Ethiopia yawatuhumu wanamgambo wa Amhara kuwa wanataka kupindua serikali
(last modified Mon, 07 Aug 2023 11:29:48 GMT )
Aug 07, 2023 11:29 UTC
  • Ethiopia yawatuhumu wanamgambo wa Amhara kuwa wanataka kupindua serikali

Afisa wa ngazi ya juu wa Ethiopia amewatuhumu wanamgambo katika eneo la Amhara kuwa wanataka kupindua serikali za jimbo na ya shirikisho kufuatia mapigano ya siku kadhaa mtawalia ambayo yamepelekea mamlaka za uongozi kutangaza hali ya hatari.

Mapigano kati ya wanmgambo wa Fano na jeshi la ulinzi wa taifa la Ethiopia (ENDF) yamekuwa yakiendelea kwa siku kadhaa sasa. Wakazi wa Gondar, mji wa pili kwa ukubwa katika eneo la Amhara wamesema kuwa sauti za mapigano ya silaha nzito yaliyoanza tokea jana Jumapili ziliendelea kusikika hadi leo asubuhi. 

Mgogoro huu unatajwa kuwa mkubwa zaidi wa usalama nchini Ethiopia tangu vilipomalizika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka miwili katika eneo la Tigray linalopakana na Amhara mwezi Novemba mwaka jana.

Temesgen Tiruneh, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa ya Ethiopia ambaye ameteuliwa kusimamia utekelezaji wa hali ya hatari amekiri kuwa wanamgambo wa Amhara hadi sasa wameteka  miji na wilaya kadhaa.  Temesgen ameongeza kuwa kikosi hicho cha ujambazi kinaendesha harakati zake kwa lengo na nia ya kuipindua serikali ya jimbo kwa nguvu na kisha kusonge mbele kuelekea makao makuu ya serikali ya shirikisho. 

Tangazo hilo la hali ya hatari linavipa vyombo vya usalama vya Ethiopia mamlaka ya kutekeleza amri ya kutotoka nje usiku, kuzuia harakati za kuingia na kutoka, kupiga marufuku kubeba silaha na vifaa vyenye ncha kali, kuzuia mikutano na mikusnayiko ya umma na kuwatia nguvuni watu pamoja na kufanya upekuzi bila kuhitaji kibali chochote. Msemaji wa serikali ya Ethiopia Legesse Tulu amesema kuwa vyombo husika tayari vimeanza kuwakamata wale wote wanaohusika na machafuko yanayoendelea. 

Legesse Tulu, Msemaji wa serikali ya Ethiopia