akasema: 'Sikuona ila mazuri.' Ni wazi kuwa kama mmoja wetu angekabiliwa na hali ngumu na ya kutisha kama hiyo asingeweza kuimudu. Hii ndio maana halisi ya subira iliyodhihirishwa kivitendo na Bibi Zainab (sa), mwanamke mwenye subira kubwa zaidi duniani, kama linavyothibitisha hilo jina lake mwenyewe. Zainab (sa) alikuwa mfano wa baba ambaye alichukua nafasi ya Imam Ali (as) katika kumtetea kwa nguvu zake zote, ndugu yake Imam Hussein (as) pamoja na malengo yake matukufu.

Sikuona ila mazuri

Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran anasema kwamba matembezi ya watu zaidi ya milioni 25 ambao kila mwaka hutembea kwa miguu zaidi ya kilomita 80 kutoka mji mtakatifu wa Najaf kuelekea mji mwingine mtakatifu wa Karbala kwa ajili ya kutetea na kuhuisha uhuru na kujibari na dhulma na madhalimu, ni tukio la miujiza ya Mwenyezi Mungu. Anasema: Njia hii ni ya mahaba, lakini sio mahaba ya kiuwendawazimu bali ni mahaba yanayoandamana na mwamko na umakini. Ni mfano wa mahaba yaliyopo kati ya waja wema wa Mwenyezi Mungu na Muumba wao.' Ayatullah Khamenei anaendelea kusema kuwa fikra ya Ahlu Bait wa Mtume Mtukufu (saw) na Mashia ni mfungamanao wa akili na hisia na vilevile imani na mahaba na kuamini kwamba jambo hili halipatikani katika medhehebu nyingine za Kiislamu. Nam, ukubwa na utukufu unaodhihirishwa katika harakati hii kubwa ya wanadamu ni jambo ambalo si rahisi kubainishwa kwa maneno. Hii ni njia ya watu walio na mapenzi makubwa kwa Mola wao ambao wameyafumbia macho anasa na mapambo yote ya dunia na kuyafungulia macho ya nyoyo zao mapambo ya kimaanawi na kiroho.

Katika zama hizi ambapo maadui wanachafua jina la Uislamu, kuchochea hisia za walimwengu na kuwatia hofu kuhusiana na dini hii tukufu kwa lengo la kuaibisha Uislamu na Waislamu, nafsi ya kusikia kwamba kuna watu zaidi ya milioni 25, Waislamu na wasiokuwa Waislamu na Mashia kwa Masuni wakiwa wamekusanyika wote kwa njia ya kuvutia na ya kudhihirisha udugu wao huko Karbala na katika Haram tukufu ya Imam Hussein (as), ni jambo linaloshangaza na kuwavutia sana walimwengu. Jambo hilo huwafanya wajiulize swali hili kwamba, je, huyu Hussein (as) ambaye amewakusanya mamilioni ya walimwengu kando yake ni nani?

Swali hili linaweza kujibiwa vizuri na kwa uwazi zaidi kupitia umati huu mkubwa na wenye mapenzi makubwa kwa Imam Hussein (as) ambao unapiga nara inayosema: 'Ni kumpenda Hussein ndiko kunatuunganisha.' Ni mtukufu huyu (as) ndiye amewakusanya katika umoja huu wa kuvutia, mamilio ya watu, kutoka nchi za Kiislamu na zisizo za Kiislamu kwa ajili ya kulitembelea kaburi lake lililojaa nuru na hivyo kutekeleza kivitendo  amri ya Mwenyezi Mungu iliyobainbishwa wazi katika Aya ya 103 ya Surat Aal Imran inayowataka watu wote kushikamana kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu kwa kusema: Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu: vile mlivyo kuwa nyinyi kwa nyinyi maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu.

Kwa kitendo hiki mamilioni haya ya watu hujikumbusha neema hii muhimu ya Mwenyezi Mungu ambayo ni uwepo wa Imam Hussein (as) na kufanikiwa kumjua, na kutambua kuwa yeye ndiye muhimili wa umoja na mshikamano kwa wale wote wanaopigania thamani za utu na kutetea haki. Wao hueneza ulimwenguni mantiki na fikra tukufu ya mapambano dhidi ya dhulma, upotofu na uistikbari ambayo ndiyo ile ile fikra ya Imam Hussein (as).

Ni kumpenda Hussein ndiko kunatuunganisha.

Huku akiwashukuru wale wote wanaojitolea na kuandaa kwa mapenzi, huruma na ukarimu mkubwa maukib au vituo vya kutoa huduma na misaada tofauti kwa wanaoshiriki matembezi ya Arubaini, Ayatullah Khamenei, Kiongozi Maudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: 'Arubaini ya Imam Hussein (as) imekuwa ni ya kimataifa na itaendelea kupanuka zaidi katika upeo huo. Hii ni damu ya Hussein bin Ali (as) ambayo licha ya kupita miaka 1400, ingali inachemka na kuendelea kuwa mpya na hai zaidi siku baada ya nyingine. Huu ndio ujumbe ule ule wa Siku ya Ashura uliopazwa kupitia koo za Aba Abdillah al-Hussein (as) na Bibi Zainab (sa) katika kipindi kigumu zaidi cha upweke wao. Pamoja na hayo, hii leo ujumbe huo umeenea na kufika katika kila pembe ya dunia.'

