Nov 03, 2022 11:08 UTC
  • Ugaidi wa ISIS unavyohudumia maadui wa taifa la Iran

Jumatano, tarehe 27 Oktoba, damu ya Waislamu waliokuwa wamekwenda kuzuru na kufanya ibada  katika Haram tukufu ya mjukuu wa Mtume wetu Muhammad (saw), Ahmad Ibn Musa (as) huko Shiraz kusini mwa Iran, ilimwagwa katika eneo hilo tukufu ambapo gaidi asiye na moyo wa kibinadamu wa kundi la Daesh aliwamiminia risasi ovyo waumini waliokuwa wakitekelea Swala ya Magharibi na kuua 15 Miongoni mwao.

Waislamu wengine wasiopungua 40 walijeruhiwa katika shambulizi hilo. Baada ya kuingia katika eneo hilo tukufu, gaidi huyo aliwamiminia risasi bila ya huruma Waislamu waliokuwa wakifanya ibada na kuua wanaume, wanawake na watoto wadogo. Gaidi huyo alijeruhiwa na askari usalama, na siku kadhaa baadaye aliaga dunia akiwa hospitalini.

Janga hilo la kusikitisha limeibua simanzi na majonzi makubwa kwa Waislamu hususan taifa azizi la Iran. Miongoni mwa wahanga wa hujuma hiyo ya kigaidi ni watoto wawili waliouliwa shahidi kwa kumiminiwa risasi kandokando ya kaburi la mjukuu wa Mtume (saw), na watoto wengine watatu walijeruhiwa. Hata hivyo kesi iliyozidisha simanzi na majonzi zaidi ni ya mtoto, Artin Sarayedaran mwenye umri wa miaka 5 ambaye baba, mama na kaka yake wameuawa katika hujuma hiyo ya kigaidi. Mtoto Artin mwenyewe aliyekuwa ameandamana na familia yake kwenye eneo hilo la ibada, alijeruhiwa na kulazwa hospitalini. 

 

Hadhrat Ahmad bin Musa ni mwana wa Imam Musa al Kadhim (as) na ndugu yake Imam Ridhaa na Bibi Fatima M'asuma (as) ambao wote ni wajukuu wa Mtume Muhammad (saw). Alisifika kwa ushujaa na uchamungu mkubwa, na kaburi lake lililoko katika mji wa Shiraz, kusini mwa Iran, ni miongoni mwa maziara muhimu yanayotembelewa na Waislamu hususan wapenzi na wafuasi wa Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (saw).

Haram ya Ahmad bin Musa (as), Shiraz-Iran

Haram na makaburi ya watoto na wajukuu wa Mtume wetu (saw) ni maeneo matakatifu kwa Waislamu ambao huzuru maeneo hayo kwa ajili ya kutawasali kuomba shafa'a yao kwa ajili ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu SW na kuonesha mapenzi kwa Mtume wake na Ahlibaiti zake watoharifu. Hata hivyo kundi la Daesh (ISIS), ambalo linafuata imani na itikadi potofu za Uwahabi, sio tu kwamba linapinga kutawasali na kufanya maombezi na shafaa kwa Mtume Muhammad (saw) na Ahlibaiti wake, bali pia linawalazimisha Waislamu wengine kufuata fikra, maoni na itikadi zake la sivyo hukumu yao ni kifo na kuuawa. Hadi sasa, wanachama wa kundi hilo wameshambulia, kuharibu au kuvunja kabisa haram tukufu za idadi kadhaa ya wajukuu wa Mtume Muhammad (saw) na maswahaba zake na viongozi wa kidini ambao walitoa mchango mkubwa na kusabilia nafsi, mali na maisha yao kwa ajili ya kutetea dini ya Uislamu. Daesh ndilo kundi kubwa zaidi lenye itikadi kali na mienendo ya kikatili linalofuata imani za Kiwahabi na linaendesha shughuli zake katika nchi kadhaa kama vile Syria, Iraq, Afghanistan, Libya na maeneo mengine ya dunia.   

