Bibi Fatimatuz Zahra SA, Fakhari ya uumbaji
Amani iwe juu ya Bibi mpwekeshaji. Amani iwe juu ya kumbukumbu ya Mtume Muhammad SAW, Bibi Fatimatuz Zahra (SA). Na kongole na pongezi ziwafikie wanawake na wanaume wote, wapenzi wa Faatimah.
Tumo katika maadhimisho ya siku ya kukumbuka kuzaliwa Bibi Faatimatuz Zahra, SA. Kabla ya jambo lolote tunatumia fursa hii kutoa mkono wa baraka na fanaka kwa Waislamu wote na kwa wapenda haki wote kwa mnasaba wa siku hii adhimu.
Ijapokuwa viumbe wote ni uthibitisho wa uwepo wa Muumba na wote Mwenyezi Mungu Mtukuf u anawaumba kwa mapenzi Yake, lakini viko baadhi ya viumbe huwa fakhari ya uumbaji wa Allah kutokana na Mwenyezi Mungu kuwapa zingatio maalumu. Ndio maana katika historia kunashuhudiwa viumbe watukufu kama Bibi Fatimatuz Zahra (SA) ambaye ni moja ya miujiza ya Mwenyezi Mungu kwa walimwengu ili kuwaonesha walimwengu dalili zilizo wazi za uwepo wa Mwenyezi Mungu Mmoja asiye na mshirika na anayestahiki kuabudiwa na
viumbe wote. Ni kwa sababu hiyo ndio maana Bwana Mtume Muhammad SAW akanukuliwa akisema: "Faatimah ni kipande cha mwili wangu, ni nuru ya jicho langu, ni tunda la moyo wangu, ni moyo na ni roho yangu. Yeye ni hurulaini katika sura ya mwanaadamu... kila anaposimama kufanya ibada, Mwenyezi Mungu anawaambia malaika Wake: Mwangalieni mja wangu aliye bora - Faatimah - amesimama mbele Yangu na dhati yake yote inatetemeka kutokana na unyenyekevu Wake mkubwa Kwangu na amesimama kuniabudu kwa mayo wake wote."

Mayo wa Bibi Khadija SA ulishughulishwa na kitu kipya. Kwa amri ya Allah fuko lake la uzazi lilibeba mimba ya kitoto kisafi na kitukuf u, na kwa amri ya Mwenyezi Mungu alikilea kitoto hicho kwa mapenzi yake yote. Wakati wa utotoni mwake, kitoto hicho kilikuwa ni mwenza na rafiki bora kabisa wa Bibi Khadija. Katika kila pumzi yake, mayo wa Khadija ulitaja jina la kitoto hicho, na ulishughulishwa na jukumu la Bibi huyo hnyo Mtukuf u mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu na mbele ya jukumu zito alilopewa mumewe, Bwana Mtume Muhammad SAW na Mola Mlezi wake. Daima mayo wa Bibi Khadija alikuwa akifikiri je kitoto hicho kidogo kingeliweza kuupoza na kuuliwaza mayo uliokabiliwa na mashaka mengi wa Bwana Mtume, na je kitoto hicho kisingelizidiwa nguvu na jukumu la kumsaidia na kuwa bega kwa bega na baba yake mbele ya maadui?
Kipindi cha ujauzito wake, kilikuwa kipindi kigumu kwa Bibi Khadija, Himila hiyo ilimletea uzito mkubwa. Ghafla akagundua kuwa yeye ndiye aliyekuwa chaguo la Mwenyezi Mungu la kuzaa Bibi Mtukufu ambaye ndiye atakayekuja kuwa chimbuko la kizazi bora kabisa duniani. Hicho kilikuwa kipindi kigumu mno pia kwa Bwana Mtume, kilikuwa ni kipindi cha kilele cha uadui wa washirikina wa Makkah. Bibi Khadija alikuwa muungaji mkono mkubwa wa Bwana Mtume, hivyo hatima yake ikawa na yeye ni kufanyiwa uadui. wa Kupindukia na washirikina wa Makkah. Alikumbwa na upweke mithili ya Hajar, Asia na Maryam. Mabibi hao watukufu nao walikabiliwa na uadui na uhasama wakati waliposhikamana na dini ya Mwenyezi Mungu. Bibi Khadija alihisi uwepo wa mabibi hao watukufu pembeni mwake. Ilikuwa ni muujiza. Bibi Khadija akamzaa binti huyo mtukufu katika kipindi ambacho sauti haikuwa ya yeyote ila ya mwanamme. Kipindi ambacho washirikina wa Makkah walikuwa wanaona ni aibu kuwa na mtoto wa kike kiasi kwamba walikuwa wakiwazika hai mabinti zao. Furaha kubwa mno ilitanda moyoni mwa Bibi Khadija baada ya kuona kwamba katika familia ya Muhammad, kumezaliwa kichanga kitukufu ambacho kilikuwa na dalili za wazi kuwa kingelikuwa ni mboni ya jicho la Mtume wa Mwenyezi Mungu. Habari za kuzaliwa kitoto hicho kitukufu liliutuliza na kuupa nguvu mpya moyo wa Bwana Mtume Muhammad SAW, ikawa ni mithili ya aliyepulizwa na upepo mwanana wa peponi katika joto kali la Hijaz. Muhammad alimpenda mno Faatimah. Mwangalio wa kina na wenye mvuto wa kipekee wa Faatimah ulipenya ndani kabisa ya moyo wa Bwana Mtume Muhammad SAW na Bibi Khadijatul Kubra. Bwana Mtume alimpa mapenzi ya kipekee Bibi Faatimah ili kuuthibitishia ulimwengu kuwa mtoto wa kike si tu si sababu ya mtu kuona aibu, bali nafasi na heshima ya mtoto wa kike ni azizi na kubwa mno na Faatimah wake huyo alikuwa ni dhihirisho la mwanaadamu kamili.
