Siku Imam Ridha (as) Alipouliwa Shahidi
Siku aliyouawa shahidi, Imam Ridha alisali kwa khushuu na unyenyekevu mkubwa Swala yake ya asubuhi.
Hali yake ilionyesha kana kwamba alikuwa anajua kuna tukio kubwa linataka kutokea. Nuru ya sura yake ilikuwa kubwa zaidi kuliko siku zote na machoni mwake mlibubujika mapenzi na mawimbi ya imani. Tahamaki, mjumbe wa Maamun akagonga mlango na kusema: “Khalifa Maamun anamwita kwake Abal Hasan yaani Imam Ridha.”
Imam akafuatana na mjumbe huyo. Maamun alinyanyuka mahala pake na kumkaribisha Imam katika sehemu yake maalumu. Wawili hao wakasimama kuangaliana. Imam akahisi moto wa chuki uliotokana na jinsi alivyomwangalia na akaingiwa na wasiwasi. Maamun alikuwa amekata tamaa kwamba licha ya kufanya njama nyingi, lakini ameshindwa kuwazuia watu wasimpende Imam Ridha na kumfuata kwa kila jambo. Alikuwa akijuwa vyema kwamba Imam Ridha hakuwa mtu wa kuvumilia dhulma na ukandamizaji na kwamba licha ya kuwa Maamun alikuwa Khalifa, lakini hakuwa na nafasi kama ya Imam Ridha ndani ya nyoyo za Waislamu. Sasa akawa anajisemea mwenyewe chini kwa chini: “Naam, njia bora kabisa ni kumuondoa katika uso wa dunia Abal Hasan.”
Maamun alipiga hatua chache mbele na bila kuangalia akachukua vishada kadhaa vya zabibu kutoka kwenye chombo kikubwa na kubwakia tembe zake. Baadaye akaenda mbele ya Imam akambusu kwenye kipaji cha uso na kumkaribisha ale zabibu akimwambia: “Yaa Ibna Rasulillah! Ewe mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu! Sijawahi kuona zabibu tamu, safi na za kuvutia kushinda hizi.”
Imam akamjibu kwa maneno yasiyotetereka akisema: “Lakini zabibu za peponi ni safi na za kuvutia zaidi.”
Maamun akamwambia: “Karibu ule zazibu hizi tamu.”
Imam alikataa. Hata hivyo Maamun akashikilia na kumlazimisha ale zabibu hizo zilizokuwa zimetiwa sumu kwa hali yoyote ile. Imam akatoa tabasamu chungu. Tahamaki rangi ya sura yake ilibadilika na hali yake ikawa mbaya. Kishada cha zabibu kikamwanguka mkononi na sasa hali ikazidi kuwa mbaya, akaanguka chini taabani.
Abu al-Salt al-Hirawi, mmoja wa wafuasi wa karibu wa Imam Ridha alishtuka mno alipoona hali hiyo. Alikuwa amejaa furaha kwa kuwa karibu na mtukufu huyo na alikuwa akinufaika kwa kila sekunde na nuru ya mjukuu huyo wa Bwana Mtume. Alikuwa amezama kwenye mawazo akikumbuka miongozo ya Imam Ridha AS aliposema: “Imam na kiongozi ni wawakilishi waaminifu duniani, ni hujja zake kwa waja Wake… Ni walinganiaji wa njia ya Allah na ni walinzi wa mipaka Yake Allah. Imam hutakaswa kutokana na aibu na madhambi. Hupambika kwa elimu na anasifika kwa ucha Mungu. Imam ni chimbuko la istikama ya kidini, heshima na fakhari kwa Waislamu…”
Abu al-Salt alikuwa amezama kwenye mawazo hayo ghafla akamuona Imam Ridha akiwa katika hali hiyo ya kusikitisha. Hapo alifahamu kuwa Maamun ametekeleza hila yake ya mwisho na wakati ulikuwa umepita, kwani sumu ilikuwa imeshaenea mwilini. Muda haukupita Imam Ridha AS akauawa shahidi. Siku hiyo ilikuwa mwishoni mwa Mfunguo Tano Safar mwaka 203 Hijria.