Katika baadhi ya nchi za Waislamu, kuna makundi mengine ya kigaidi na yanayochochea vita ambayo msingi wake wa kifikra ni mitazamo na itikadi potofu za Kiwahabi. Al-Qaida, Boko Haram nchini Nigeria, Sipah-e-Sahaba (Jeshi la Sahaba) nchini Pakistan na al Shabab huko Somalia na nchi nyingine kadhaa za Mashariki mwa Afrika ni miongoni mwa makundi ya kigaidi ambayo yaliundwa kutokana na itikadi za potofu za Kiwahabi. Wakati huo huo, inashuhudiwa kwamba Uwahabi umepungua katika kituo na chanzo chake, yaani huko Saudi Arabia. Kundi la Kiwahabi lililoundwa na "Muhammad bin Abdul Wahhab" kwa mujibu wa fikra potofu za Ibn Taimiyyah ilianza shughuli zake katikati ya karne ya 18 huko Najd, na kufanya jinai za kutisha kama vile mauaji ya wapinzani katika Bara Arabu na Iraq, kuharibu makaburi ya watu wengi wa kizazi cha Mtume Muhammad (saw) kama Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) huko Karbala na maziara ya maimamu waliozikwa kwenye makaburi ya Baqi huko Madina, kubomoa makaburi ya Maswahaba na pia kuharibu athari za kale za Kiislamu huko Makka na Madina. Baada ya kuanzishwa Ufalme wa Saudi Arabia mwaka 1932, Mawahabi waliokuwa wakisaidiwa kwa dola za mafuta za serikali ya Riyadh, walieneza sana itikadi zao potofu katika nchi na maeneo mengine ya Waislamu na kujenga shule nyingi za kidini na misikiti. Matokeo ya harakati hizi ilikuwa kulea na kutayarisha watu wenye fikra potofu za Uwahabi na roho za kikatili, ambao ingawa ni wachache, lakini wanapewa mazingatio kutokana na propaganda nyingi na pia mashambulizi yao ya kigaidi.

Abu Aisha al Umari, gaidi wa Daesh aliyeua Waislamu Shiraz

Ijapokuwa Daesh (ISIS) ni kundi linaloonekana kidhahiri kuwa la kidini lenye itikadi za chuki na misimamo mikali, lakini mara nyingine limekuwa na mielekeko na malengo yanayofanana na ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel. Kwa msingi huo licha ya madai na propaganda nyingi zinazofanywa na Marekani ikidai kupambana na kundi hilo linalowakufurisha Waislamu wengine, lakini kuna ushahidi mwingi unaothibitisha kuwa, Washington inalitumia kundi la Daesh kama wenzo na mkono wake wa siri wa kupeleka mbele na kutimizia mipango na malengo yake. Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, aliwataja waziwazi mtangulizi wake, Barack Obama na aliyekuwa waziri wa mambo ya nje, Hillary Clinton kuwa miongoni mwa waanzilishi wa kundi la Daesh. Vilevile Edward Snowden, mkandarasi wa zamani wa Shirika la Usalama la Taifa la Marekani (NSA), amefichua ukweli huo akisema: "Vyombo vya ujasusi vya Marekani, Uingereza na utawala wa Kizayuni wa Israel vilishiriki katika kuunda ISIS, na vilianzisha kundi hilo katika operesheni iliyopewa jina la Mzinga wa Nyuki, (Beehive) au “Hornet’s Nest”. Mbali na kuua wanajeshi na askari usalama katika nchi za Iraq na Syria, kundi hilo la Daesh pia limeua kwa halaiki maelfu ya raia wasio na hatia katika nchi hizo. Kwa sasa kundi hilo linaendesha shughuli zake nyingi huko Afghanistan. Shughuli na harakati za kijeshi za ISIS ziliongezeka zaidi huko Afghanistan baada ya kuondoa kwa wanajeshi wa Marekani nchini humo. Baadhi ya ripoti za kuaminika zinaonesha kuwa, Marekani ilitayarisha mazingira ya kuhamishwa wanachama wengi wa Daesh kutoka Syria na Iraq na kupelekwa Afghanistan ili kuliimarisha zaidi kundi hilo baada ya kupata kipigo cha mbwa koko huko Iraq na Syria. Huko Afghanistan pia wapiganaji wasio na huruma wa ISIS wameua mamia ya watu wa Afghanistan katika makumi ya operesheni za kigaidi. Miongoni mwa oparesheni zao za hivi karibuni ni shambulio lililofanywa na wanamgambo wa Daesh dhidi ya kituo cha elimu mjini Kabul, ambapo wanafunzi 53, wengi wao wakiwa wasichana, waliuawa na zaidi ya mia moja kujeruhiwa. 

