Jan 01, 2023 12:22 UTC
  • Mukhtasari wa Maisha na Historia ya Shahidi Haj Qassem Soleimani

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili ya sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran popote pale yanapokufikieni matangazo haya kutoka hapa mjini Tehran.

Leo nimekuandalieni kipindi maalumu ambacho ni cha kwanza katika mfululizo wa vipindi vitakavyokujieni katika siku hizi za kukumbuka kuwadia mwaka wa tatu tangu alipouawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH). Kuweni nami hadi mwisho wa dakika hizi chache ambapo katika sehemu hii ya kwanza tutazungumzia kwa mukhtasari historia na maisha ya kamanda huyu shujaa wa Kiislamu. Karibuni.

 

Ilikuwa tarehe 3 Januari 2020. Wakati nilipofungua radio, nilisikia sauti ya kisomo cha Qur’ani. Sauti iliponingia vyema masikioni mwangu na kutua moyoni, nilihisi kana kwamba sauti ya Qarii ina kitu maalumu. Kama vile lahani na sauti yake ya kughani ya kupanda na kushuka ya kusoma kwake Qur’ani ilikuwa tofauti kabisa na siku nyingine. Kwa sekunde kadhaa fikra na akili yangu vikashughulishwa na jambo hili. Mara sauti ya Qur’ani ikakatika ghafla na ikaanza kusikika sauti ya mtangazi wa radio. Mtangazaji alisema maneno machache lakini ilikuwa ni habari mbaya na chungu. Kamanda wa kikosi cha Quds Luteni Jenerali Qassem Soleimani aliyekuwa amefanya safari nchini Iraq kwa mwaliko wa serikali ya nchi hiyo, ameuawa shahidi mapema asubuhi ya leo kwa shambulio la kombora la lililofanywa na jeshi la Marekani jirani na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad. Kwa utaratibu huo, maisha ya hapa duniani ya mtu ambaye maisha yake yalijaa jihadi na mapambano kwa ajili ya kutetea na kulinda ardhi za Kiislamu na kueneza jina la dini ya Mwenyezi Mungu yakawa yamefikia tamati. Kama ambavyo jina lake lilikuwa likileta wahaka na woga katika nyoyo za wapenda vita na madhalimu, kwa kiwango hicho hicho jina lake lilikuwa pozo kwa nyoyo zenye majeraha za madhulumina na wahanga wa vita vya ulimwengu wa kufru na ulahidi. Katika siku za mwanzo za kuuawa kwake shahidi, Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema katika kutoa wasifu wake ambapo alimtaja kama ni maktaba. Alisema: Tusimuangalie Haj Qassem Soleimani, shahidi azizi kwa jicho la mtu mmoja, bali tumtazame kwa jicho la maktaba, njia na shule ya kujifunza. Maneno haya ni moja ya wasifu alioutioa Kiongozi Muadhamu khusiana na Luteni Jenerali shahdidi Qassem Soleimani.

 

 

Shahidi Haj Qassem Soleimani alizaliwa katika kijiji cha Ghanat Malek kilichoko katika mkoa wa Kerman ambao kijiografia unapatikana kusini mashariki mwa Iran. Imekuja katika historia ya maisha yake iliyochapishwa baada ya kuuawa kwake shahidi kwa anauni ya Az Chizi Nemetarsidam “Sikuwa nikiogopa kitu” ya kwamba: Mimi nimezaliwa mwaka 1956. Katika msimu wa baridi kali nilikumbwa na maradhi ya surua. Baba na mama yangu walikaa tamaa na kupona maradhi yangu. Walihangaika na kutumia kila dawa za kienyeji, lakini bila mafanikio kwani maradhi yangu hayakupona. Kwa mujibu wa baba yangu, katika hali ambayo theluji ilikuwa imeshuka kwa wingi na kufika hadi magotini, walinifunga kwa mbeleko kwa mama yangu na kuanza safari ya kuelekea katika mji wa Robor kwa ajili ya kutafuta tiba kwa daktari. Ala kulli haal, baada ya muda, kadari ya Allah ikawa kwamba, nibakie hai.

