UN: Mauaji makubwa na uhalifu wa kivita unaendelea kufanywa Ethiopia
Wataalamu huru wa haki za binadamu walioteuliwa na Umoja wa Mataifa wamesema, uhalifu wa kivita umeendelea kufanywa bila kusitishwa nchini Ethiopia karibu mwaka mmoja baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano kufikiwa kati ya Serikali ya nchi hiyo na vikosi kutoka eneo la kaskazini la Tigray
Ripoti ya hivi karibuni iliyotolewa na tume hiyo ya kimataifa ya wataalamu wa haki za binadamu kuhusu Ethiopia imeeleza kuhusu ukatili unaofanywa na pande zote kwenye mgogoro wa nchi hiyo tangu tarehe 3 Novemba 2020 ambayo ni tarehe ya kuanza kwa vita vya kijeshi huko Tigray, ukatili huo ukiwa ni pamoja na mauaji ya watu wengi, ubakaji, njaa, uharibifu wa maskuli na vituo vya matibabu, watu kufurushwa kwa lazima na kuwekwa kizuizini kiholela.
Mwenyekiti wa tume hiyo Mohamed Chande Othman amesema machafuko hivi sasa yako karibu katika kiwango cha kitaifa na yanahusisha ripoti za ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya raia katika jimbo la Ahmar na pia ukatili unaoendelea.
Chande ameonya kuwa “hali ni mbaya katika majimbo ya Oromia, Ahmara na maeneo mengine ya nchi hiyo ikiwemo mwenendo wa ukiukaji, ukwepaji wa sheria na ongezeko la matumizi ya kijeshi zaidi kwa madai ya ulinzi na usalama na hivyo kuongeza hatari ya kufanyika ukatili na uhalifu.”
Tume hiyo ya haki za binadamu kuhusu Ethiopia imesema katika jimbo la Amhara ambako serikali ilitangaza hali ya dharura mwezi uliopita, imekuwa ikipokea ripoti za makundi ya watu hasa raia kukamatwa kiholela na angalau kulikuwa na shambulio moja la ndege zisizo na rubani au drone lililofanywa na serikali.
Pia imeelezwa kwamba maeneo mengi ya mijini yako chini ya amri ya kutotembea ovyo na kutawala kwa amri ya kijeshi bila kuwajali raia.
Tume hiyo imesema mfumo huo mara nyingi huambatana na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.../