Imam Hussein (as) si shakhsia wa sehemu, madhehebu wala kundi fulani bali ni mfano na ruwaza kwa wanadamu wote. Hata kama sehemu kubwa ya wanaozuru Haram takatifu ya mtukufu huyo (as) ni wananchi wa Iraq lakini Waislamu wengi pia hushiriki katika matembezi adhimu ya kijamii ya kimaanawi ya Arubaini na ziara ya haram hiyo kutoka nchi tofauti za dunia na hasa Iran, Pakistan, India, Afghanistan, Azerbaijan, Uturuki na nchi nyingine za Kiarabu na Kiafrika. Vilevile kushiriki katika matembezi hayo Waislamu kutoka nchi za Ulaya na Marekani na kuwaona wakiwa katika hali maalumu ya kimaanawi ni jambo linalovutia, kupendeza na kuwa na taathira kubwa. Nukta nyingine inayovutia katika matembezi hayo ni kuona idadi kubwa ya Waislamu wa Kisuni na hata Wakristo wakishiriki katika matembezi hayo, jambo linalobainisha wazi kwamba malengo ya Imam Hussein (as) yaliwajumuisha watu wote. Kuhusu suala hilo, Ayatullah Khamenei anasema: 'Makumi ya nchi tofauti hushiriki katika matembezi ya Arubainina na watu wa Iraq kuwa wenyeji wa wageni hao. Hivyo tufanye juhudi za kuimarisha zaidi mshikamano katika matembezi hayo kati ya ndugu Waislamu, baina ya Wairaki na wasiokuwa Wairaki, Mashia na Masuni, Waarabu na Wafursi na vile vile Waturuki na Wakurdi. Mshikamano huu huleta saada na ni ishara ya rehema ya Mwenyezi Mungu.

Nukta muhimu hapa ni kwamba, hata wale maadui walio na malengo maovu ya kutaka kuuangamiza Uislamu na kueneza propaganda chafu dhidi ya Waislamu, wanakiri wazi kwamba matembezi adhimu ya Arubaini ndio mkusanyiko mkubwa zaidi wa wanadamu duniani. Nam, hakika ya ucha-Mungu na mapenzi kwa Imam Hussein (as) katika matembezi ya Arubaini hupata maana yake halisi kwa kutilia maanani kwamba mkusanyiko wa watu milioni 25 huwa ni mkusanyiko wa ndugu ambao wote wanafuatilia kuimarisha mshikamano wao kupitia matembezi hayo ya kimaanawi na kwa madhumuni ya kutoa shukrani zao kwa kujitolea Imam Hussein (as) katika njia ya kuulinda Uislamu dhidi ya hatari iliyokuwa ikiukabili katika zama zake na kutangaza uungaji mkono wao kwa malengo yake matukufu. Waislamu wanaoshiriki matembezi hayo hufaya hayo yote ili huenda ikiwa ni sehem ndogo tu ya pozo la moyo uliojaa machungu na huzuni wa Bibi Fatwimah (as), kutokana na mwanaye, ambaye pia ni mjukuu mtukufu wa Bwana Mtume (saw) kuchinjwa kinyama na maadui wa Uislamu.
Matembezi ya mamilioni ya Arubaini katika upeo wa umoja na mshikamano

Kisa cha Karbalaa na moto ambao umekuwa ukiwaka kwa karne nyingi katika nyoyo za wanadamu bila kujali dini na rangi zao, kinathibitisha wazi kuwa mapambano ya Ashura na hamasa ya Karbala ina uhusiano mkubwa na wa karibu na muundo mzima wa jamaii ya mwanadamu na yote hayo yanatokana na msisimko wa uhuru na ucha-Mungu wa wafuasi wa Imam Hussein (as) katika mapambano hayo. Ukubwa wa mapambano hayo ni wa hali ya juu kiasi kwamba hautambui mipaka ya mataifa, makabila wala tofauti za rangi. Watu wote bila kujali rangi na itikadi zao za kidini, humtambua Imam Hussein (as) kama nembo ya kimataifa ya mapambano dhidi ya dhulma na uonevu. Bila shaka kukipenda kizazi cha Mtume Mtukufu (saw) na hasa, mjukuu wake Mtukufu, Imam Hussein (as) kuko ndani ya damu zetu tokea utotoni na ni wazi kuwa mapenzi ya Imam Hussein (as) yamejaa katika nafsi ya kila mtu aliye na maumbile safi na anayetafuta ukweli na haki.

Tags