Kijiji alichozaliwa Luteni Jenerali Qassem Soleimani, kama vilivyokuwa akthari ya vijiji vya Iran katika zama za utawala wa kidhalimu wa Kipahlavi; vilikuwa na ukata na umasikini na vilikosa huduma muhimu za maisha. Wakazi wake walikuwa wakipitisha siku za maisha yao kwa taabu, ugumu na mashaka makubwa. Qassem akiwa na umri wa miaka 14 alilazimika kuondoka katika kijiji chao na kwenda mjini. Ameandika katika kumbukumbu zake: Mkopo wa benki aliochukua baba yangu katika Benki ya Ushirika ya Kijiji ulinitia wasiwasi mno kuliko hata mama yangu. Kutokana na hofu ya kutiwa jela baba yangu kutokana na mkopo huo, nililia mara chungu nzima…kwa msingi huo nikakata shauri kwenda mjini na kufanya kadiri ninavyoweza ili kulipa deni la mkopo wa benki wa baba yangu. Baba na mama yangu walipinga uamuzi wangu wa kuondoka, kwani kiumri ndio kwanza nilikuwa nimeingia katika mwaka wa 14, tena nikiwa kijana dhaifu kimwili ambaye mpaka wakati huo sikuwa nimetoka na kusafiri isipokuwa katika mji wa Robor pekee, mji ambao uko jirani na kijiji cha Ghanat Malek.

 

Tajiriba yake ya kwanza ilikuwa ni katika jengo lillilokuwa halijakamilika na hivyo kufanya kazi hapo ya kubeba matofali. Hii ni katika hali ambayo, mikono yake midogo haikuwa na uwezo wa kubeba hata tofali moja. Anasema: nilijishughulisha kwa muda wa siku sita kuanzia mawio mpaka machweo. Hata hivyo umbo langu jembamba na umri wangu mdogo havikuwa na uwezo wa kustahamili kazi kama hii. Damu ilikuwa ikichirizika kutoka katika mikono yangu midogo.

Kipato chake kilikuwa kidogo, hivyo alihitajia muda mwingi mpaka aweze kulipa deni la mkopo wa baba yake. Kwa msingi huo akakata shauri kufanya kazi katika hoteli moja. Sambamba na kazi hiyo alianza kufanya kazi nyingine ya kuuza matunda na hatimaye aliweza kulipa deni la baba yake la mkopo wa benki baada ya miezi mitano. Ni katika kipindi hiki ambapo sasa wasiwasi ukawa umemuondoka na akawa ameweza kujipatia kipato. Akajiandikisha jina katika eneo la michezo ya jadi. Akajiunga na mafunzo ya karate na kufanikiwa kupata mkanda wa kijani. Siku mbili kwa wiki alikuwa akifanya pia mazoezi ya kuinua vyuma na kujenga misuli. Haj Qassem ameandika katika kitabu chake cha “Sikuwa Nikiogopa Kitu”: “Kufanya mazoezi na kujihusisha na michezo kulikuwa na taathira kubwa chanya kwa maadili yangu ya kidini na ilikuwa moja ya sababu muhimu za kunizuia kutumbukia katika mambo machafu ya kimaadili, licha ya kuwa ni kijana. Hususan mazoezi ya michezo ya kijadi ambayo yana misingi ya kimaadili na kidini.”

Ilikuwa mwaka 1974 wakati Haj Qassem Soleimani aliposikia kwa mara ya kwanza neno dhidi ya Shah. Ilikuwa ni pale mtoto wa bosi wake pale alipokuwa akifanya kazi hotelini alipozungumzia vituo na maeneo ya ufisadi ya Shah. Baada ya muda mmoja wa watu katika familia alizungumzia dhulma ya Shah na sio ufisadi wake.

Shahidi Qassem Soleimaani ameandika katika kitabu chake cha “Az Chizi Nemitarsidam” Yaani “Sikuwa Nikiogopa Kitu”: Nikaona Bahram naye anasema maneno ambayo yanashabihiana na Yazdan Panah, lakini sio ufisadi wa Shah bali dhulma aliyokuwa akiifanya Shah dhidi ya raia, anawatia gerezani na kuwaua. Shah haruhusu kusomwe maombolezo ya Imam Hussein (as). Mimi ambaye tangu utoto wangu nilikuwa katika usomaji wa maombolezo ya Imam Hussein (as)… nikiwa nawasubiria wasomaji wa simulizi za maombolezo ya Imam Hussein (as) nilipaza sauti na kusema: “Anafanya ushenzi kwa kuzuia hayo”. Baada ya kusikia maneno yangu haya uso wa Bahram ulibadilika na kuwa kama chokaa na kisha hajui la kufanya alisema: Unataka tukamatwe?