Baadhi ya wanafunzi waliouawa shahidi katika shambulio la Daesh huko Kabul.

Hapana shaka yoyote kwamba, Iran ni miongoni mwa nchi ambazo Marekani na ISIS wana uadui mkubwa na wa muda mrefu dhidi yake. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran mwaka 1979, Waislamu wa Iran walikata mkono wa Marekani hapa nchini na Jamhuri ya Kiislamu ikawa kigezo cha kuigwa na mataifa mengine katika kukabiliana na ubeberu wa Marekani. Tunaweza kusema kuwa, kuna sababu mbili za uadui wa kundi la kigaidi la Daesh dhidi ya Iran na Wairani. Kwanza ni fikra na itikadi potofu na za Kiwahabi za kundi hilo zinazowatambua Waislamu wengine hususan wafuasi wa madhehebu ya Ahlubaiti wa Mtume kuwa ni makafiri kwa sababu tu ya kuheshimu na kuzuru kaburi la Mtume na kizazi chake kitoharifu. Kwa msingi wa itikadi na fikra hizo, kundi hilo lenye misimamo ya kufurutu mipaka linaamini kuwa, amali ya Waislamu ya kuomba shafaa na maombezi ya Mtume na Ahlubaiti zake kwa Mwenyezi Mungu ni shirki, na kwa msingi huo wanapaswa kuuawa. Sababu ya pili ya uadui wa Daesh dhidi ya Waislamu wa Iran na maeneo mengine ya dunia ni mapambano ya kishujaa ya wapiganaji wa Kiirani na mataifa mengine dhidi ya kundi hilo huko Syria na Iraq chini ya uongozi wa Luteni Jenerali Qassem Soleimani. Mapambano hayo ya aina yake ndiyo yaliyopelekea kuanguka na kuporomoka utawa wa kundi hilo katika nchi hizo mbili Novemba mwaka 2017. Miaka miwili baadaye Wamarekani walimuua kigaidi kamanda huyo shujaa aliyekuwa akikabiliana na ugaidi huko Iraq.

Kwa msingi huo janga la mauaji Waislamu wakati wa Swala ya Magharibi katika Haram ya mjukuu wa Mtume (saw) huko Shiraz, japokuwa halina thamani yoyote katika upande wa vipimo vya kijeshi bali ni kilele cha ukatili wa kupindukia, lakini limeifurahisha sana Marekani na vibaraka wake kama Daesh na tawala za kiimla za kanda hii na Magharibi mwa Asia. Jinai hiyo ya kutisha ya kuwalenga na kuwaua watu waliokuwa wakifanya ibada, inaweza kutathminiwa kuwa ni katika fremu ya vikwazo na mashinikizo ya Marekani dhidi ya taifa la Iran. Pamoja na hayo yote uzoefu umethibitisha kwamba, kundi lolote la kigaidi linalothubutu kuvuruga amani na usalama wa Iran litapata jazaa na kipigo shadidi cha mashujaa wa Kiirani.       

Tags