Amnesty: Askari wa Eritrea walifanya jinai za kivita Tigray, Ethiopia
(last modified Tue, 05 Sep 2023 10:53:39 GMT )
Sep 05, 2023 10:53 UTC
  • Amnesty: Askari wa Eritrea walifanya jinai za kivita Tigray, Ethiopia

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema wanajeshi wa Eritrea waitifaki wa serikali ya Ethiopia walifanya jinai za kivita katika eneo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia.

Katika ripoti yake mpya, Amnesty imesema wanajeshi wa Eritrea walifanya jinai za kivita, na huenda pia jinai dhidi ya binadamu dhidi ya wakazi wa Tigray mwaka jana. Amnesty International imeeleza namna askari wa Eritrea walivyoua raia kinyume cha sheria na kuwabaka wanawake kwa miezi kadhaa baada ya kusainiwa makubaliano ya amani mwaka jana.

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limesema liliwahoji watu 49 baina ya Mei na Juni mwaka huu katika wilaya zilizoko mipakani za Mariam Shewito na Kokob Tsibah eneo la Tigray, ambao wametoa ushuhuda wa kufanyika jinai za kivita. Ushuhuda huo umeoana na uliotolewa na madaktari, maafisa wa serikali na wafanyakazi wa kijamii katika eneo hilo.

Hata hivyo Rais wa Eritrea Isaias Afwerki hivi karibuni aliyataja madai hayo ya kukiukwa haki za binadamu na wanajeshi wa Eritrea katika eneo la Tigray wakati wa vita vya miaka miwili katika eneo hilo kuwa ni njozi tupu.

Vikosi vya Tigray

Jeshi la Eritrea liliviunga mkono vikosi vya ulinzi vya Ethiopia katika vita kati ya serikali ya Addis Ababa na harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) vilivyoanza Novemba mwaka 2020. 

Vita hivyo vilimalizika kwa kusainiwa makubaliano ya amani mwezi Novemba mwaka jana; makubaliano ambayo yalitaka kuondoka vikosi vya nchi ajinabi huko Tigray. 

Hata hivyo jina la Eritrea halikuashiriwa moja kwa moja kwenye makubaliano hayo. Serikali ya Asmara inaihesabu harakati ya wapiganaji wa TPLF kuwa ni adui wake.