Sauti ya pumzi za Faatimah ilikuwa na ujumbe wa matumaini na ilikuwa ni manukato katika maisha ya maisha ya mapenzi ya mwana kwa baba. Hivi ndivyo alivyokuwa Faatimah tangu utotoni mwake, alikuwa ndani ya nyumba ya Wahyi, nyumba ambayo Malaika wa Wahyi Jibril AS alikuwa akimshukia Bwana Mtume kwa amri ya Mola wake. Bibi Faatimah alinawirishwa na mazingira bora kabisa ya kimaanawi na alivuuka vilele vingi na kumfikisha kwenye ukamilifu wa kibinaadamu, vilele ambavyo hakuna mwanamke mwengine yeyote aliyewahi kuvifikia.

Maisha ya Bibi Faatimah yamejaa ibra na mafundisho mengi. Wataalamu wa elimu nafsi wanaamini kuwa kuweko maana ya maisha ndiyo sababu kuu ya kuendelea maisha ya kuridhisha. Katika maisha ya kila mwanaadamu kuna vitu vya thamani. Utafiti uliofanywa nchini Ufaransa unaonesha kuwa, asilimia 89 ya watu wanaamini kikamilifu kwamba mwanadamu anahitajia kuwa na kitu maalumu ambacho itabidi aishi kwa ajili yake. Asilimia 61ya walioshiriki katika utafiti na uchunguzi huo wa maoni inaonesha kuwa wanaamini kwamba katika maisha yao kuna kitu au mtu maalumu anayewafanya waone umuhimu wa maisha.
Maisha ya Bibi Faatimah yalikuwa na vitu vingi vya thamani vinavyomfanya aishi na ambavyo ni funzo kwa kila mtu. Wengine wanaishi kwa ajili ya mali, wengine kwa ajili ya watoto wengine kwa ajili ya uluwa na ziko sababu nyingine nyingi zinazowafanya watu waishi kwa ajili yake, lakini sababu bora zaidi ya maana ya maisha ni imani kwa Mwenyezi Mungu. Imani ya Mwenyezi Mungu ni ngao madhubuti na bora kabisa inayoyapa maisha maana yake halisi. Maisha ya Bibi Fatimah yalijaa imani kwa Mwenyezi Mungu. Bwana Mtume Muhammad SAW amenukuliwa akisema: "Kwa yakini Mwenyezi Mungu ameujaza imani moyo na viungo vyote vya binti yangu Faatimah."
*******
Kama tulivyosema hivi sasa tumo katika nyakati za kuadhimisha siku aliyozaliwa Binti Mtukufu wa Bwana Mtume Muhammad SAW yaani Bibi Faatimatuz Zahra SA. Hapa tunakunulieni kisa kifupi ili kuhitimishia makala yetu hii.
Salman alikuwa ni mmoja wa masahaba watukufu wa Bwana Mtume. Siku moja alifuatana na Bibi Faatimah hadi nyumbani kwa Bwana Mtume. Walipokuwa njiani kuelekea nyumbani kwa Bwana Mtume: Salman alisema Samahani! Mabinti wa Kaysari na Qasir wanavaa nguo za Hariri lakini binti wa Muhammad, mwanaadamu bora kabisa amevaa abaa lililochakaa. Wakati walipofika nyumbani kwa Bwana Mtume SAW, Bibi Faatimah alimwambia baba yake kwamba: Baba yangu mpenzi! Salman amestaajabishwa na mavazi yangu. Bwana Mtume SAW akamwelekea Salman na kumwambia: Salman! Binti yangu (si binti wa kaisari na wafalme wanaopenda fakhari za kidunia, bali binti yangu) ni miongoni mwa walio mstari wa mbele katika mbio za kwenda kwa Mwenyezi Mungu.
Kwa mara nyingine tunatumia fursa hii kutoa mkono wa baraka na fanaka kwa Waislamu wote na kwa wapenda haki wote kwa mnasaba wa siku hii adhimu. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.