Sep 30, 2023 15:46 UTC

Raia wa Niger wamelishambulia lori la Ufaransa lililokuwa limebeba maji kwa ajili ya wanajeshi wa nchi hiyo walioko nchini humo kinyume cha sheria.

Raia hao wa Niger wamelishambulia lori lililokuwa likisafirisha chupa za maji kwa ajili ya wanajeshi vamizi wa Ufaransa karibu na kambi ya jeshi la Ufaransa huko Niamey, mji mkuu wa Niger, na kumwaga mzigo wake.

Raia hao wametaka wanajeshi wa Ufaransa kuondoka nchini katika nchi hiyo ya ukanda wa Sahel. Hapo awali, maelfu ya watu wa Niger walikusanyika mbele ya kambi ya jeshi la Ufaransa mjini Niamey na kutoa nara dhidi ya serikali ya Paris.

Waandamanaji hao pia walipiga nara dhidi ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS ambayo imeiwekea Niger vikwazo vya kiuchumi.

Baada ya wiki kadha za vuta nikuvute, hatimaye wiki iliyopita Ufaransa ilisalimu amri mbele ya takwa la Niger na kutangaza kwamba, balozi wa nchi hiyo nchini Niger, Sylvian Itte, atarejea Paris.

Baraza la kijeshi la Niger pia limeitaka Ufaransa kuondoa wanajeshi wake nchini humo ifikapo Septemba 3. Baraza hilo pia lilitishia kwamba vinginevyo baada ya tarehe hii, makamanda wa kijeshi wa Ufaransa watawajibika kwa matukio yoyote yatakayotokea.

Baada ya kumuondoa madarakani rais wa zamani wa nchi hiyo, Mohamed Bazoum aliyetambuliwa kuwa kibaraka wa Ufaransa, utawala wa kijeshi nchini Niger ulichukua msururu wa maamuzi dhidi ya Paris ikiwa ni pamoja na kumfukuza balozi wa Ufaransa, kufuta makubaliano ya nchi mbili, na kufunga anga ya nchi hiyo kwa ndege za Ufaransa.

Tags