Oct 04, 2023 06:49 UTC
  • Mabalozi wa kigeni wanaoishi Tunisia walaani jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel

Baadhi ya mabalozi wa nchi za kigeni wanaoishi nchini Tunisia wamelaani vikali jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kutoa taarifa ya pamoja kwa mnasaba wa kukumbuka mashambulizi ya anga ya utawala huo dhidi ya Tunisia.

Katika taarifa hiyo ya pamoja iliyotolewa kwa mnasaba kutimia miaka 38 tangu baada ya shambulio la anga la utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo la Hammam al-Shat nchini Tunisia, tarehe 1 Oktoba 1985, kundi la mabalozi wa kigeni wanaoishi Tunisia wamelaani vikali jinai hiyo ya Israel na kutangaza kuwa, mashambulizi hayo yalikiuka sheria na kanuni zote za kimataifa hususan Hati ya Umoja wa Mataifa.

Mabalozi wa nchi za kigeni nchini Tunisia sambamba na kutangaza mshikamano wao kamili na serikali na wananchi wa Tunisia na vilevile wananchi wa Palestina, wamepongeza misimamo ya serikali ya Tunis na rais wa nchi hiyo katika kuwaunga mkono wananchi wa Palestina.

Taarifa ya mabalozi hao ilisomwa na Wael al-Fahoum, balozi wa Palestina nchini Tunisia, katika eneo la tukio, wakati wa kumbukumbu ya mashahidi wa hujuma hiyo ya Israel.

Mabalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Palestina, Russia, Yemen, Venezuela, Indonesia, Cuba n.k walikuwa miongoni mwa mabalozi waliotia saini taarifa hiyo.

Shambulio la anga la utawala wa Kizayuni katika eneo la Hammam al-Shat nchini Tunisia hapo mwaka 1985 lilipelekea kuuawa shahidi na kujeruhiwa idadi kadhaa ya raia wa Tunisia na Wapalestina waliokuwa wakiishi nchini humo, na kusababisha uharibifu mkubwa katika nyumba za raia na majengo ya kibinafsi na ya umma.

Tags