Jan 06, 2021 04:41 UTC
  • Rais Saleh: Jenerali Suleimani alisimama bega kwa bega na taifa la Iraq

Rais Barham Saleh wa Iraq amesema Shahidi Qassem Suleimani, aliyekuwa Mkuu wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC alisimama bega kwa bega na wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu katika vipindi vyote vya matatizo na misukosuko.

Rais wa Iraq alisema hayo jana Jumanne kwa mnasaba wa kuadhimisha kumbukumbu ya mwaka wa kwanza wa kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Suleimani na Abu Mahdi al Muhandis, aliyekuwa Naibu wa Mkuu wa Harakati ya al Hashdu-Sha'abi pamoja na wanamapambano wenzao wanane.

Amesema nchi hiyo inawakumbukuka na kuwaenzi makamanda hao wawili waliokuwa na shakhsia za kipekee, kutokana na rekodi yao ndefu ya kupambana na ugaidi na udikteta.

Rais huyo wa Iraq amewataja wawili hao kama makamanda wa vita dhidi ya ugaidi katika eneo la Asia Magharibi na mauaji yao yameacha pengo kubwa katika uga huo.

Makamanda wa Muqawama

Kauli ya Rais Barham Salehh inakuja siku mbili baada ya mamilioni ya wananchi wa Iraq kufanya maandamano makubwa katika mji mkuu Baghdad na mikoa mingine ya nchi hiyo, kwa mnasaba wa kukumbuka siku walipouliwa shahidi makamanda hao wa muqawama sanjari na kutangaza upinzani dhidi ya uwepo kijeshi wa Marekani katika ardhi ya nchi hiyo.

Ikumbukwe kuwa, Januari 3, mwaka uliomalizika 2020, Hajj Qassem Suleimani, Abu Mahdi al Muhandis, Naibu wa Mkuu wa Harakati ya al Hashdu-Sha'abi na wanamapambano wenzao wanane waliuliwa kigaidi na kidhulma na wanajeshi magaidi wa Marekani, katika shambulio la anga lililofanywa na magaidi hao karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad nchini Iraq.

Tags