OCHA: Mamilioni ya Wasudan wamekuwa wakimbizi kutokana na kuendelea vita na mapigano
Sep 24, 2023 03:15 UTC
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa mamilioni ya watu wamelazimika kuyahama makazi yao na kuwa wakimbizi kutokana na kuendelea vita na mapigano kati ya Jeshi na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka, RSF nchini Sudan.
Kwa mujibu wa Al Jazeera, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imetangaza kuwa Wasudan wapatao milioni tano na laki tatu wameyahama makazi yao kutokana na mapigano yanayoendelea kati ya jeshi na vikosi vya RSF.
Kwa mujibu wa ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu, zaidi ya watu milioni moja wamevuka mipaka ya Sudan na kuingia katika nchi jirani kutokana na mapigano yanayoendelea kati ya jeshi na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka.
Mapigano ya silaha nchini Sudan yalianza Aprili 15 mwaka huu kati ya vikosi vya Jeshi na vile vya usaidizi wa haraka , chanzo kikiwa ni ugomvi wa kuwania madaraka; na juhudi za upatanishi wa kimataifa za kukomesha mapigano hayo kwa kuzileta pande hizo mbili kwenye meza ya mazungumzo hadi sasa hazijazaa matunda.
Usitishaji vita umeshatangazwa mara kadhaa nchini humo kupitia upatanishi huo wa kimataifa, lakini umekuwa ukikiukwa mara kwa mara na pande zinazopigana.
Mapigano hayo kati ya vikosi vya Jeshi na vya RSF yanaendelea katika maeneo tofauti ya Sudan, lakini yamejikita zaidi katika mji mkuu Khartoum, na hadi sasa yameshasababisha vifo vya watu wasiopungua 5,000 wengi wao wakiwa raia, na zaidi ya 12,000 kujeruhiwa.../