Aug 23, 2023 02:39 UTC
  • Umoja wa Afrika (AU) waisimamishia uanachama Niger

Umoja wa Afrika (AU) umesimamisha uanachama wa Niger katika taasisi hiyo kubwa zaidi ya kibara; huo ukiwa ni muendelezo wa vikwazo na mashinikizo dhidi ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya mwezi uliopita.

Uamuzi huo ulitangazwa jana Jumanne, mwishoni mwa mkutano wa Baraza la Usalama na Amani la Umoja wa Afrika uliofanyika Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia ambapo yapo makao makuu ya AU.

Aidha AU imesema inapinga vikali uingiliaji wowote wa maajinabi ukiwemo wa kijeshi katika masuala ya ndani ya nchi za bara Afrika. Kadhalika imesema inachunguza mapendekezo ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa Niger.

Taarifa ya AU imeeleza kuwa, "Tunathamini uamuzi wa ECOWAS wa kuandaa vikosi vya kutumwa Niger, na Kamisheni ya AU itaweka kwenye mizani athari na matokeo ya uamuzi huo (wa kushambuliwa kijeshi Niger)."

Jumuiya ya ECOWAS imetishia kuchukua hatua za kijeshi kubadili hatua ya mwezi uliopita ya kupinduliwa Rais Mohamed Bazoum iwapo mazungumzo yatashindwa kufikia lengo linalokusudiwa.

Mkutano wa ECOWAS

Wakati huohuo, ECOWAS imekataa pendekezo la utawala wa kijeshi wa Niger la kufanya uchaguzi ndani ya miaka mitatu, na kuzidisha mzozo wa kisiasa ambao unaweza kusababisha uingiliaji wa kijeshi, iwapo hakuna makubaliano yataafikiwa kufuatia mapinduzi ya mwezi Julai. 

Kiongozi wa mapinduzi ya Niger ameahidi kulirudisha taifa hilo la Afrika Magharibi katika utawala wa kiraia ndani ya miaka mitatu. Jenerali Abdourahamane Tchiani alitoa tangazo hilo baada ya kukutana na wapatanishi kutoka jumuiya ya kanda ya Afrika Magharibi ECOWAS katika mji mkuu, Niamey.

Tags