Msisitizo wa Russia katika kupanua uhusiano wa kina na nchi za Afrika
Vladimir Putin, Rais wa Rusia, amesisitiza udharura wa kupanuliwa uhusiano wa kina na nchi za Kiafrika akisema: Russia itatuma nafaka za bure kwa nchi 6 za Afrika katika miezi michache ijayo.
Putin ambaye alikuwa akihutubia mkutano wa pili wa kilele kati ya nchi hiyo na Afrika huko St. Petersburg, Russia, ametangaza kwamba katika kipindi cha miezi mitatu hadi minne ijayo, nchi hiyo itatuma tani elfu 25,000 hadi 50,000 za nafaka katika nchi za Burkina Faso, Zimbabwe, Mali, Somalia, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Eritrea. Amesema uhusiano wa Russia na nchi za Afrika utapanuliwa zaidi katika nyanja za kilimo, nishati, sayansi na elimu.
Huo ulikuwa mkutano wa pili rasmi wa Russia na nchi za Kiafrika. Mkutano wa kwanza katika mfumo huu ulifanyika mwaka wa 2019 na uliandaliwa na Jiji la Sochi nchini Russia, tukio ambalo lilitambuliwa na baadhi ya wachambuzi kama hatua ya kurejea Warusi barani Afrika.
Mkutano wa mara hii wa Russia na wakuu wa nchi za Afrika umefanyika huku nchi za Magharibi zikijaribu kuwazuia viongozi wa nchi za Afrika kushiriki katika mkutano huo; hata hivyo licha ya juhudi hizo zote, Moscow ilitangaza kuwa nchi 49 kati ya jumla ya nchi 54 za Afrika na wakuu wa serikali au marais 17 wa nchi wameshiriki katika mkutano wa St. Petersburg.
Miongoni mwa mambo muhimu yaliyojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na upelekaji wa nafaka zinazohitajiwa na nchi za Kiafrika, njia za kupanua uhusiano na ushirikiano wa kiuchumi na kisiasa, na kudhamini usalama.
Kutokana na kuendelea vita kati ya Russia na Ukraine, suala la kudhamini nafaka na mbolea za kemikali limekuwa moja ya mambo yanayozitia wasiwasi nchi za Afrika. Katika mazingira hayo, nchi za Magharibi zimefanya jitihada za kuilaumu Russia na kuitaja kuwa ndiyo inayohusika na ongezeko la umaskini na mgogoro wa usalama wa chakula barani Afrika. Hii ni licha ya kwamba, katika miezi ya karibuni maafisa wa Russia walifanya juhudi kubwa za kukidhi mahitaji ya chakula na nafaka zinazohitajiwa na nchi hizo kupitia makubaliano ya nafaka; hata hivyo vizingiti ilivyowekwa na nchi za Magharibi vimekuwa sababu ya kutofika nafaka zinazohitajika katika nchi za Afrika na kuilazimisha Russia kufuta rasmi makubaliano ya usambazaji wa nafaka.
Mafisa wa serikali ya Moscow wamesisitiza mara kwa mara kwamba, nchi za Ulaya zimetumia vibaya makubaliano hayo na kwamba nafaka hizo zimepelekwa kwenye nchi tajiri. Katika muktadha huu, Rais wa Russia amesema: "Hakuna kifungu hata kimoja cha makubaliano ya nafaka kuhusu usafirishaji wa mbolea za kemikali na nafaka za Russia kwenye masoko ya dunia ambacho kimetimizwa, na uuzaji wa nafaka zinazotokea Ukraine katika nchi za ulimwengu wa tatu baada ya kupelekwa katika nchi za Magharibi umeiimarisha Marekani na Ulaya." Kwa msingi huo Moscow imeahidi rasmi kusambaza nafaka zinazohitajiwa na baadhi ya nchi za Afrika moja kwa moja na bila wasita. Putin amesema: "Kwa upande mmoja, nchi za Magharibi zinazuia usambazaji wa nafaka na mbolea za kemikali ya Russia, na kwa upande mwingine, zinatulaumu kinafiki kutokana na mgogoro unaoshuhudiwa sasa katika soko la chakula duniani."
Suala la usalama na kuongeza ushirikiano lilikuwa miongoni mwa masuala yaliyopewa mazingatio katika mkutano wa Russia na Afrika. Moscow pia imeahidi kuzidisha ushirikiano na mabadilishano ya kibiashara na nchi za Afrika na kutumia sarafu nyingine badala ya dola katika miamala ya kibiashara.
Alaa kulli hal, mkutano wa St. Petersburg umefanyika wakati nchi za Magharibi zikiendeleza njama za muda mrefu za kuitenga Russia katika uwanja wa kimataifa. Msemaji wa Ikulu ya Kremlin, Dmitry Peskov, ametangaza kuwa: "Nchi za Magharibi zimetumia mashinikizo yasiyo na kifani dhidi ya nchi za Afrika ili kuzuia mkutano kati ya viongozi wa Russia na Afrika."
Hata hivyo, nchi za Afrika zimekuwa zikitangaza daima kwamba zitadumisha uhusiano wao na hazitaingia katika mchezo huo mchafu. Kwa hakika nchi za Afrika hasa katika miaka ya hivi karibuni, zimejaribu kuwa na nafasi kubwa zaidi katika uga wa kimataifa na katika kuamiliana na nchi mbalimbali, na baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, nchi za bara hilo zitakuwa miongoni mwa wachezaji wakuu katika nyanja za siasa za kimataifa katika siku za usoni.
Andrey Bystritskiy, Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Maendeleo na Usaidizi wa Klabu ya Majadiliano ya Valdai, anasema kuhusiana na suala hili kwamba: "Afrika inaweza kuwa kituo kikuu cha mfumo mpya wa dunia, na hili ni jambo lenye umuhimu. Katika miaka ya hivi karibuni, Afrika imeanza kwa kasi kubwa kuwa na nafasi muhimu kwenye jukwaa la dunia."
Mkutano wa Afika na Russia huko St. Petersburg pia unaweza kutambuliwa kuwa ni katika mwelekeo wa kuongeza ushirikiano wa siku zijazo kati ya Russia na Afrika.