 

Miaka miwili baadaye alianza safari za kwenda na kurejea msikitini. Taratibu akajifunza Qur’ani na tafsiri yake na kama anavyosema mwenyewe akaanza kuwa na mapenzi na taasubi ya kidini katika nafsi yake. Mfalme Shah alikuwa ameanzisha katika makao makuu ya miji vituo vya ufisadi kwa ajili ya kuwapotosha vijana. Hata hivyo katika mkoa wa Kerman yaani mji wa asili wa Qassem Soleimani hakuweza kufanikiwa katika hilo. Mwaka 1976 kulifanyika sherehe katika mji wa Kerman ambapo utawala wa Shah uliwaalika waimbaji na wanenguaji. Haj Qassem akishirikiana na mmoja wa marafiki zake walitoboa na kutia pancha idadi kadhaa ya magari na kwa njia hiyo wakawa wameonyesha upinzani wao kwa hafla hiyo.

Ameandika katika kitabu chake cha “Az Chizi Nemitarsidam” Yaani “Sikuwa Nikiogopa Kitu”, kuhusiana na mapambano yake ya kwanza na polisi kwamba: Ilikuwa mwezi Muharram mwaka 1976, nilikuja hotenili na nikawa naangalia barabarani kupitia dirishani. Upande ule wa barabara ambao ni mkabala wetu kulikuwa ni makao makuu ya Baraza la Miji na Polisi wa Jiji Kerman. Msichana alikuwa akitembea akiwa hana hijabu huku nywele zake ndefu zilikiwa zinaning’inia. Katika zama hizo, mandhari kama hiyo lilikuwa jambo la kawaida kabisa. Katika njia ya kutembea watu kwa miguu askari mmoja wa jiji akawa amemkosea adabu binti huyo. Kitendo hiki kibaya tena katika siku ya Ashura, kilinivuruga mno. Bila ya kujali kitakachotokea, nilikata shauri kukabiliana naye.

Nilitoka kwa kasi ya ajabu na kufika mahali pale na kumtandika mapigo kadhaa ya karate na kumdondosha chini, kiasi kwamba, damu ikawa inamtirikika kutoka puani. Polisi wa usalama barabarani akapinga filimbi. Polisi wawili wa jiji wakakimbilia upande wake. Mimi nikatoka mbio na kukimbilia upande wa hoteli na baada ya kuingia nikajificha chini ya kitanda katika moja ya vyumba vya hoteni. Idadi kubwa ya polisi walijaa katika kila sehemu ya hoteli, wakafanya msako lakini hawakunipata. Kumpiga askari wa jiji kuliniongezea ujasiri na ushujaa.

Katika safari moja aliyoifanya Mash’had Haj Qassem Soleimani alifahamiana na vijana wawili. Kwa mara ya kwanza alisikia jina la Ayatullah Khomeini. Mwaka 1978 hali ya mji wa Kerman ilibadilika kutokana na kusambaa maandamano katika miji ya Qom na Tabriz dhidi ya utawala wa Shah. Kila siku sauti kubwa ya malalamiko na upinzani wa wananchi dhidi ya utawala wa Shah ilikuwa ikisikika na kurindima.

Imekuja katika kitabu cha:  cha “Az Chizi Nemitarsidam” Yaani “Sikuwa Nikiogopa Kitu”, ya kwamba: “Picha ya Khomeini ilikuwa kioo changu cha kila siku. Kwa siku nilikuwa nikiiangalia picha yake mara kadhaa.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo ambacho kimetupia jicho kwa mukhtasari maisha ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani kuanzia kipindi chake cha utoto hadi katika zama za kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu umefikia tamati. Nakushukuruni kwa kuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki maalumu. Hadi tutakapokutana tena katika kipindi kingine kitakachotupia jicho sifa na shakhsia ya Haj Qassem Soleimani.

Wassalaam Alaykum Warahmatullah Wabarakaatuh.

Tags