Waasi wa Kituareg watangaza kudhibiti kambi nyingine ya jeshi la Mali
(last modified Thu, 05 Oct 2023 07:53:53 GMT )
Oct 05, 2023 07:53 UTC
  • Waasi wa Kituareg watangaza kudhibiti kambi nyingine ya jeshi la Mali

Wapiganaji wa Kituareg huko kaskazini mwa Mali wametangaza kuwa wameteka kambi nyingine ya jeshi la nchi hiyo na kufanya idadi ya kambi walizotwaa katika wiki kadhaa zilizopita kufikia tano.

Msemaji wa Harakati ya Azawad, Mohamed Mouloud Ramadane, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba wapiganaji wa Kituareg wameidhibiti kambi ya jeshi katika meneo la Tossa baada ya kupigana na jeshi la Mali. Hata hivyo hakukuwa na taarifa yoyote kutoka kwa jeshi la Mali kuhusu madai hayo.

Baraza Kuu la Umoja wa Azawad pia lilisema jana Jumatano katika taarifa fupi kwenye mitandao ya kijamii kwamba "limechukua udhibiti" wa kambi ya jeshi la Mali huko Tossa, katika mkoa wa Gao.

Harakati za Azawad ni muungano wa vikundi kadhaa vinavyoundwa na Watuareg, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamika kwamba wametelekezwa na serikali na wanapigania kujitawala eneo la jangwa walilolipa jina la "Azawad".

Tangu mwishoni mwa mwezi wa Agosti, eneo la kaskazini mwa Mali limeshuhudia hujuma na mashambulizi dhidi ya jeshi, katika muktadha wa ushindani wa kudhibiti eneo hilo, sanjari na kuendelea kuondoka ujumbe wa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, kujibu ombi la baraza la kijeshi linalotawala Mali.