Maadili bora, elimu ya hali ya juu, imani thabiti na kubwa kwa Mwenyezi Mungu na kuwajali watu ni miongoni mwa sifa maalumu zilizompambanua Imam Ridha AS na watu wengine. Alikuwa na hima kubwa ya kuzingatia masuala ya kimaanawi na kujishughulisha na ibada. Daima alikuwa akishughulikia masuala ya Waislamu na akifanya juhudi kubwa kutatua matatizo ya waliotingwa. Alikuwa akifanya hima ya kuwatembelea wagonjwa na akikaribisha wageni kwa unyenyekevu. Imam Ridha AS alikuwa na elimu kubwa kiasi kwamba wasomi na wataalamu wa Kiislamu wakimiminika kwa wingi kwake. Katika kipindi cha Uimamu wake, Imam Ridha alipata taufiki ya kuwa na wanafunzi wengi na alivirithisha vizazi vya baada yake athari kubwa katika upande wa tafsiri ya Qur’an, hadithi, akhlaki, ahkam na tiba ya Kiislamu. Alikuwa akitoa mafunzo bora kwa Waislamu na sambamba na hayo, alikuwa mwanamapambano katika uwanja wa kisiasa.
Kiujumla ni kuwa tangu mwanzoni mwa nusu ya pili ya karne ya kwanza Hijria, ukhalifa wa nchi za Kiislamu uliingia kwenye mkondo wa usultani uliopenda ufakhari na kujikweza watawala wake. Tangu wakati huo Maimamu kutoka kizazi cha Bwana Mtume walianza mapambano yao ya kisiasa ya kukabiliana na ufisadi na upotofu ndani ya Uislamu. Wakati wa Uimamu wake, Imam Ridha AS naye alitumia kipindi hicho kupambana na dhulma na ukandamizaji. Pamoja na hayo lakini, zama za Uimamu wake zilitofautiana kiasi fulani na zama zilizopita. Imam aliingia katika kipindi kigumu cha mtihani mzito ambao kufanikiwa na kutofanikiwa kwake ndiko kungeliamua mustakbali wa umma wa Kiislamu. Kipindi chake kilikwenda sambamba na ukhalifa ya Maamun kutoka Bani Abbas, khalifa ambaye alikuwa na hila na ujanja mwingi. Siku moja Maamun alimwendea Imam Ridha AS na kumwambia: “Yaa ibna Rasulillah! Ewe mwana wa Mtume! Elimu, ukamilifu, ucha Mungu, takwa na ibada yako kubwa vyote hivyo vinanielea vyema na ninakiri kwamba wewe ndiye unayestahiki zaidi kuongoza dola ya Kiislamu.”
Imam Ridha AS akamjibu: “Naona fakhari kuwa mtumwa wa Mwenyezi Mungu… na ninamuomba Allah anipe cheo kikubwa mbele Yake.”
Maamun akamwambia: “Mimi nimeamua kuacha cheo changu cha ukhalifa wa dola la Kiislamu na ninakukabidhi wewe.” Kwa ufupi maelezo yalikuwa marefu hadi kufikia sehemu ambayo Imam Ridha alimwambia Maamun kuwa “Ninajua lengo lako ni kutaka watu waseme kuwa Aliyyu bin Musa Ridha ameacha ucha Mungu kwa kustahabu dunia, ukhalifa na cheo cha kifalme.” Hatima ya yote ni kuwa Maamun alimlazimisha Imam Ridha kuingia serikalini licha ya Imam kusisitiza kuwa hakufanya hivyo kwa hiari ya nafsi yake.
Uongozi wa Imam Ridha kwa zile sehemu alizoachiwa aongoze ulikuwa wa kiadilifu na wa kuzingatia mafundisho ya Mwenyezi Mungu kiasi kwamba fursa hiyo ndogo aliyopewa na Maamun ilitosha kwa watu wengi kukiri kuwa yenye ndiye aliyestahiki kuwa Imam na kiongozi wa jamii ya Kiislamu.
Mwishowe Maamun alitambua kuwa lengo lake la kutaka watu wamchukie Imam Ridha na wamuhesabu ni mpenda dunia halikutumia. Ndio maana akaamua kutumia mbinu ile ile iliyotumiwa na waliomtangulia na akamuua shahidi Imam wa zama zake. Tunatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote kwa mnasaba wa kukumbuka siku aliyouawa shahidi Imam Ridha AS.