Rais Kagame dunia ichukue hatua za kusitisha mizozo
(last modified Thu, 21 Sep 2023 03:02:39 GMT )
Sep 21, 2023 03:02 UTC
  • Rais Paul Kagame wa Rwanda
    Rais Paul Kagame wa Rwanda

Rais Paul Kagame wa Rwanda amesema, pamoja na changamoto zinazoendelea duniani ikiwa ni pamoja na athari mbaya za janga la COVID19 na mabadiliko ya tabianchi, kuna haja ya kuwa na dunia yenye amani na matumaini, na kwa msingi huo amesisitiza kuwa, “tusipoze tu joto linaloathiri tabianchi bali pia tupoze mizozo.”

Akihutubia Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA78, jijini New York, Marekani katika siku ya pili ya mkutano huo, Kagame amesema: “Mpaka sasa hakuna dalili yoyote inayotia matumaini ya kumaliza mizozo inayoendelea duniani, hatuoni hata matumaini kutoka kwa wale wenye ushawishi, kuwa mwisho unakaribia.”

Katika hotuba yake hiyo ya dakika 10, kiongozi wa Rwanda amezungumzia pia umuhimu na udharura wa kuhakikisha bara la Afrika linawakilishwa kikamilifu katika bodi zinazofanya maamuzi kuhusu masuala yajayo ambayo Afrika ina maslahi nayo.

Kwa udharura huo huo Afrika lazima ijiandae kikamilifu kuzungumza kwa lugha moja na hatimaye mfumo unaofaa zaidi lazima utoe uzito sawa kwa mahitaji na vipaumbele vya kila mtu. Hilo ndilo linalojenga ubia wa haki na usawa, na ulimwengu wa haki na amani zaidi, na hilo ndilo kila mtu anasema anataka.”

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Kuhusu mgogoro wa wahamiaji, Rais wa Rwanda amesema nchi yake ipo bega kwa bega na wahamiaji na wakimbizi.

Uamuzi huu umetokana na uzoefu wetu na kutambua kwa dhati maumivu ya kupoteza kila kitu na kutokuwa na sehemu unayoweza kuiita nyumbani. Na hii ni sehemu ya ahadi yetu ya kutomuacha mtu yeyote nyuma.” 

Kila mwaka wahamiaji na wakimbizi wanafanya safari za hatari lengo likiwa ni kusaka maisha bora na Rwanda imeahidi kuendelea kufanya kazi na wadau ukiwemo Umoja wa Mataifa na Kamishna wa Wakimbizi kusaka suluhu ya kudumu.