Oct 05, 2023 13:46 UTC
  • Baraza la Kijeshi Niger: Kituo cha kijeshi cha Ufaransa kitavunjwa mwisho wa mwaka huu

Baraza la kijeshi la Niger limetangaza katika taarifa kwamba kituo cha kijeshi cha Ufaransa kilichoko katika mji mkuu Niamey, ambako ndiko waliko wanajeshi wengi wa Ufaransa kitavunjwa ifikapo mwisho wa mwaka huu wa 2023.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Sputnik, Baraza la Kijeshi la Niger limesisitiza katika taarifa hiyo iliyotolewa leo kwamba wanajeshi 400 wa Ufaransa wataondoka wiki hii katika kambi ya kijeshi ya Olam iliyoko kaskazini mwa Niamey.
 
Baraza la kijeshi la Niger lilitangaza wiki iliyopita pia kwamba ratiba ya kuondoka vikosi vya Ufaransa nchini humo inapasa itekelezwe kama ilivyoafikiwa katika makubaliano ya ratiba hiyo.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alitangaza hapo awali kwamba vikosi vya jeshi la nchi yake vitaondoka Niger ifikapo mwisho wa 2023.

 
Kufuatia mashinikizo ya Baraza la Kijeshi la Niger kutaka maafisa wa kidiplomasia na askari wa jeshi la Ufaransa waondoke nchini Niger, Macron alilazimika kumrejesha mjini Paris balozi wa nchi hiyo wa mjini Niamey, Sylvian Ite.
 
Uhusiano kati ya Niger na Ufaransa umezorota tangu Paris ilipoitangaza serikali ya kijeshi ya Niger kuwa ni utawala haramu na usio wa kisheria, na hivyo kuchochea hisia za chuki dhidi ya Ufaransa miongoni mwa wananchi wa Niger.../

 

Tags