Hatua ya Burkina Faso ya kufuta mikataba ya kikoloni ya Ufaransa
(last modified Thu, 17 Aug 2023 02:29:52 GMT )
Aug 17, 2023 02:29 UTC
  • Hatua ya Burkina Faso ya kufuta mikataba ya kikoloni ya Ufaransa

Rais Ibrahim Traoré wa Burkina Faso ametangaza kuwa nchi yake imefuta mikataba kadhaa iliyokuwa imesaini na serikali ya Ufaransa, ambayo hadi sasa imekuwa na sura ya ukoloni na ya kujali maslahi ya upande mmoja.

Traoré, ambaye alikuwa akihutubia taifa kwa mnasaba wa Siku ya Vijana Duniani, amezungumzia hali ya nchi yake ikiwa moja ya nchi maskini iliyoathiriwa na ukoloni na akasema: "kwa kuwa hadi sasa imesainiwa mikataba mingi ambayo inatubakisha kwenye umasikini, kwa hiyo kufutwa kwa mikataba hii na makampuni ya Ufaransa ilikuwa ni hatua ya kwanza, na sisi tumeianza kazi hii."
 
Rais wa Burkina Faso amesema, vita dhidi ya ubeberu "vitakuwa vigumu na vitachukua muda mrefu, lakini si jambo lisilowezekana"; na akatangaza uamuzi wa kufutwa mkataba na kampuni ya Ufaransa wa utumiaji uwanja wa ndege wa Dancin ulioko katika mji mkuu wa Burkina Faso, Ouagadougou na vilevile kufutwa makubaliano ya ushuru kwa lengo la kuzuia utozaji kodi maradufu; makubaliano ambayo yalitiwa saini kati ya Burkina Faso na Ufaransa mwaka 1965 na akabainisha kuwa: "mkataba huu uliruhusu makampuni, ambao kwa kweli ni Wafaransa, kulipa Ufaransa ushuru wao wa mapato wanayokusanya nchini Burkina Faso.
Rais Ibrahim Traoré wa Burkina Faso

Inavyoonekana, kampeni kali imeanza barani Afrika ya kukabiliana na hatua na mikataba ya ukoloni mamboleo ya nchi za Ulaya na hasa Ufaransa, ambayo imepamba moto zaidi hasa baada ya mapinduzi ya kijeshi ya hivi majuzi nchini Niger na kusitishwa uuzaji wa madini ya urani kwa Ufaransa. Kwa hakika kuwepo Ufaransa kwa muda wa miaka kadhaa katika nchi za Afrika Magharibi katika eneo la Sahel ikiwa ni pamoja na Burkina Faso na Niger, na unyonyaji wa kisiasa na kiuchumi inaozifanyia nchi hizo kwa upande mmoja; na kuendelea kuwaweka kwenye umasikini watu wa nchi hizo kwa upande mwingine, kumepelekea wananchi wengi wa mataifa hayo mawili ya Afrika Magharibi wapinge uwepo wa Ufaransa katika nchi zao. Wakati huo huo, hali ya sasa si shwari kwa Ufaransa, ambayo inategemea migodi ya urani ya Niger kwa ajili ya kudhamini fueli ya urani ya kuendeshea vinu vyake vya nyuklia na wakati huohuo imetiliana saini mikataba mingi na serikali ya Burkina Faso.

Wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa imetangaza kuwa inaunga mkono "kwa dhati" juhudi zozote zinazofanywa na Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi ECOWAS za kumrejesha madarakani rais aliyepinduliwa wa Niger, Mohamed Bazoum. Mkabala na msimamo huo wa Ufaransa, Burkina Faso na Mali zimetangaza kuwa zinauchukulia uingiliaji wowote wa kijeshi wa Ufaransa dhidi ya wafanya mapinduzi nchini Niger kuwa ni sawa na "kutangaza vita" dhidi yao. Msimamo huo wa Burkina Faso na Mali umekabiliwa na mjibizo mkali wa Paris kupitia wizara yake ya mambo ya nje ambayo ilitangaza siku ya Jumapili kuwa imesitisha misaada ya maendeleo na bajeti kwa Burkina Faso.

Upinzani dhidi ya Ufaransa barani Afrika

Katika wiki za hivi karibuni, maafisa waandamizi wa Burkina Faso na Niger wameanzisha mashambulizi makali ya maneno dhidi ya sera na hatua za kikoloni za nchi za Ulaya barani Afrika. Kuhusiana na hilo, sifa na uungaji mkono kwa Traoré umeongezeka hasa baada ya hotuba yake ya ukosoaji dhidi ya nchi za Magharibi aliyoitoa katika mkutano wa pamoja wa Russia na Afrika uliofanyika mjini St. Petersburg. Baada ya mapinduzi ya kijeshi ya Julai 26 katika nchi jirani ya Niger dhidi ya maslahi ya Ufaransa, Rais wa Burkina Faso alikosoa vikali ukoloni na unyonyaji zinaofanyiwa nchi za Kiafrika na madola ya kikoloni hususan Ufaransa na akataka uchukuliwe msimamo wa kukabiliana nao. Traoré alitangaza kuwa, bila ya shaka karibuni hivi Burkina Faso itafikia hatua halisi ya kujitawala na akafafanua kwa kusema: "vita tunayopigana sio kwa ajili ya Burkina Faso tu, bali ni vita kwa ajili ya Afrika nzima." Kwa hiyo, “wakati umefika wa sisi kuamka na kutolazimika tena kuvuka bahari na kufa kwa ajili ya kumtafuta mwokozi wanayejivunia naye watu wengi.”

Ukoloni na Unyonyaji wa madola ya Magharibi katika bara la Afrika

Hata kama katika karne ya 21 zama za ukoloni wa jadi zimefikia tamati na nchi za Magharibi, hasa za Ulaya, zikiwa zinajua fika kwamba, haiwezekani tena kuendeleza uhusiano uliokuwepo wakati wa enzi za ukoloni baina yao na nchi za Kiafrika ambazo ziliwahi kuwa makoloni yao. Kwa sababu hiyo, nchi za kikoloni kama Ufaransa na Uingereza na pia Marekani, zikiwa ndio vinara wa nchi za Magharibi, zinajaribu kuendeleza ukoloni mamboleo kwa sura nyingine na kudumisha satua na ushawishi wao katika nchi za Kiafrika kwa kuzingatia maslahi yao na kuendelea kuzinyonya nchi hizo kama ilivyokuwa hapo awali. Hii ni pamoja na ukweli kwamba, katika hali na mazingira ya sasa bara la Afrika linaongeza hatua kwa hatua nafasi na sauti yake katika mlingano wa kimataifa kwa kuzingatia uwezo wake wa rasilimaliwatu na wa maliasili pamoja na akiba kubwa ya utajiri wa madini na nishati lilionao, na kuifanya Magharibi na nchi zinazoinukia kuwa na nguvu kubwa za kiuchumi zivutiwe zaidi na bara hilo. Hali hiyo imeibua ushindani unaozidi kuongezeka baina ya nchi za Magharibi na zile zinazochipukia kuwa madola mapya yenye nguvu za kiuchumi wa kuongeza na kuimarisha uwepo na ushawishi wao katika Bara la Afrika.../

 

Tags