Aug 04, 2023 12:09 UTC
  • Ujumbe wa ECOWAS waondoka Niger bila kukutana na kiongozi wa mapinduzi

Ujumbe wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) umeondoka katika mji mkuu wa Niger, Niamey bila kukutana na kiongozi wa mapinduzi, Jenerali Abdourahmane Tchiani, huku rais aliyeondolewa madarakani, Mohamed Bazoum akitoa wito kwa jamii ya kimataifa kusaidia kurejesha utawala wa kikatiba.

Ripoti kutoka mji mkuu wa Niger, Niamey, zinasema kwamba ujumbe wa ECOWAS ulikutana na wawakilishi kadhaa wa baraza tawala la kijeshi, lakini haukukutana na kiongozi wa mapinduzi ya Niger, Jenerali Abdourahmane Tchiani, na sababu za suala hilo bado hazijafahamika.

Ujumbe huo ulibakia saa chache mjini Niamey, ambako ulifika Alhamisi jioni, ili kutafuta njia ya kumaliza mgogoro wa Niger, huku mawaziri wa ulinzi wa ECOWAS wakitarajiwa kuhitimisha majadiliano yao leo Ijumaa kuhusu uwezekano wa kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya wafanyamapinduzi.

Baraza la kijeshi linalotawala Niger jana lilitangaza msururu wa maamuzi na mabadiliko kadhaa ili kuimarisha nafasi yake baada ya kupinduliwa kwa Rais Mohamed Bazoum.

Baraza hilo limebadilisha kamanda wa Kikosi cha Gadi ya Taifa na kamanda wa vikosi vya Usalama, baada ya kubadilisha afisa mkuu wa Idara ya Ujasusi ya Jeshi Nje ya Nchi siku moja kabla yake.

Viongozi wa mapinduzi ya Niger pia wametangaza kufuta makubaliano ya ushirikiano wa kijeshi na Ufaransa, na kuahidi kujibu mara moja uingiliaji wowote wa kijeshi wa kigeni. 

Viongozi wa jeshi la Niger

Jumatano iliyopita wiki iliyopita, kikosi cha Gadi ya Rais wa Niger kilimpindua kiongozi wa nchi hiyo, Mohamed Bazuom. Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya nchi hiyo vilisema katika taarifa yao kwa vyombo vya habari kupitia televisheni ya taifa kuwa rais huyo anashikiliwa na maafisa wa kijeshi waliofanya mapinduzi.

Makamanda waliohusika na mapinduzi hayo wanamtuhumu Bazuom kuwa anahusika na hali mbaya ya usalama inayoshuhudiwa nchini Niger.

Tags