Jul 26, 2023 06:07 UTC
  • Bunge la Ghana lafuta hukumu ya kifo

Bunge la Ghana limepiga kura ya kubatilisha adhabu ya kifo nchini humo, na kuifanya nchi hiyo iwe miongoni mwa mataifa ya Afrika ambayo yamefuta hukumu hiyo katika miaka ya karibuni.

Kwa mujibu wa Idara ya Magereza ya Ghana, adhabu ya mwisho ya kifo kutekelezwa nchini humo ilikuwa mwaka 1993, ingawaje watu 176 kufikia mwaka jana walikuwa katika orodha ya kusubiri kunyongwa baada ya kuhukumiwa kifo.

Ripoti ya Kamati ya Bunge la Ghana imesema muswada huo uliopasishwa Bungeni utafanyia marekebisho Sheria ya Makosa ya Jinai, ambapo sasa hukumu ya kifungo cha maisha jela itatolewa badala ya adhabu ya kifo.

Ingawaje Rais Nana Akufo-Addo wa Ghana anasubiriwa kuidhinisha muswada huo kuwa sheria, lakini hatua hiyo ya Bunge imepongezwa na wanaharakati wa haki za binadamu nchini humo ambao wameitaja kuwa ya kihistoria.

Mwaka jana pia, Equatorial Guinea ilitangaza kufuta adhabu ya kifo, miaka minane baada ya adhabu ya mwisho kutekelezwa nchini humo.

Tags