Vyama Tanzania vyataka CHADEMA ifutiwe usajili kwa kuchochea udini na kutusi viongozi
Baadhi ya vyama vya siasa vya upinzani nchini Tanzania vimeitaka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ya nchi hiyo ivifutie usajili vyama vinavyokiuka sheria katika ufanyaji mikutano ya hadhara, kwa kutoa lugha za kuchochea ubaguzi, udini na kejeli dhidi ya viongozi wa serikali.
Wito huo ulitolewa katika mkutano wa dharura wa Baraza la Vyama vya Siasa uliofanyika jana jijini Dar es Salaam kujadili hali ya kisiasa nchini humo kwa kushirikisha viongozi wa kisiasa na kidini.
Miongoni mwa vyama vinavyotuhumiwa kutumia mikutano ya hadhara kutoa lugha zisizo na staha dhidi ya viongozi wa serikali, hususan wakati wanawasilisha hoja zao kuhusu sakata la uwekezaji wa bandari ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambapo Makamo Mwenyekiti wake Bara, Tundu Lissu, ametakiwa kuripoti katika ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), kujibu tuhuma za kutoa lugha chafu dhidi ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Mwenyekiti wa Chama cha Kijamii CCK, David Mwajojele, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) Ali Omar Juma, Katibu Mkuu wa Tanzania Labour Party (TLP) Richard Lymo na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Mvita Mustafa Ali ni miongoni wa waliotoa miito ya kuchukuliwa hatua dhidi ya vyama na wanasiasa wanaotumia lugha chafu majukwaani.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba amewataka wanasiasa kuacha kutoa lugha zinazochochea udini na ubaguzi pamoja na kuhatarisha muungano.
Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe yeye amesema changamoto ya utoaji lugha zisizo na maadili katika mikutano ya hadhara, inachochewa na kitendo cha serikali kuchelewesha marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa.
Chadema haikuhudhuria mkutano huo.../